Oktoba 25, 2016, rais wa Turkmenistan alitoa msamaha kwa wafungwa zaidi ya 1,500. Hata hivyo, Mashahidi wa Yehova wawili, Bahram Hemdemov na Mansur Masharipov, waliofungwa kwenye gereza la LBK-12 lililoko Seydi hawakupata msamaha.

Bw. Hemdemov amefungwa tangu Machi 2015 kwa sababu ya kuendesha mkutano wa dini uliofanywa kwa amani kwenye nyumba yake iliyopo jijini Turkmenabad. Mahakama ya Turkmenistan ilimhukumu kifungo cha miaka minne gerezani kwa madai ya kufanya utendaji wa dini kinyume cha sheria. Bw. Masharipov, alikamatwa Juni 2016 jijini Ashgabad kwa mashtaka ya uwongo na akahukumiwa kifungo cha mwaka mmoja gerezani. Familia zao na Mashahidi wa Yehova duniani pote wamehuzunishwa na kitendo hicho cha kutoachiliwa kwa wanaume hao wawili lakini wanatumaini kwamba wataachiliwa, msamaha mwingine utakapotolewa.