Katika maamuzi kumi yaliyofanywa karibuni, Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Kibinadamu iliagiza serikali ya Turkmenistan iheshimu mikataba yake ya kulinda haki za kibinadamu za raia wake. * Maamuzi yaliyofanywa mwaka wa 2015 na 2016, ilisema kwamba serikali inapaswa kuacha kuwaadhibu wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri na kwamba inapaswa kufuata Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa, ambao Turkmenistan imeutia sahihi.

Mashahidi Watafuta Suluhisho

Uamuzi wa Kamati hiyo unategemea malalamiko yaliyopelekwa Septemba 2012 na wanaume kumi ambao ni Mashahidi walioadhibiwa kwa kukataa kujiunga na utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri. Wanaume tisa kati yao walifungwa katika magereza yenye hali mbaya na iliripotiwa kwamba walipigwa na kuvunjiwa heshima. Pia, walikabiliana na hali mbaya ya hewa katika magereza machafu na yaliyokuwa na wafungwa wengi kupita kiasi na walikuwa katika hatari ya kuambukizwa magonjwa.

Kila uamuzi wa Kamati hiyo ulisema kwamba Turkmenistan ilikuwa imekiuka “uhuru wa mawazo, dhamiri, na ibada” wa watu wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri. Katika kisa cha wanaume tisa waliofungwa gerezani, Kamati hiyo ilisema kwamba Turkmenistan “haikuwatendea kibinadamu na iliwavunjia heshima” na kwamba ilikuwa “imewanyanyasa au kuwatendea kikatili, haikuwatendea kibinadamu na iliwavunjia heshima.”

Kamati hiyo ilisema kwamba ili kurekebisha ukiukwaji huo wa haki, serikali ya Turkmenistan inapaswa kufuta rekodi za uhalifu za Mashahidi, kuwalipa ridhaa ya kutosha, na kufikiria upya sheria yake ili kuhakikisha “inadumisha haki ya wale wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri.” Kamati hiyo pia iliagiza serikali ichunguze bila ubaguzi na kufuatilia kwa kina ripoti za kutendewa vibaya na iwafungulie mashtaka watu wote waliohusika na vitendo hivyo.

Mwaka wa 2013, wanaume wengine watano ambao ni Mashahidi walipeleka malalamiko kwenye Kamati hiyo kwa sababu waliadhibiwa kwa kukataa kujiunga na utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri. Wakili wao wanatarajia uamuzi wa malalamiko yao utatolewa hivi karibuni.

Mateso Makali Aliyokabili Navruz Nasyrlayev

Navruz Nasyrlayev

Uamuzi mmoja uliotolewa na Kamati hiyo Julai 15, 2016 ulimhusu Navruz Nasyrlayev. Alipoitwa kwa mara ya kwanza ajiunge na utumishi wa kijeshi mnamo Aprili 2009 akiwa na umri wa miaka 18, aliwaeleza wenye mamlaka kwamba dhamiri yake haimruhusu kujiunga na utumishi wa kijeshi. Hata hivyo, alieleza kwamba alikuwa tayari kufanya utumishi wa badala wa kiraia. Baadaye, alihukumiwa miaka miwili katika gereza la LBK-12 lililoko Seydi kwa madai ya kukwepa utumishi wa kijeshi. Akiwa huko, mara kwa mara alifungwa kwenye chumba cha upweke, na alipigwa sana na walinzi waliokuwa wameziba nyuso zao.

Mnamo Januari 2012, mwezi mmoja baada ya kuachiliwa huru, Bw. Nasyrlayev aliitwa tena ajiunge na utumishi wa kijeshi. Kwa mara nyingine alieleza kwamba yuko tayari kufanya utumishi wa badala wa kiraia lakini akahukumiwa kwa mashtaka kama ya awali na kufungwa miaka mingine miwili kwenye “gereza lenye sheria na ulinzi mkali” ambako hali inaelezwa kwamba ilikuwa ya “kusikitisha sana.” Kama ilivyokuwa mara ya kwanza alipokuwa gerezani; alipigwa na walinzi wa gereza na kulazimishwa kufanya kazi zenye kumshushia heshima.

Washiriki wa familia ya Bw. Nasyrlayev waliteseka pia. Muda mfupi baada ya Kamati hiyo kutuma malalamiko yake kwa serikali ya Turkmenistan ili iyatekeleze, maofisa wa polisi walivamia nyumba ya familia yake iliyoko Dashoguz na kuwatesa sana washiriki wa familia yake pamoja na wageni wao—hasa ili kulipiza kisasi kwa sababu ya malalamiko hayo ya Kamati.

Ingawa Bw. Nasyrlayev aliachiliwa kutoka gerezani mnamo Mei 2014, bado anaendelea kuteseka kwa sababu ya madhara ya kifungo chake. Kamati hiyo ilitambua kwamba aliteseka kwa sababu ya mateso makali na kwamba kuhukumiwa kwake mara mbili na kufungwa “kwa msingi uleule, yaani, kwa sababu ya dhamiri.” Kamati hiyo ilihitimisha kwa kusema hivi: “ Kukataa kwa [Bw. Nasyrlayev] kujiunga na utumishi wa kijeshi kulitegemea imani yake ya kidini . . . , na hukumu na vifungo alivyokabili ni ukiukwaji wa uhuru wake wa mawazo, dhamiri, na ibada.”

Je, Turkmenistan Itarekebisha Jinsi Inavyowatendea Mashahidi wa Yehova?

Katika ripoti yake ya awali ya mwaka wa 2012 ya haki za binadamu nchini Turkmenistan, Kamati hiyo iliisihi serikali “isiwakamate watu wote wanaokataa kujiunga na utumishi wa kijeshi kwa msingi wa dhamiri na kuwaachilia wale ambao imewahukumu vifungo gerezani.” Serikali ya Turkmenistan ilitekeleza kwa sehemu kwa kumwachilia huru Shahidi wa mwisho kutoka gerezani mnamo Februari 2015 ambaye alifungwa kwa kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri. Tangu wakati huo, hakuna Shahidi ambaye amehukumiwa kwenda gerezani kwa kukataa kujiunga na utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri.

Hata hivyo, bado serikali ya Turkmenistan inakiuka mikataba ya kimataifa ya kulinda haki za kibinadamu kwa kuwakamata na kuwaadhibu wanaokataa kujiunga na utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri.

  • Katika visa kadhaa, serikali ya Turkmenistan imewafunga wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri kifungo cha nje katika kambi za kurekebisha tabia. Tangu mwishoni mwa mwaka wa 2014, mahakama pia zimewaamuru Mashahidi wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri walipe asilimia 20 ya mshahara wao kwenye bajeti ya Nchi kwa kipindi cha mwaka mmoja hadi miwili. Kwa sasa, kuna Mashahidi wa Yehova wawili waliofungwa kwenye kituo cha kurekebisha tabia.

  • Katika visa vingine, maofisa wamewashinikiza sana wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri ili kuwalazimisha kuvunja imani wanayoshikilia kwa unyoofu.

Artur Yangibayev

Kwa mfano, Juni 16, 2016, mkuu wa polisi na wawakilishi wawili wa Kitengo cha Kijeshi walienda kwenye nyumba ya Artur Yangibayev, Shahidi ambaye alikuwa ametuma ombi la utumishi wa badala wa kiraia. Maofisa hao walimpeleka kwenye ofisi ya mwendesha mashtaka, ambapo walimtendea kwa njia iliyomfanya awe na mkazo mkubwa wa kiakili hivi kwamba akalazimika kuandika barua ya kubatilisha ombi lake la utumishi wa badala wa kiraia. Baadaye, Bw. Yangibayev alilalamika kwa sababu ya kushinikizwa, na baada ya kuwekwa mahabusu kwa majuma matatu, aliachiliwa lakini alitolewa hukumu ya miaka miwili lakini haijatekelezwa. *

Ukiukwaji Mwingine wa Haki za Binadamu Ambao Haujasuluhishwa

Zaidi ya kuwatesa wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri, Turkmenistan pia inazuia utendaji wa kidini na kuwaadhibu wanaoshiriki. Ripoti ya Januari 2017 ya Kamati ya Umoja wa Mataifa Dhidi ya Mateso iliisihi serikali ya Turkmenistan “ihakikishe kwamba uchunguzi unafanywa bila ubaguzi . . . kuhusu madai ya kwamba Shahidi wa Yehova anayeitwa Bahram Hemdemov aliteswa alipokuwa mahabusu, mnamo, Mei 2015 [na] kuhusu kukamatwa kwa Shahidi wa Yehova aitwaye Mansur Masharipov, kupigwa sana, na kupelekwa na kufungwa katika kituo cha kuwatibu watu walioathiriwa na dawa za kulevya mnamo Julai 2014.” Bw. Masharipov tayari ameachiliwa baada ya kutumikia kifungo chake cha mwaka mmoja gerezani. Bw. Hemdemov, alihukumiwa kwa madai ya uwongo kwamba alishiriki utendaji wa kidini kinyume cha sheria, na Bw. Masharipov, alifungwa kwa mashtaka ya uwongo kwa sababu ya utendaji wake wa kidini. Wote wawili hawana hatia.

Mashahidi wa Yehova nchini Turkmenistan wanatumaini kwamba hivi karibuni serikali itachukua hatua kusuluhisha mambo hayo ili kuwe na uhuru wa ibada na dhamiri. Kwa kufanya hivyo, itaonyesha kwamba inawaheshimu wanaume wanaochukua msimamo kwa sababu ya dhamiri zao na itaonyesha wazi kwamba inajitahidi kurekebisha rekodi zake kuhusiana na suala la haki za binadamu.

^ fu. 2 Sheria za kimataifa zinatambua kwamba kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri ni haki ya msingi ya kibinadamu, na nchi nyingi zinatekeleza haki hiyo kupitia sheria zao. Hata hivyo, Turkmenistan—pamoja na Azerbaijan, Eritrea, Singapore, Korea Kusini, na Uturuki—si kwamba zinakataa tu kutambua haki hii bali pia zinaendelea kuwakamata Mashahidi wa Yehova wanaokataa kujiunga na utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri.

^ fu. 18 Hukumu inatolewa lakini inakosa kutekelezwa kwa muda au hukumu nyingine inatolewa badala ya ile inayomnyima mtu uhuru. Bw. Yangibayev anafuatwa na polisi kwa ukawaida na hajatumikia kifungo gerezani.