Hamia kwenye habari

Aibek Salayev, Matkarim Aminov, na Bahram Shamuradov walikuwa miongoni mwa Mashahidi waliopewa msamaha wa Rais

NOVEMBA 13, 2014
TURKMENISTAN

Turkmenistan Yawaachilia Mashahidi wa Yehova Waliofungwa kwa Sababu ya Imani Yao

Turkmenistan Yawaachilia Mashahidi wa Yehova Waliofungwa kwa Sababu ya Imani Yao

Kwa tukio lisilotazamiwa, Rais Gurbanguly Berdimuhamedov alitoa msamaha wa kuachiliwa huru kwa Mashahidi wa Yehova nane, waliokuwa wamefungwa nchini Turkmenistan kwa sababu ya imani yao. Walikuwa miongoni mwa wafungwa wengine walioachiliwa huru Oktoba 22, 2014. Sita kati ya Mashahidi hao walifungwa kwa kukataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri na wawili kwa mashtaka ya uwongo kuhusu shughuli za kidini.

Merdan Amanov na Pavel Paymov

Wanaume Mashahidi wenye umri kati ya miaka 18 na 23, waliokataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri, walifungwa kwenye kambi ya Seydi Labor Colony iliyo katika jangwa la Turkmenistan. Merdan Amanov, Pavel Paymov, Suhrab Rahmanberdyyev, na Amirlan Tolkachev walifungwa kwenye kambi ya kawaida. Matkarim Aminov na Dovran Matyakubov (hawapo kwenye picha) walifungwa kwenye kambi yenye ulinzi mkali zaidi, kwa kuwa walihukumiwa kama “watu waliorudia makosa.” Walipokuwa gerezani, wanaume hao walitendewa kwa ukatili na kuishi kwenye hali mbaya sana.

Aibek Salayev mwenye umri wa miaka 35 na Bahram Shamuradov aliye na umri wa miaka 42, Mashahidi wawili waliofungwa kwa mashtaka ya uwongo, walifungwa pia kwenye kambi ya Seydi. Wote wawili walikuwa wakitumikia vifungo vya miaka minne kwa sababu ya imani na shughuli zao za kidini. Waliteseka sana kwa sababu ya kutendewa vibaya walipokuwa chini ya kizuizi na kufungwa isivyo haki kwa msingi wa ushahidi wa uwongo.

Amirlan Tolkachev

Ni Shahidi mmoja tu, Ruslan Narkuliev, ambaye bado yupo gerezani nchini Turkmenistan. Alihukumiwa kwa kukataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri majuma machache tu kabla ya kutolewa kwa msamaha wa Rais, na huenda wenye mamlaka katika Ofisi ya Rais hawakuwa na habari kumhusu msamaha ulipotangazwa. Wawakilishi wake wa kisheria wanashirikiana na wenye mamlaka nchini Turkmenistan ili aachiliwe huru.

Rais Berdimuhamedov alifanya uamuzi unaostahili pongezi kwa kuwaachilia huru wanaume hao nane waaminifu. Wanaothamini uhuru wa kidini wanatumaini kwamba uamuzi huo ni mwanzo tu wa mabadiliko nchini Turkmenistan, badiliko litakalowaruhusu Mashahidi wa Yehova waishi kulingana na dhamiri zao bila hofu ya kuteswa au kufungwa.