Hamia kwenye habari

Mashahidi wa Yehova

Chagua lugha Kiswahili

MEI 16, 2017
TURKMENISTAN

Mansur Masharipov Aachiliwa Huru Kutoka Gereza la Turkmenistan

Mansur Masharipov Aachiliwa Huru Kutoka Gereza la Turkmenistan

Mei 12, 2017, wenye mamlaka nchini Turkmenistan walimwachilia huru Mansur Masharipov kutoka gerezani. Anafurahi sana kwamba amerudi kwa familia yake baada kutumikia kifungo cha karibu mwaka mmoja gerezani.

Bw. Masharipov alikataa kujiunga na utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri. Mnamo Mei 2004, Mahakama ya Dashoguz ilimhukumu kifungo cha miezi 18 katika kambi ya kazi ngumu ya Seydi, gereza lenye sifa mbaya ya uonevu, kuwanyima wafungwa mahitaji yao, na magonjwa. Alikabiliwa na matatizo ya afya, ingawa aliachiliwa mapema kwa sababu msamaha maalumu aliopata mnamo Mei 2005. Mwezi Julai 2014, polisi walivamia nyumba yake, wakapekua, na kuchukua machapisho yake ya kidini. Alipokuwa katika kituo cha polisi, aliendelea kupigwa na polisi mara nyingi na kutishwa, na kisha akapelekwa kwenye kituo cha kuwasaidia waraibu wa dawa za kulevya—walimpeleka hapo si kwa sababu walihangaikia afya yake, bali ili kumpa dawa za kulevya. Dawa hizo zilimfanya awe mgonjwa na kupooza. Kwa sababu ya kuhofia uhai wake, Bw. Masharipov alifaulu kutoroka na akaendelea kujificha mpaka alipokamatwa Juni 30, 2016.

Mashahidi wa Yehova wanafurahia kuachiliwa kwa Bw. Masharipov. Hata hivyo, wanahangaishwa na matendo ya kikatili ambayo wenye mamlaka wa Turkmenistan wanatumia kuwazuia Mashahidi kufanya utendaji wao wa kidini kwa uhuru. Pia, Mashahidi wanaendelea kujitahidi ili Bahram Hemdemov aachiliwe huru. Sasa ameanza mwaka wa tatu tangu afungwe katika gereza la kambi ya kazi ngumu la Seydi kwa sababu ya kukisimamia kikundi cha Mashahidi kilichokuwa kikifanya ibada kwa amani nyumbani kwake.