Bibi Rahmanova na familia yake

Saa mbili asubuhi, Septemba 2, 2014, Bibi Rahmanova aliachiliwa huru kutoka gerezani, lakini mashtaka yake hayakufutiliwa. Mapema siku hiyo, majaji wa Mahakama ya Mkoa ya Dashoguz walisikiliza rufani yake. Ingawa hawakumwondolea Bibi mashtaka ya uwongo, walibadili adhabu aliyopewa ya kifungo cha miaka minne gerezani wakaamua atumikie kifungo chenye masharti nje ya gereza * na wakaamuru aachiliwe haraka kutoka gerezani. Uamuzi wa mahakama ulisema kwamba majaji walizingatia mambo kama vile Bibi ni mwanamke na ana mtoto wa miaka minne na kwamba hana rekodi yoyote ya uhalifu.

Bibi alikata rufani kupinga uamuzi uliotolewa Agosti 18 ambapo alihukumiwa kutokana na mashtaka ya uwongo ya “kumshambulia polisi” na “kufanya fujo.” Bibi na mume wake, Vepa, walikamatwa na polisi Julai 5 kwenye kituo cha treni huko Dashoguz baada ya kupokea mizigo yao, ambayo ilitia ndani machapisho kadhaa ya kidini. Vepa alifutiwa mashtaka baadaye. Hata hivyo, Bibi alipelekwa gerezani Agosti 8. Akiwa huko, Bibi alipigwa vibaya sana.

Kuangazia Ukosefu wa Haki Nchini Turkmenistan

Wakili wa Bibi anaona kuwa kuachiliwa kwake kumechangiwa kwa sehemu na malalamiko kutoka mataifa mengine yaliyopinga ukosefu wa haki aliotendewa.

Kisa chake si cha pekee kwa Mashahidi wa Yehova nchini Turkmenistan. Haki za msingi za kibinadamu za Mashahidi nchini humo huvunjwa mara nyingi sana. Mashahidi wanane wanatumikia vifungo gerezani kwa sababu ya imani yao—sita wamehukumiwa kwa kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri na wawili kwa mashtaka ya uwongo. Wanaishi katika mazingira magumu sana na wanatendewa vibaya.

Inafurahisha kwamba majaji wa Mahakama ya Mkoa ya Dashoguz wamemwachilia Bibi, lakini wameshindwa kurekebisha ukosefu wa haki. Wale wanaothamini haki ya kila mwanadamu ya kuheshimiwa wanatumaini kwamba wenye mamlaka nchini Turkmenistan watazingatia mambo yote na kutumia viwango vya kimataifa vya haki za kibinadamu ili kuruhusu uhuru wa ibada nchini humo.

^ fu. 2 Mahakama ya mkoa ilibadili adhabu aliyopewa ya kifungo cha miaka minne gerezani na kuamua atumikie kifungo chenye masharti kinachotia ndani kuzuiliwa mambo fulani kwa miaka mitatu. Ndani ya kipindi hicho, anapaswa kujiendesha vizuri na hapaswi kuondoka au kuhama mji anaoishi bila kupata ruhusa kutoka kwa wenye mamlaka.