Katika maamuzi yake manne yaliyotolewa karibuni, Kamati ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa ilikata kauli kwamba serikali ya Turkmenistan inawaadhibu isivyo haki wanaume wanaokataa kujiunga na utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri. * Pia kama hiyo ilisema kwamba hali mbaya za gerezani zilikiuka haki nyingine zilizo katika Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa (ICCPR). Maamuzi ya Kamati hiyo yanaiagiza nchi ya Turkmenistan iache kukiuka sheria ya kimataifa ya haki za kibinadamu.

Azimio Moja Latokeza Hukumu Mbili

Machi 2015, Kamati ilipitia kesi ya Zafar Abdullayev, raia wa Turkmenistan ambaye ni Shahidi wa Yehova. Wenye mamlaka walimhukumu mara mbili kwa kukataa kujiunga na utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri. Kesi ya Bw. Abdullayev ilisikilizwa Aprili 2009, naye alisema wazi mbele ya Mahakama ya Jiji la Dashoguz kwamba kwa sababu ya kujifunza Biblia, ameazimia kutotumia silaha, kutojifunza vita, na kutounga mkono shughuli za kijeshi. Pia alieleza kwamba yuko tayari kabisa kufanya utumishi wa badala wa kiraia. Hata hivyo, mahakama ilimhukumu kifungo cha masharti cha miezi 24 * kwa “kukataa kujiandikisha jeshini.”

Miezi 11 baada ya kumaliza kifungo chake, Bw. Abdullayev alifikishwa tena mbele ya mahakama hiyo ili kujibu tena shtaka la kutotii amri nyingine ya kujiunga na utumishi wa kijeshi. Alikuwa na msimamo uleule. Mahakama ikamhukumu kifungo cha miezi 24 gerezani.

Kamati ilikata kauli kwamba kumwadhibu Bw. Abdullayev mara mbili kwa kukataa utumishi wa kijeshi kulikiuka azimio la kwamba “hakuna mtu anayepaswa kushtakiwa au kuadhibiwa tena kwa kosa ambalo tayari alihukumiwa.” (Ona ICCPR Kifungu cha 14, fungu la 7.) Pia, Kamati ilikata kauli kwamba mashtaka yote mawili yalikuwa kinyume cha “haki ya kuwa na uhuru wa kufikiri, wa dhamiri, na wa kidini.”—Ona ICCPR Kifungu 18, fungu la 1.

“Haki ya kukataa kujiunga na utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri inahusiana na haki ya kuwa na uhuru wa kufikiri, wa dhamiri, na wa kidini. Haki hiyo inamruhusu mtu yeyote kukataa kujiunga na utumishi wa kijeshi ikiwa jambo hilo linapingana na dini au imani yake.”—Kamati ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa

Maisha ya Gerezani

Mara tu Bw. Abdullayev alipowasili kwenye gereza la Seydi LBK-12, wasimamizi wa gereza walimtenga peke yake kwa siku kumi. Alipokuwa huko, walinzi wa gereza alimpiga na kumtendea mambo mengine mabaya sana.

Kati ya mwaka 2010 na 2011, Mashahidi wengine watatu, Ahmet Hudaybergenov, Mahmud Hudaybergenov, na Sunnet Japparow, pia walifungwa kwa kukataa kujiunga na utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri. Wanaume hao walieleza kwamba walipitia mateso yaleyale walipowasili katika gereza la Seydi na walipigwa tena na tena kwa muda wote waliokuwa wamefungwa gerezani.

Zafar Abdullayev

Mashahidi hao wanne walieleza mambo yanayofanana kuhusu hali ya gerezani. Wafungwa 40 hivi waliwekwa kwenye vyumba vichafu na ambavyo havikuwa hata na mahali pa kuketi isipokuwa sakafu ya saruji. Wakati wa usiku, walikuwa na blanketi chafu tu ambazo hazikutosha wafungwa.

Mnamo Oktoba 2015, Kamati ilitoa maamuzi yake kuhusu kesi za Messrs. Hudaybergenov, Hudaybergenov, na Japparow. Kama tu ilivyotoa uamuzi kuhusu Bw. Abdullayev, Kamati hiyo iliamua kwamba mambo waliyotendewa wanaume hao na mwenye mamlaka yalikuwa kinyume cha azimio la kwamba “hakuna mtu atakayeteswa, kuadhibiwa, au kutendewa kwa ukatili, kinyama, au kwa njia yenye kumshushia hadhi.” (Ona ICCPR Kifungu cha 7.) Pia Kamati hiyo ilikata kauli kwamba kuishi kwenye hali hizo mbaya sana kulikiuka haki ya wafungwa kutendewa “kwa utu na kwa heshima inayomstahili mwanadamu.”—Ona ICCPR Kifungu cha 10.

Wajibu wa Kurekebisha Tatizo la Kukiuka Haki za Kibinadamu

Kamati ya Haki ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa inatambua kwamba sheria ya Turkmenistan inawataka raia wanaume kujiandikisha jeshini. Hata hivyo, Kamati hiyo inasisitiza kwamba Mkataba wa ICCPR unamruhusu mtu kukataa kujiunga na jeshi ikiwa sababu zake zinategemea imani. Kitendo cha kuwashtaki na kuwaadhibu kwa sababu ya misingi hiyo ni kinyume cha haki ya msingi ya kuwa na “uhuru wa kufikiri, wa dhamiri, na wa kidini.”

Maamuzi ya kamati yanaiwajibisha serikali ya Turkmenistan ipitishe “sheria inayounga mkono haki ya kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri,” kuchunguza kikamili madai ya “vitendo vya kikatili, kinyama au vyenye kushushia heshima,” na kuwashtaki wote wanaowatendea wengine vibaya. Pia Kamati iliitaka serikali kuwalipa fidia wanaume hao waliotendewa kinyume cha haki, kutia ndani malipo sahihi na kufuta rekodi zao za uhalifu kuhusu kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri.

Maendeleo Zaidi Yanahitajika

Serikali ya Turkmenistan imefanya maendeleo katika kushughulika na wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri. Februari 2015, ilimwachilia huru Shahidi wa mwisho aliyekuwa amefungwa kwa sababu ya kutumia haki hiyo ya kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri.

Hata hivyo, nchi ya Turkmenistan bado imewafunga watu wengine kwa sababu ya dhamiri. Bahram Hemdemov, mwanamume mwenye familia na ambaye ni Shahidi wa Yehova, bado yuko gerezani. Wenye mamlaka walimkamata mwanamume huyo polisi walipovamia mkutano wa ibada uliokuwa ukifanywa ndani ya nyumba yake Machi 14, 2015. Baadaye mahakama ilimhukumu kifungo cha miaka minne gerezani kwa sababu ya utendaji wa kidini. Sasa Bw. Hemdemov anaendelea kukabiliana na minyanyaso na kuishi kwenye hali mbaya sana katika kambi ya mateso ya Seydi.

Mashahidi wa Yehova na raia wote wa Turkmenistan wanatazamia kwa hamu kuona serikali ikitimiza matakwa ya mikataba ya kimataifa ya kuheshimu haki za binadamu, kutia ndani haki ya msingi ya kuwa na uhuru wa kufikiri, wa dhamiri, na wa kidini.

^ fu. 2 Ona Mawasiliano ya Kamati ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa: Na. 2218/2012, Zafar Abdullayev v Turkmenistan, 25 Machi 2015 (CCPR/C/113/D/2218/2012); Na. 2221/2012, Mahmud Hudaybergenov v Turkmenistan, 29 Oktoba 2015 (CCPR/C/115/D/2221/2012); Na. 2222/2012, Ahmet Hudaybergenov v Turkmenistan, 29 Oktoba 2015 (CCPR/C/115/D/2222/2012); Na. 2223/2012, Sunnet Japparow v Turkmenistan, 29 Oktoba 2015 (CCPR/C/115/D/2223/2012).

^ fu. 4 Kifungo cha masharti kinamzuia mtu kufanya mambo fulani badala ya kufungwa gerezani na hivyo kunyimwa uhuru kabisa. Alipohukumiwa mara ya kwanza, Bw. Abdullayev alikubali kwamba polisi wafuatilie utendaji wake kwa ukawaida, kwa hiyo hakufungwa gerezani.