Hamia kwenye habari

Kerven Kakabayev—alihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja gereza kwa kukataa kujiunga na utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri

MACHI 28, 2018
TURKMENISTAN

Turkmenistan Imepuuza Haki ya Uhuru wa Dhamiri

Januari 2018, Arslan Begenjov na Kerven Kakabayev walihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja gerezani kwa kosa la kuepuka utumishi wa kijeshi. Vijana hao wawili ni Mashahidi wa Yehova na walikuwa wamekataa kuandikishwa jeshini kutokana imani yao ya kidini. Ingawa walikuwa tayari kufanya utumishi wa badala wa kiraia, serikali ya Turkmenistan bado haitambui haki ya msingi ya watu wanaokataa kujiunga na utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri na haitoi utumishi wowote wa badala wa kiraia.

Kukamatwa, Kuhukumiwa, na Kufungwa

Wenye mamlaka walimkamata Bw. Begenjov Januari 2 na kumweka kwenye jengo la muda la mahabusu mpaka wakati wa kusikilizwa kwa kesi yake. Januari 17, mahakama ilimpata na hatia ya kuepuka utumishi wa kijeshi na ilimhukumu kifungo cha mwaka mmoja gerezani. Bw. Begenjov amekata rufaa kupinga hukumu hiyo isiyo ya haki.

Mnamo Januari, Bw. Kakabayev pia alikamatwa na Januari 29 alihukumiwa isivyo haki kifungo cha mwaka mmoja gerezani. Kesi yake iliposikilizwa, mahakama haikumruhusu awasilishe maamuzi ya Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Kibinadamu ambayo yanaunga mkono kesi yake. Kwa kusikitisha, mahakama haitaweza kusikiliza rufaa ya Bw. Kakabayev. Maofisa wa gereza walikataa kuwasilisha hati za rufaa ambazo mawakili wake walikuwa wametayarisha kwa ajili yake. Matokeo ni kwamba mawakili hao walishindwa kutia sahihi hati hizo kwa muda wa siku kumi tangu hukumu itolewe kama sheria inavyosema.

Bw. Kakabayev ameadhibiwa kwa mara ya pili sasa kwa kukataa kujiunga na utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri. Desemba 2014, wenye mamlaka walimpa adhabu ya kutumikia utumishi wa kubadili tabia kwa miaka miwili, yaani, alipaswa kulipa asilimia 20 ya mshahara wake kwenye bajeti ya serikali kwa kipindi hicho chote.

“Imeendelea Kutotambua Haki za Wale Wanaokataa Utumishi wa Kijeshi kwa Sababu ya Dhamiri”

Serikali ya Turkmenistan inadai kuheshimu uhuru wa msingi wa raia zake. Hata hivyo, inakataa kutambua haki ya wale wanaokataa kujiunga na utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri licha ya kuelezwa ifuate viwango vya kimataifa.

Mwaka wa 2015 na 2016, Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Kibinadamu ilitoa uamuzi wake dhidi ya Turkmenistan kutokana na malalamiko kumi yaliyopelekwa huko na Mashahidi waliokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri. Katika maamuzi hayo, Kamati iliikosoa Turkmenistan kwa kuwatesa na kuwafunga Mashahidi kwa kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri. Mnamo Aprili 2017 Kamati hiyo ilirudia tena kueleza hangaiko lake kuhusu Turkmenistan “[kuendelea] kutotambua haki za wale wanaokataa kujiunga na utumishi wa lazima wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri na kuendelea kuwatesa na kuwafunga Mashahidi wa Yehova kwa kukataa kujiunga na utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri.” Imeiagiza Turkmenistan itoe utumishi wa badala wa kiraia, ikomeshe mateso kwa wale wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri, na iwaachilie wale wote ambao wamefungwa gerezani kwa kukataa kujiunga na utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri.

Kwa miaka kadhaa sasa, serikali imefanya mabadiliko kadhaa ya jinsi inavyowatendea wale wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri. Tangu Desemba 2014, badala ya kuwafunga Mashahidi wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri, ilikuwa ama inawakata asilimia 20 ya mshahara wao kwa kipindi cha mwaka mmoja hadi miwili kama adhabu (kama hali aliyokuwa amekabili Bw. Kakabayev mwaka 2014) au katika visa vingine, wanapewa hukumu yenye masharti. * Mnamo Februari 2015 ilimwachilia kutoka gerezani Shahidi wa mwisho aliyehukumiwa kwa kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri. Kwa kusikitisha, katika kesi za hivi karibuni za Bw. Begenjov na Bw. Kakabayev, serikali ya Turkmenistan imerudia matendo yake ya zamani badala ya kuboresha hali ili kuonyesha inatambua haki za wale wanaokataa kujiunga na utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri.

Mashahidi Wanafungwa si kwa Kukataa tu Kujiunga na Jeshi kwa Sababu ya Dhamiri

Zaidi ya kuwafunga Bw. Begenjov na Bw. Kakabayev, bado wenye mamlaka wameendelea kumfunga Bahram Hemdemov gerezani kwa sababu ya kutekeleza haki yake ya kuabudu. Akiwa Shahidi wa Yehova, alikamatwa na kufungwa kwa sababu ya kufanya mkutano wa kidini katika nyumba yake iliyoko jijini Turkmenabad. Yeye ni baba ya watoto wanne na ingawa rais wa Turkmenistan ametoa msamaha mara kadhaa kwa wafungwa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, Bw. Hemdemov ameendelea kuwa gerezani tangu mwaka wa 2015. Serikali imewaachilia maelfu ya wafungwa lakini imekataa maombi ya kumwachilia huru Bw. Hemdemov.

Mashahidi wa Yehova wanatamani waabudu wenzao nchini Turkmenistan wasiendelee kukabili hali hiyo. Wanatumaini kwamba karibuni Turkmenistan itaheshimu haki ya uhuru wa ibada na dhamiri na itarekebisha ukosefu wa haki uliopo.

^ fu. 10 Hukumu yenye masharti inamfanya mtu awe katika aina fulani ya kifungo cha nje chenye masharti badala ya kutumikia gerezani.