Mashahidi wa Yehova wameanza utendaji wao nchini Turkmenistan mwishoni mwa miaka ya 1980. Muda mfupi baada ya kupata uhuru wake kutoka Muungano wa Sovieti Oktoba 1991, serikali ilianza kuwekea dini vikwazo vikali.

Mashahidi wa Yehova hawatambuliki kisheria nchini Turkmenistan. Baadhi ya Mashahidi wamepigwa vibaya sana, wamewekwa vizuizini, nyumba zao zimepekuliwa, wamefungwa gerezani, na wametozwa faini kwa sababu tu ya kuhubiri. Nyakati nyingine, wamefungwa gerezani kutokana na mashtaka ya uwongo yaliyotolewa na polisi. Kwa kuwa Turkmenistan haina utumishi badala kwa ajili ya raia ambao hawataki kujiunga na jeshi, vijana Mashahidi wananyanyaswa na kuadhibiwa kutokana na msimamo wa kutojiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri. Mashahidi wa Yehova wamepeleka malalamiko yao katika Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Kibinadamu na mashirika mengine ya kimataifa.

Mnamo Oktoba 2014, Rais wa Turkmenistan alitoa msamaha wa kuachiliwa huru kwa Mashahidi nane waliofungwa gerezani isivyo haki. Mashahidi wametoa shukrani zao kwa serikali ya Turkmenistan kwa hatua hiyo nzuri. Wanatumaini kwamba serikali itafanya mengi zaidi ili kuwapa haki yao ya kuabudu.