Hamia kwenye habari

Hamia kwenye menyu ya pili

Mashahidi wa Yehova

Kiswahili

NOVEMBA 24, 2015
TURKMENISTAN

Turkmenistan Imemhukumu Bahram Hemdemov Kifungo cha Miaka Minne Gerezani Kwa Sababu ya Utendaji wa Dini

Turkmenistan Imemhukumu Bahram Hemdemov Kifungo cha Miaka Minne Gerezani Kwa Sababu ya Utendaji wa Dini

Mei 19, 2015, mahakama ya Turkmenistan ilimhukumu Shahidi wa Yehova aitwaye Bahram Hemdemov, mwenye umri wa miaka 52 kifungo cha miaka minne gerezani. Polisi walimkamata Bw. Hemdemov miezi miwili kabla ya hukumu hiyo kwa sababu ya kufanya mkutano wa dini nyumbani kwake jijini Turkmenabad. Kwa sasa amepelekwa kwenye kambi ya kazi ngumu katika mji wa Seydi.

Kuvamiwa kwa Mkutano wa Dini

Machi 14, 2015, Polisi walivamia mkutano wa dini uliokuwa ukifanywa katika nyumba ya Bw. Hemdemov. Polisi waliwashambulia, waliwatesa na kuwafungulia mashtaka wahudhuriaji wote 38 kwa madai ya kufanya utendaji wa dini kinyume cha sheria. Walimfunga Bw. Hemdemov, pia, walimhoji na kumpiga mara nyingi. Wenye mamlaka walimnyang’anya mali zake kama vile gari, kompyuta na pesa.

Baadaye Mahakama ya Wilaya ya Serdarabad iliwatoza faini Mashahidi 30 na kuwahukumu nane kati yao kifungo cha siku 15 gerezani. Mwana wa Bw. Hemdemov aitwaye Serdar, alifungwa mara mbili gerezani na kila mara alikaa gerezani kwa siku 15. Wakati akitumikia kifungo hicho wenye mamlaka walimtenga na wengine, wakamhoji, wakampiga sana na kumtesa. Shahidi mwingine aliyefungwa mara mbili, siku 15 kwa kila kipindi, ni Emirdzhan Dzhumnazarov ambaye pia alipigwa sana na kuteswa.

Mei 19, 2015, Hakimu Gochmurad Charyev wa Mahakama ya Mkoa ya Lebap alimhukumu Bahram Hemdemov miaka minne gerezani kwa mashtaka ya uwongo ya “kuchochea chuki ya dini.” Juni 10, 2015 alihamishwa kutoka Turkmenabad hadi kambi ya kazi ngumu ya Seydi.

Msimamizi wa gereza alikataa kumruhusu mtu yeyote kumtembelea Bw. Hemdemov gerezani—kutia ndani ndugu wa karibu—mpaka muda wa kukata rufaa ulipopita. Hivyo, askari huyo alimzuia Bw. Hemdemov au mtu yeyote kukata rufaa ya kupinga hukumu. Akiwa gerezani, maofisa walimshinikiza akiri shutuma za uwongo za kukiuka sheria, walimlazimisha kufanya kazi ngumu, na walimpiga sana ili kulipiza kisasi kwa sababu ya mashtaka ambayo mke wake alifungua mahakamani kwa niaba yake.

Gulzira Hemdemova, mke wa Bahram, alikata rufaa kwenye Mahakama Kuu ya Turkmenistan. Ingawa hakukuwa na ushahidi wowote wa vitendo vya uhalifu, mwenyekiti msaidizi wa Mahakama Kuu alikataa rufaa hiyo. Mapema mwezi Agosti, wakili wa Bw. Hemdemov alifungua jalada la kukata rufaa. Hata hivyo, Agosti 25, 2015, Mahakama Kuu ilikataa rufaa hiyo kwa madai ya kwamba Bw. Hemdemov “anaeneza imani ya dini ya Mashahidi wa Yehova.”

“Mamlaka nchini Turkmenistan imeongeza vitendo vya ukosefu wa haki. . . . Inastaajabisha, kuona hata Mahakama Kuu ya Turkmenistan imepuuza ukosefu wa haki aliofanyiwa Bahram Hemdemov.”—Philip Brumley, wakili.

Kampeni za Unyanyasaji Jijini Turkmenabad

Kufikia mwishoni mwa mwaka 2014, mamlaka nchini Turkmenistan zilionyesha dalili za kuheshimu utendaji wa dini ya Mashahidi wa Yehova. Septemba 2014, serikali ilimweka huru Bibi Rahmanova aliyekamatwa Agosti 2014 na kufungwa kwa sababu ya mashtaka ya uwongo. Mashahidi nane waliofungwa kwa sababu ya kushiriki utendaji wa imani yao walipata msamaha wa rais na kuwekwa huru Oktoba 2014. Licha ya maendeleo hayo mazuri, baadhi ya wenye mamlaka wameendeleza ukiukwaji wa haki ya kuabudu kwa kuwakamata, kuwaweka vizuizini, na kuwanyanyasa baadhi ya Mashahidi wa Yehova jijini Turkmenabad.

Februari 6, 2015, polisi waliwakamata Mashahidi wa Yehova wanne—Viktor Yarygin, Rustam Nazarov, Charygeldy Dzhumaev, na Jamilya Adylova. Waliwashtaki kwa kosa la “kuanzisha fujo ndogo” kwa sababu walikuwa na machapisho ya dini. Wakala wa Wizara ya Usalama wa Taifa aliwapiga Mashahidi watatu, kutia ndani Bi. Adylova. Maofisa walimpiga sana Bw. Dzhumaev hivi kwamba alipoteza fahamu mara kadhaa. Mahakama ya Jiji la Turkmenabad ilimtoza faini Bw. Yarygin, ikamhukumu Bw. Nazarov kwenda gerezani kwa siku 30, na iliwahukumu Bw. Dzhumaev na Bi. Adylova kwenda gerezani siku 45 kila mmoja *. Mashahidi hao wanne wamepeleka malalamiko yao kwenye Ofisi ya Rais na Mwendesha Mashtaka Mkuu wa serikali jijini Ashgabad.

Majuma mawili baadaye, polisi walivamia nyumba ya Zeynep Husaynova ili kutafuta machapisho ya dini “yasiyo halali.” Walimnyag’anya machapisho yake ya dini, na kutishia kumstaki na kumfunga gerezani kwa siku 15.

Shahidi mwingine, Dovlet Kandymov, alishtakiwa kwa sababu ya kufanya utendaji wa dini usio halali na akafungwa mara tatu mfululizo na kila kipindi alitumikia siku 15. Akiwa chini ya ulinzi, maofisa walimpiga mara nyingi kwa sababu alikataa kutoa ushahidi dhidi ya mwabudu mwenzake Bahram Hemdemov.

Je, Turkmenistan Itaheshimu Mkataba Wake wa Uhuru wa Ibada?

Wenye mamlaka jijini Turkmenabad hawakuwasumbua Mashahidi wa Yehova Tangu wakati wa majira ya kuchipua ya mwaka 2015. Hata hivyo, bado Bahram Hemdemov yupo gerezani kwa sababu ya imani yake ya dini.

Bahram na mke wake Gulzira, pamoja na mtoto wao

Shughuli za dini zinazochochea amani, kutia ndani shughuli za Mashahidi wa Yehova zinapaswa kulindwa kisheria nchini Turkmenistan. Katiba ya nchi inampa mtu haki ya “kushiriki ibada akiwa peke yake au pamoja na watu wengine” na “haki ya kuwa na imani yoyote na kuwa huru kueleza maoni yake kuhusu imani hiyo kwa watu wengine.” Zaidi ya hayo, Turkmenistan imesaini Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa, ambao unataka watu wawe na uhuru wa mawazo, dhamiri, na ibada.

Philip Brumley, wakili wa Mashahidi wa Yehova, alisema hivi:

Mamlaka nchini Turkmenistan imeongeza vitendo vya ukosefu wa haki katika kila idara. Maofisa wa polisi jijini Turkmenabad walifanya makosa ya jinai na kikatili walipovamia mikutano ya dini inayofanywa kwa amani. Mahakama jijini Turkmenabad haichukui hatua yoyote dhidi ya matendo hayo yasiyo ya haki. Inastaajabisha, kuona hata Mahakama Kuu ya Turkmenistan imepuuza ukosefu wa haki aliofanyiwa Bahram Hemdemov.

Kwa heshima Mashahidi wa Yehova wanaiomba serikali ya Turkmenistan iwasajili kisheria, iwaruhusu kuabudu kwa uhuru, na imalize uonevu kama ule uliotokea jijini Turkmenabad mapema mwaka huu. Tunaiomba serikali imweke huru Bw. Bahram Hemdemov ili aungane na familia yake.

Mashahidi wa Yehova wanatambua kwa unyoofu kwamba wakati uliopita serikali ya Turkmenistan iliwaweka huru wafungwa ili kufidia ukosefu wa haki uliotendeka. Vivyo hivyo, ingefaa serikali ihakikishe kwamba Bahram Hemdemov anawekwa huru mapema iwezekanavyo na kuruhusu uhuru mkubwa zaidi wa ibada.

^ fu. 11 Kwa mujibu wa sheria za Turkmenistan, kiwango cha juu cha hukumu kwa “fujo ndogo” ni kufungwa siku 15 gerezani. Hata hivyo, mahakama ilimhukumu Bw. Dzhumaev na Bi. Adylova mara tatu na kila mara walihukumiwa siku 15 gerezani.