Hamia kwenye habari

TAJIKISTAN

Wamefungwa kwa Sababu ya Imani Yao​—Tajikistan

Wamefungwa kwa Sababu ya Imani Yao​—Tajikistan

Januari na Februari 2019, maofisa wa Idara ya Kudhibiti Uhalifu Mkubwa (DOCC) waliwahoji Mashahidi 24 wa Yehova, jijini Khujand na katika miji ya karibu, nchini Tajikistan. Septemba 10, 2019, Mahakama ya Jiji la Khujand ilimhukumu Shamil Khakimov mwenye umri wa miaka 68, kifungo cha miaka saba na nusu gerezani kwa mashtaka ya uwongo ya ‘kuchochea chuki ya kidini.’ * Hukumu ndefu ya Bw. Khakimov imepunguzwa na hivyo amepangiwa kuachiliwa Mei 16, 2023.

Shamil Khakimov

Bw. Khakimov ni mjane na afya yake ni mbaya kwa kuwa ana tatizo la shinikizo la damu na matatizo mengine makubwa ya afya. Mwanaye wa pekee, alikufa mnamo Septemba 2021. Machi 2021, Bw Khakimov alihamishiwa kwenye zahanati iliyo gerezani ambako alipata nafuu kidogo lakini bado hajapata matibabu yoyote ya kitaalamu. Mashahidi wenzake wanamwandalia chakula na dawa zinazohitajika. Jitihada zinafanywa kumpata daktari nchini Tajikistan ambaye atakuwa tayari kumtibu.

Jitihada za Kumsaidia Bw. Khakimov’s Aachiliwe

Mapema mwaka wa 2021, Nury Turkel, Mkuu wa Tume ya Uhuru wa Ibada wa Kimataifa ya Marekani, alimtambua rasmi Bw. Khakimov kuwa Mfungwa wa Kidini kwa Sababu ya Dhamiri. Hivyo basi akatuma ombi Bw Khakimov aachiliwe huru mara moja. Februari 25, 2022, miaka mitatu baada ya Bw. Khakimov kukamatwa, Bw. Turkel alisema hivi:

 • “Kwa miaka mitatu, Khakimov amelazimishwa kuteseka gerezani kwa sababu ya kushiriki utendaji wa kidini kwa amani. Mamlaka nchini Tajikistan zimekataa kuandaa matibabu yanayofaa kwa ajili ya Khakimov aliye na vidonda miguuni; pia walikataa kumruhusu ahudhurie mazishi ya mwanaye, mtu pekee aliyeruhusiwa kumtembelea gerezani; isitoshe wamemzuia kushiriki imani yake na wengine au kusoma Biblia hadharani. . . . Ni lazima mmwachilie huru ili kukomesha mateso ya kimwili, kiakili, na kiroho anayoendelea kukabiliana nayo.”

Machi 15, 2021, mawakili wa Bw. Khakimov walituma maombi ya haraka kwa Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Kibinadamu (CCPR) ili iingilie kati upesi. CCPR ilichukua hatua haraka na ikakubali maombi hayo baada ya siku nne tu. Kamati hiyo iliiomba nchi ya Tajikistan “ihakikishe, bila kuchelewa, kwamba [Bw. Khakimov] anapewa matibabu anayostahili kwenye kituo maalumu cha afya kulingana na mahitaji yake, na kwamba [Bw. Khakimov] aachiliwe na kupewa kifungo cha badala wakati ambapo kesi yake inasubiri kusikilizwa na [CCPR].” Bw. Khakimov amewasilisha maombi ya rufaa kwa kutegemea uamuzi wa CCPR; hata hivyo, mahakama nchini humo, kutia ndani Mahakama Kuu, zimekataa maombi hayo.

Novemba 2021, mawakili wa Bw. Khakimov waliwasilisha ombi kwenye Mahakama ya Jiji la Khujand la kumwachilia kwa muda ili apate matibabu anayohitaji, lakini ombi hilo lilikataliwa bila hata kufikiriwa. Hivi karibuni, mawakili wake waliwasilisha hoja kwa wasimamizi wa gereza wakiomba aachiliwe kwa sababu ya matatizo yake ya kiafya. Pia, waliomba kifungo chake kipunguzwe. Hata hivyo, kifungo chake hakijapunguzwa na amebaki gerezani.

Mfuatano wa Matukio

 1. Juni 17, 2022

  Bw. Khakimov peke yake ndiye aliyefungwa kwa sababu ya imani yake nchini Tajikistan.

 2. Septemba 21, 2021

  Baada ya msamaha kutolewa nchi nzima Bw. Norov aliachiliwa kutoka gerezani baada ya kufungwa miezi 11 ya kifungo chake cha miaka 3.5.

 3. Septemba 9, 2021

  Hukumu ya Bw. Khakimov inapunguzwa tena kwa mwaka mmoja. Sasa anapaswa kuachiliwa Mei 16, 2023.

 4. Januari 7, 2021

  Bw. Norov ahukumiwa kifungo cha miaka mitatu na nusu katika kambi ya kazi ngumu kwa kuwa alikataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri.

 5. Novemba 1, 2020

  Jovidon Bobojonov apewa msamaha wa rais na kuachiliwa huru baada ya kutumikia miezi tisa ya kifungo chake cha miaka miwili.

 6. Oktoba 1, 2020

  Rustamjon Norov awekwa kizuizini kwa nguvu kwa kuwa alikataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri, licha ya kwamba aliomba kufanya utumishi wa badala wa kiraia.

 7. Julai 4, 2020

  Uongozi wa gereza la YaS 3/5 ulimtaarifu Bw. Khakimov kwamba hukumu yake imepunguzwa kwa miaka miwili, miezi mitatu na siku kumi. Hivyo, anatarajia kuachiliwa huru Mei 16, 2024.

 8. Aprili 2, 2020

  Bw. Bobojonov ahukumiwa kifungo cha miaka miwili katika gereza la wahalifu.

 9. Januari 28, 2020

  Bw. Bobojonov ahukumiwa kwa kosa la kutoroka utumishi wa kijeshi.

 10. Oktoba 9, 2019

  Mahakama ya Rufaa yakubaliana na uamuzi uliofanywa na Mahakama ya jiji la Khujand katika kesi ya Bw. Khakimov.

 11. Oktoba 4, 2019

  Jovidon Bobojonov akamatwa kwa nguvu kwa sababu ya kukataa kujiandikisha jeshini.

 12. Septemba 10, 2019

  Bw. Khakimov ahukumiwa kwa mashtaka ya uwongo ya ‘kuchochea chuki ya kidini’ na hivyo afungwa kwa miaka saba na nusu gerezani.

 13. Agosti 5, 2019

  Kesi ya Bw. Khakimov inaanza kusikilizwa katika Mahakama ya jiji la Khujand. Anakaa gerezani kesi yake inapoendelea.

 14. Juni 25, 2019

  Mahakama ya jiji la Khujand yamwongezea Bw. Khakimov muda wa kubaki mahabusu mpaka Julai 26, 2019.

 15. Mei 31, 2019

  Mahakama ya Mkoa wa Sughd yakubaliana na uamuzi wa kumwongezea Bw. Khakimov muda wa kubaki mahabusu.

 16. Mei 24, 2019

  Mahakama ya jiji la Khujand yamwongezea Bw. Khakimov muda wa kubaki mahabusu mpaka Juni 26, 2019.

 17. Aprili 29, 2019

  Mahakama ya Mkoa wa Sughd yakubaliana na uamuzi wa kumwongezea Bw. Khakimov muda wa kubaki mahabusu.

 18. Aprili 23, 2019

  Mahakama ya jiji la Khujand yamwongezea Bw. Khakimov muda wa kubaki mahabusu mpaka Mei 26, 2019.

 19. Machi 12, 2019

  Mahakama ya Mkoa wa Sughd yaunga mkono uamuzi wa Mahakama ya Jiji la Khujand wa kumweka Bw. Khakimov mahabusu kwa miezi miwili.

 20. Februari 28, 2019

  Mahakama ya Jiji la Khujand yamweka Bw. Khakimov mahabusu kwa miezi miwili.

 21. Februari 26, 2019

  Bw. Khakimov akamatwa kwa mashtaka ya uwongo ya ‘kuchochea chuki ya kidini.’

 22. Februari 1, 2019

  Shamil Khakimov aitwa kwenye kituo cha polisi, afanyiwa upekuzi, na kuhojiwa. Baada ya kuwa kizuizini kwa saa nane, maofisa wa polisi walimpeleka Bw. Khakimov nyumbani, ambako walichukua vitu vyake vya kibinafsi na pasipoti.

 23. Mwishoni mwa Januari–Mwanzoni mwa Februari 2019

  Maofisa wa DOCC katika jiji la Khujand wapekua nyumba saba na kuwahoji Mashahidi 24, baadhi yao kwa saa 14.

^ Sheria 189 kifungu cha (2) cha Sheria ya Uhalifu ya Jamhuri ya Tajikistan.