Januari 11, 2018, Kamati ya Washauri wa Mambo ya Kijeshi katika Mahakama Kuu ya Tajikistan ilikataa rufaa ya Daniil Islamov ya kutaka afutiwe mashtaka na aachiliwe kutoka gerezani. Bila kueleza sababu, mahakimu waliamua kufanya kesi katika vyumba vya faragha bila kumpa Bw. Islamov nafasi ya kujitetea nao wakaunga mkono mashtaka ya uwongo kwamba ana msimamo wa kuepuka utumishi wa kijeshi. Amewekwa kizuizini katika jengo lililoko Kurgan-tyube hadi muda wake wa kifungo utakapokamilika mnamo Aprili 2018.

Anaadhibiwa kwa Sababu Serikali Imeshindwa Kutoa Utumishi wa Badala wa Kiraia

Bw. Islamov aliripoti kwa ofisi ya kuandikisha wanajeshi alipoitwa mnamo Aprili 2017 na aliwaeleza maofisa hao kuwa yeye ni Shahidi wa Yehova na hawezi kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri yake. Hata hivyo, aliwaeleza maofisa hao kwamba yuko tayari kufanya utumishi wa badala wa kiraia. Maofisa hao walikataa ombi hilo na wakampeleka kwa lazima kwenye kambi ya jeshi. Alipokuwa kizuizini, maofisa walijaribu mara kwa mara kumlazimisha Bw. Islamov ale kiapo cha jeshi na avae sare za jeshi, lakini alikataa. Julai 31, 2017, alishtakiwa kwa kuepuka utumishi wa kijeshi, na aliendelea kuwa katika kambi ya jeshi hadi kesi yake iliposikilizwa Oktoba 13, 2017.

Akiwa kifungoni, Bw. Islamov alipeleka malalamiko yake kwa wenye mamlaka wa Tajikistan ili kupinga kifungo alichohukumiwa ambacho si cha haki. Wakili wa jeshi alisema kwamba Bw. Islamov hawezi kuomba utumishi wa badala wa kiraia kwa sababu hakuna sheria iliyopitishwa ya kuidhinisha utumishi huo na hakuna utumishi wowote wa badala kwa ajili ya wale wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri. Ingawa kuna maandishi yanayoonyesha kwamba raia wa Tajikistan wanaweza kufanya utumishi wa badala wa kiraia, serikali haijaanza kutekeleza programu hiyo. Kamati ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (CCPR) imeisihi mara mbili Tajikistan itambue haki za wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri na itoe utumishi wa badala wa kiraia, lakini serikali imeshindwa kutekeleza jambo hilo. *

Tajikistan Ina Hatia ya Kumfunga Mtu Isivyo Haki

Kwa kuwa kifungo cha Bw. Islamov kinakiuka sheria za kimataifa, wakili wake amepeleka mashtaka kwenye Kamati ya Umoja wa Mataifa Inayoshughulikia Vifungo Visivyo vya Haki (WGAD). Oktoba 5, 2017, WGAD ilitoa maoni yake kwa njia ya maandishi, ikieleza kwamba haki ya wanaokataa kujiunga na jeshi inatambulika katika sheria za kimataifa na kwamba serikali inatambua hilo kwa sababu ilipata mapendekezo ya Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Kibinadamu. Kamati ya WGAD ilihitimisha maoni yake kwa kueleza kuwa Tajikistan ina hatia ya kumfunga isivyo haki Bw. Islamov kwa sababu serikali imemnyima haki zake na hakuna msingi wa kisheria wa kumfunga. Zaidi ya hilo maelezo hayo yalisema kwamba Bw. Islamov “amebaguliwa kwa misingi ya imani yake ya kidini.” Kamati hiyo (WGAD) iliisihi serikali “ichukue hatua haraka ili kurekebisha hali anayokabili Bw. Islamov” na “imwachilie Bw. Islamov mara moja.”

Amekataa Kujiunga na Jeshi kwa sababu ya Dhamiri— Wala si “Mwanajeshi Aliyeandikishwa”

Licha ya mwongozo wa wazi wa WGAD na sheria ya Tajikistan, Oktoba 13, 2017, mahakama ya jeshi ilimshtaki Bw. Islamov kwa madai ya kwamba alikuwa “mwanajeshi aliyeandikishwa ambaye alitoroka ili kuepuka kutimiza majukumu yake ya kijeshi” na ikamhukumu kifungo cha miezi sita gerezani. Katika hukumu hiyo, si kwamba mahakama ilipuuza tu uamuzi wa WGAD na suala kubwa zaidi la utumishi wa badala wa kiraia bali pia ilieleza kimakosa kwamba Bw. Islamov ni “mwanajeshi aliyeandikishwa” na ni “mfanyakazi wa jeshi.” Yeye si mwanajeshi wala mfanyakazi wa jeshi kwa sababu hajawahi kuandikishwa jeshini, hajawahi kula kiapo cha jeshi, wala kuvaa sare za jeshi.

Mawakili wa Bw. Islamov walikata rufaa kwenye Kamati ya Washauri wa Mambo ya Kijeshi katika Mahakama Kuu ya Tajikistan si ili tu Bw. Islamov aachiliwe mapema bali pia afutiwe mashtaka hayo ya uwongo ya kutoroka utumishi wa jeshi. Rufaa hiyo imekazia uangalifu uamuzi uliotolewa na WGAD na imeomba serikali itekeleze maagizo ya uamuzi huo bila kukawia.

Kwa kuwa Januari 11 Mahakama Kuu iliunga mkono hukumu ya Bw. Islamov, mawakili wake wamekata rufaa katika Mahakama hiyo ili kuomba kesi hiyo ichunguzwe upya. Ikiwa Mahakama hiyo itakataa rufaa hii, Bw. Islamov hatakuwa tena na sehemu ya kupata msaada wa kisheria nchini Tajikistan na huenda akapeleka malalamiko yake katika Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Kibinadamu.

“Haki ya mtu kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri inatambuliwa na sheria za kimataifa . . . Bila shaka . . . Bw. Islamov analaumiwa kwa sababu ya imani yake ya kidini akiwa Shahidi wa Yehova.”—Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Kibinadamu, Maoni yaliyokubaliwa na Kamati ya Umoja wa Mataifa Inayoshughulikia Vifungo Visivyo vya Haki katika sehemu ya 79: Na. 43/2017, Tajikistan, U.N. Doc. A/HRC/WGAD/2017/43 (Agosti 21, 2017), uku. 34.

Msimamo Imara wa Mashahidi wa Yehova

Gregory Allen, Wakili Msaidizi wa Mashahidi wa Yehova, alieleza jinsi alivyovunjwa moyo na Tajikistan ilivyomtendea Bw. Islamov. Alisema hivi: “Daniil ni mtu wa dini na anapenda amani ambaye amekataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri yake. Tangu Vita vya Pili vya Ulimwengu, makumi ya maelfu ya Mashahidi wamefungwa gerezani kwa sababu ya msimamo wao wa kutounga mkono upande wowote katika vita. Kama waabudu wenzake, Daniil hawezi kupuuza dhamiri yake mbele za Mungu kwa ajili ya faida za kibinafsi. Vijana kama Daniil hawapaswi kupewa adhabu.”

Mashahidi wa Yehova wanatumaini wenye mamlaka nchini Tajikistan watatekeleza uamuzi wa WGAD na wataheshimu haki za Mashahidi vijana ambao—kama Daniil Islamov—wanakataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri kwa kuwa wana imani yenye nguvu.

[MAELEZO YA CHINI]

^ fu. 5 Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Kibinadamu, Uchunguzi wa Mwisho: Tajikistan, UN Doc. CCPR/CO/84/TJK, (Julai 18, 2005), uku. 20; Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Kibinadamu, Uchunguzi wa Mwisho, UN Doc. CCPR/C/TJK/CO/2, (Agosti 22, 2013), uku. 21.