Mahakama kuu nchini Sri Lanka zimekubaliana kupitia tena kesi kadhaa zinazohusiana na vurugu waliyofanyiwa Mashahidi wa Yehova na watu wenye msimamo mkali wa kidini. Tangu mwaka 2013, Mashahidi wamevumilia visa vya kushambuliwa na umati wenye hasira, kutishwa, na kutukanwa vinavyochochewa na watawa wa Kibudha wenye msimamo mkali. Uhalifu huo na chuki ya kidini inaendelea kwa sababu polisi hawajachukua hatua ya kuwalinda Mashahidi au dini nyingine ndogo, hivyo kuwachochea watu wenye msimamo mkali wa kidini kuendeleza vitendo hivyo.

Mambo Yaliyofanya Mahakama Kuu Kuingilia Kati

Machi 1, 2014, huko Talawa (Mkoa wa Kaskazini ya Kati), wanawake wawili ambao ni Mashahidi wa Yehova walikuwa wakizungumza na wengine kuhusu mafundisho ya dini yao—jambo ambalo ni halali nchini Sri Lanka. Watawa wawili wa Kibudha na polisi wawili waliwasingizia kuwa “wanawalazimisha watu kubadili imani.” Polisi waliwakamata wanawake hao na kuwapeleka kituoni ambapo watawa na polisi waliwatukana kwa saa nyingi. Polisi hawakuwashtaki wanawake hao kwa kosa lolote lakini waliwaweka mahabusu usiku mzima.

Katika kisa kingine kilichotokea Oktoba 29, 2014, huko Walasmulla (Mkoa wa Kusini), polisi waliwakamata wanawake wanne (wanaoonyeshwa kwenye picha) na kuwafunga usiku kucha pamoja na wahalifu waliohukumiwa. Ingawa hawakupata madhara yoyote mwilini, walitukanwa muda wote waliokuwa hapo.

Katika visa vyote hivyo, Mashahidi waliwashtaki maofisa na kufungua kesi ya kukiukwa kwa haki za msingi katika Mahakama Kuu ya Sri Lanka. Mahakama kuu imeona kwamba madai hayo yana msingi na imekubali kusikiliza kesi hizo. Wanawake waliohusika katika kisa cha Talawa walisema hivi: “Tunafurahi kwamba Mahakama Kuu imekubali kusikiliza jambo hili. Imefanya tuanze kuamini tena mfumo wa sheria wa Sri Lanka.” Kesi ya awali iliyoendeshwa mnamo Mei 29, 2015, Jaji Sisira de Abrew alisema kwamba Mashahidi “ni watu wenye fadhili” na pia machapisho ya kidini wanayosambaza “hayapingi dini ya Budha.” Kesi hizo zimepangwa kusikilizwa baadaye mwaka huu.

Mahakama ya Rufaa Kuangalia Tena Hali ya Polisi Kutochukua Hatua

Katika jiji kuu la Colombo, Mashahidi wa Yehova wamefungua kesi katika Mahakama ya Rufaa wakitaja matukio 11 ambayo polisi hawakuchukua hatua. Katika kisa kimoja, mtawa wa Budha alimpiga kikatili Niroshan Silva na kisha akampeleka kwa nguvu kituo cha polisi ili akamshtaki. Hata hivyo, badala ya kumlinda Bw. Silva, polisi walimpiga vibaya sana.

Bw. Silva alisema, “Hatuombi tutendewe kwa njia ya pekee nchini Sri Lanka, ila tu haki itendeke katika kutetea haki ya msingi ya uhuru wa ibada wa watu wote.” Mahakama alikubali kusikiliza kesi hiyo.

Maendeleo ya Sasa

Sri Lanka imekubali kwamba kuna chuki ya kidini na imeahidi “kuongeza jitihada za kutetea uhuru wa ibada.” Mashahidi wa Yehova wanaona tamko hilo la kukiri kuwa maendeleo.

Bw. J. C. Weliamuna, wakili mkuu wa haki za msingi ambaye anawatetea Mashahidi, alisema hivi: “Sri Lanka imekuwa na dini nyingi kwa miaka mingi, na dini zote hizo zilikuwa zikishirikiana kwa amani hadi hivi karibuni. Baadhi ya dini zimeharibu ushirikiano huo kwa kuwatisha na kuwatendea jeuri Mashahidi wa Yehova na vikundi vingine vidogo vya dini, na hivyo kuvunja haki za kikatiba za Mashahidi. Wenye mamlaka hawapaswi kusikiliza mashtaka ya uwongo badala yake wanapaswa kufanya uchunguzi wa kutosha.”

Mashahidi wanatumaini kwamba mahakama zitalinda haki ya msingi ya kuendesha shughuli za dini yao kwa amani. Kwa sasa wanategemea serikali kutumia sheria zilizopo na kutetea uhuru wa msingi ambao unahakikishwa na katiba ya nchi.