Nchi ya Singapore huwafunga gerezani Mashahidi wa Yehova vijana kwa kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri. Ingawa Sheria ya Utumishi wa Kitaifa ya Singapore ya mwaka wa 1967 inawaruhusu watu kutojiunga na jeshi kwa sababu za kiafya au sababu nyingine, hairuhusu kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya imani. Kwa kuwa serikali ya Singapore inawalazimisha watu kutumikia jeshini na haitambui haki za watu wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri, Mashahidi hutumikia vifungo viwili vyenye urefu wa jumla ya miezi 39 gerezani.

Shahidi mwanamume anapofikisha umri wa miaka 18, sheria inamlazimisha kujiunga na jeshi. Akikataa, anazuiliwa kwenye kambi ya kijeshi kwa miezi 15. Mwishoni mwa kipindi hicho, anaachiliwa huru na kisha kuamrishwa avae sare za kijeshi na kuzoezwa kuwa mwanajeshi. Akikataa tena, anazuiliwa mara ya pili kwa miezi 24 chini ya sheria za kijeshi.

Singapore Imekataa Kutii Maagizo ya Umoja wa Mataifa

Umoja wa Mataifa sikuzote imeyahimiza mataifa wanachama “kutambua kwamba kukataa kujiunga na jeshi ni mojawapo ya njia ambazo mtu huonyesha kwamba ana haki ya uhuru wa kufikiri, dhamiri, na dini, na ambazo hutambuliwa na Azimio la Watu Wote la Haki za Kibinadamu.” Ingawa nchi ya Singapore imekuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa tangu 1965, imesema kwamba haikubaliani na Umoja wa Mataifa kuhusiana na suala hilo. Tarehe 24 Aprili, mwaka wa 2002, ofisa mmoja wa serikali ya Singapore aliiandikia barua Tume ya Haki za Kibinadamu ya UM. Barua hiyo ilisema kwamba “matendo au imani ya mtu inapohitilafiana [na haki ya ulinzi wa taifa], haki ya serikali ya kudumisha usalama wa taifa lazima itangulizwe.” Bila kueleza sababu hususa, ofisa huyo aliandika hivi: “Hatutambui kwamba mataifa yote yanapaswa kuheshimu haki ya kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri.”

Mfululizo wa Matukio

 1. Juni 14, 2017

  Jumla ya Mashahidi wa Yehova tisa wako gerezani kwa kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri.

 2. Novemba 2013

  Jumla ya Mashahidi 18 wamezuiliwa kwa kukataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri.

 3. Aprili 24, 2002

  Ofisa wa serikali anakiri kwamba Singapore haitambui haki ya kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri.

 4. Februari 1995

  Kuongezeka kwa ukandamizaji na kukamatwa kwa raia wa Singapore ambao ni Mashahidi wa Yehova.

 5. Agosti 8, 1994

  Mahakama Kuu ya Singapore yafutilia mbali rufaa ambayo Mashahidi walikata.

 6. Januari 12, 1972

  Serikali ya Singapore yafutilia mbali kusajiliwa kisheria kwa Mashahidi wa Yehova.