Hamia kwenye habari

Hamia kwenye menyu ya pili

Mashahidi wa Yehova

Kiswahili

Wanafunzi Mashahidi ambao mwanzoni walinyimwa ripoti zao za shule kwa sababu ya kukataa kulipa kodi za kanisa

JUNI 14, 2016
RWANDA

Serikali ya Rwanda Yadhibiti Ubaguzi wa Kidini Shuleni

Serikali ya Rwanda Yadhibiti Ubaguzi wa Kidini Shuleni

Serikali ya Rwanda ilichukua hatua ya kuondoa ubaguzi wa kidini shuleni kwa kutoa agizo kwamba imani za kidini za wanafunzi zinapaswa kuheshimiwa. Agizo hilo ni habari njema kwa wanafunzi ambao dhamiri zao haziwaruhusu kujihusisha katika shughuli fulani zinazofanywa shuleni.

Asilimia kubwa ya shule nchini Rwanda kwa kiasi fulani zinamilikiwa na serikali lakini uongozi wa shule hizo upo chini ya mashirika ya kidini. Kila mtu anaweza kuandikishwa katika shule hizo, hivyo shule hizo zina wanafunzi ambao ni washiriki wa dini mbalimbali. Hata hivyo, viongozi fulani wa shule hizo wanawalazimisha wanafunzi wajihusishe na utendaji wa kidini au wa kizalendo au walipe kodi za kanisa. Wanawaadhibu wanafunzi ambao imani yao ya kidini haiwaruhusu kufanya mambo hayo. Waziri wa serikali anayesimamia elimu ya shule za msingi na za sekondari alifafanua maoni ya baadhi ya viongozi hao wa shule hivi: “Wanafunzi wetu hawaruhusiwi kuabudu kwa njia inayopingana na imani yetu.”

Agizo la Serikali Latetea Uhuru wa Dhamiri

Viongozi wa serikali waliingilia kati na kutatua tatizo hilo wakiwa na agizo la rais lenye sheria mpya zilizokusudiwa kuondoa ubaguzi wa kidini shuleni. Kipengele cha 12 cha Agizo la serikali Na. 290/03, kinaeleza kwamba kila shule inapaswa kuheshimu uhuru wa kuabudu wa wanafunzi na kuwaruhusu kusali kulingana na imani yao ikiwa dini au kanisa lao limesajiliwa kisheria na ikiwa kufanya hivyo hakuvurugi masomo yao. Agizo hilo lilichapishwa kwenye Gazeti Rasmi la Serikali Desemba 14, 2015.

Kila shule itaheshimu uhuru wa ibada wa wanafunzi.—Agizo Na. 290/03, Kipengele cha 12

Kitendo hicho cha serikali kinaunga mkono uamuzi wa Mahakama ya Kati ya Karongi, uliohusu wanafunzi Mashahidi waliofukuzwa shule mnamo Mei 2014. Wasimamizi wa shule hiyo hawakuheshimu haki ya wanafunzi hao ya kukataa kushiriki katika ibada ya dini iliyotolewa shuleni. Mahakama iliona kuwa wanafunzi hao hawana hatia yoyote na wakaruhusiwa kuendelea na masomo yao.

Katika kesi nyingine, mwalimu mkuu wa shule moja kwenye Wilaya ya Ngororero alikataa kuwapa wanafunzi 30 ripoti zao za shule kwa kuwa walikataa kulipa kodi ya kanisa (ambayo si sehemu ya ada). Baada ya wazazi wa wanafunzi hao kulalamika kwa mkurugenzi wa elimu wa wilaya hiyo, mwalimu huyo aliwapa wanafunzi hao wote ripoti zao mwishoni mwa mwaka.

Wanafunzi Mashahidi Wafaidika

Chantal Uwimbabazi, Shahidi ambaye alikuwa mwanafunzi wa shule moja katika Wilaya ya Ngororero, alifukuzwa shule kwa sababu ya kukataa kuhudhuria Misa ya Kikatoliki iliyoongozwa shuleni. Alidhihakiwa na wanafunzi wenzake na watu wengine hivi kwamba akashindwa kuendelea na masomo yake kwa mwaka mmoja. Hatimaye aliandikishwa katika shule nyingine iliyo mbali zaidi na nyumbani na yenye gharama ya juu zaidi, jambo lililosababisha changamoto kubwa kwa mama yake ambaye ni mjane na mwenye kipato kidogo. Chantal alifurahi kusikia kuhusu sheria hiyo mpya. Alisema hivi. “Ninafikiri kwamba wanafunzi wengine wanaosoma katika shule zinazoendeshwa na mashirika ya kidini watafurahia masomo yao bila ukiukwaji wa haki zao.

Sheria hiyo mpya inapatana na Katiba ya Rwanda, inayotoa uhuru wa dini na haki ya kupata elimu. Wanafunzi ambao ni Mashahidi wa Yehova na wazazi wao wanatarajia kwa hamu kuona mwisho wa vitendo vya ubaguzi wa kidini. Wanaishukuru sana serikali kwa hatua ilizochukua ili kulinda uhuru wa ibada wa wanafunzi.