Mashahidi wa Yehova wameanza utendaji wao nchini Rwanda tangu mwaka wa 1970. Waliomba kusajiliwa kisheria mwaka wa 1992, na kufikia mwaka wa 2002, serikali ilikubali usajili huo. Mashahidi wanajulikana sana kwa sababu ya msimamo wa kutoshiriki katika siasa na kwa ujumla wana uhuru wa ibada. Hawakushiriki kwa njia yoyote katika mauaji yenye kutisha wakati wa mauaji ya halaiki ya mwaka wa 1994, hata baadhi yao walihatarisha maisha yao ili kuokoa wengine. Hata hivyo, baadhi ya watu wanawabagua Mashahidi kwa sababu ya kuendelea kudumisha msimamo wao wa kutoshiriki katika siasa.

Baadhi ya wakuu wa shule wamewafukuza watoto wa Mashahidi kwa sababu ya kukataa kushiriki katika sherehe za kizalendo na kidini shuleni. * Kwa kuongezea, serikali imeweka sheria kwa walimu kushiriki katika semina zinazohusisha mazoezi ya kijeshi na kuimba nyimbo ya taifa. Kwa sababu hiyo, mamia ya walimu ambao ni Mashahidi wamepoteza kazi. Katika mwaka wa 2010, serikali ya Rwanda ilitaka watumishi wote wa umma walishiriki katika sherehe za kula kiapo zilizohusisha bendera ya taifa. Hivyo, watumishi wa serikali ambao ni Mashahidi wa Yehova, walipoteza kazi zao.

Ingawa kuna changamoto hizo, Mashahidi wa Yehova nchini Rwanda wanashukuru sana kwamba wana uhuru wa ibada. Wanatumaini kwamba hatimaye, wakuu wa serikali ya Rwanda watatambua kwamba kutoshiriki kwao katika siasa si tishio kwa serikali.

^ fu. 3 Mashahidi wa Yehova wanaona kushiriki katika sherehe za kizalendo kuwa ibada na kuvunja amri ya Mungu inayotutaka tumwabudu yeye tu. Ingawa hawashiriki katika sherehe hizo, wanaheshimu maamuzi ya wale walioamua kushiriki.