Serikali ya Nagorno-Karabakh inawafunga gerezani Mashahidi wa Yehova wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri. Serikali hiyo haitambui haki ya watu wanaokataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri na haina mpango wa utumishi wa badala wa kiraia. Hivyo, Mashahidi vijana wanaotimia umri wa kuingia jeshini wanafungwa gerezani wanapokataa kupigana na wanadamu wenzao kwa sababu ya imani yao ya kidini.

Maombi ya Kufanya Utumishi wa Badala wa Kiraia Yakataliwa

Januari 29, 2014, Shahidi wa Yehova anayeitwa Artur Avanesyan, aliagizwa na Kitengo cha Kijeshi cha Jiji la Askeran aripoti kwa ajili ya utumishi wa kijeshi. Siku iliyofuata, Bw. Avanesyan aliwasilisha maombi ya kufanya utumishi wa badala wa kiraia katika ofisi za Kitengo cha Kijeshi cha Nagorno-Karabakh. Bila kukawia, wakili wake alikutana na wenye mamlaka katika serikali ya Nagorno-Karabakh na wa Armenia, na kusaidia katika maombi yake ya utumishi wa badala wa kiraia nchini Armenia.

Akitarajia kwamba maombi yake yangekubaliwa, Bw. Avanesyan alihamia nchi ya Armenia, na Februari 13, 2014, alijaza ombi kwenye Kitengo cha Kijeshi mjini Masis, Jamhuri ya Armenia, la kufanya utumishi wa badala wa kiraia. Alitarajia kuitwa mbele ya baraza la Armenia linaloshughulikia utumishi wa badala wa kiraia, badala yake, Julai 14, 2014, Bw. Avanesyan, aliagizwa afike kwenye kituo kikuu cha polisi cha Yerevan. Alipofika kituoni, alikuta polisi wa Nagorno-Karabakh wakimsubiri. Walimkamata na kumrudisha Nagorno-Karabakh. Siku iliyofuata, aliwekwa chini ya kizuizi na kushtakiwa katika Mahakama ya Mwanzo ya Nagorno-Karabakh.

Wakati wa mashtaka yake, aligundua kwamba miezi minne mapema, mahakama ilikuwa imeagiza akamatwe na afungwe gerezani akisubiri kusikilizwa kwa kesi yake. Mahakama ilipitisha hukumu hiyo, na mara moja Bw. Avanesyan alifungwa. Mahakama ilikataa rufani zote za kuomba asiwekwe chini ya kuzuizi kabla ya kesi yake kusikilizwa.

Septemba 30, 2014, mahakama ilimshtaki na kumhukumu kifungo cha miezi 30. Mahakama ya Rufani ilipitisha hukumu hiyo. Hivyo Bw. Avanesyan akakata rufani katika Mahakama Kuu ya Nagorno-Karabakh, lakini Desemba 25, 2014, mahakama hiyo ilikubaliana na hukumu iliyokuwa imetolewa.

Serikali ya Nagorno-Karabakh inaendelea kuwafunga gerezani vijana wanaume kwa sababu ya kufuata dhamiri zao zilizozoezwa na Biblia. Kwa kufanya hivyo, inapingana na viwango vya kimataifa vinavyoruhusu wanaokataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri, kufanya utumishi wa badala wa kiraia.

Mfuatano wa Matukio

 1. Desemba 25, 2014

  Mahakama Kuu ya Nagorno-Karabakh yakubaliana na hukumu ya awali ya Artur Avanesyan.

 2. Septemba 30, 2014

  Mahakama ya Mwanzo ya Martakert, Nagorno-Karabakh yamshtaki na kumhukumu Artur Avanesyan kifungo cha miezi 30.

 3. Julai 14, 2014

  Artur Avanesyan akamatwa nchini Armenia na kupelekwa Nagorno-Karabakh na kuwekwa chini ya kiziuzi akisubiri kufikishwa mahakamani.

 4. Desemba 30, 2011

  Karen Harutyunyan, Shahidi mwenye umri wa miaka 18, ahukumiwa kifungo cha miezi 30 kwa kukataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri.

 5. Februari 16, 2005

  Areg Avanesyan, mmoja wa Mashahidi wa Yehova, afungwa kwa kukataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri na kuhukumiwa kifungo cha miezi 48.

 6. Juni 12-13, 2001

  Mashahidi watatu wahukumiwa kifungo cha miezi sita hadi mwaka mmoja kwa kukataa kushiriki katika mazoezi ya kijeshi kwa sababu ya dhamiri.