Hamia kwenye habari

Hamia kwenye menyu ya pili

Mashahidi wa Yehova

Kiswahili

MACHI 2, 2015
KYRGYZSTAN

Uhuru wa Kidini Upo Katika Njia Panda Nchini Kyrgyzstan

Uhuru wa Kidini Upo Katika Njia Panda Nchini Kyrgyzstan

Uhuru wa kidini nchini Kyrgyzstan uliongezeka Septemba 4, 2014, Baraza la Katiba la Mahakama Kuu lilipotangaza kwamba visehemu vya Sheria ya Kidini ya mwaka wa 2008 havipatani na Katiba. Hilo lilifungua njia kwa Mashahidi wa Yehova katika maeneo ya kusini mwa Kyrgyzstan kujiandikisha kisheria. *

Licha ya uamuzi huo, Kamati ya Taifa ya Mahusiano ya Kidini (SCRA) bado inakataa kuwaandikisha kisheria Mashahidi walio eneo la kusini mwa Kyrgyzstan. SCRA inasema kwamba sheria ya awali inaendelea kutumika hadi bunge litakapopitisha marekebisho ya Sheria ya Kidini ya mwaka wa 2008, na hivyo Mashahidi wa Yehova hawawezi kuandikishwa kisheria. Matokeo ni kwamba utendaji uleule wa kidini ulioandikishwa kisheria na kuendeshwa kwa amani katika eneo la kaskazini umekutana na ubaguzi na vipingamizi katika eneo la kusini mwa Kyrgyzstan. *

Wakamatwa kwa Sababu ya Utendaji wa Kidini Usiosajiliwa

Juni 30, 2014, katika jiji la Naryn, lililo kusini-mashariki mwa Kyrgyzstan, Zhyldyz Zhumalieva mwenye umri wa miaka 46, alikuwa akitumia muda wake binafsi kushiriki pamoja na jirani zake imani yake ya kidini. Wenye mamlaka katika jiji la Naryn walimkamata na kumhukumu kwa kushiriki na jirani zake imani yake ya kidini akiwa mshiriki wa shirika la kidini lisilosajiliwa. * Tangu Kyrgyzstan ipate uhuru, hii ndiyo mara ya kwanza Shahidi ameshtakiwa kwa sababu ya utendaji wake wa kidini.

Mahakama ya Wilaya ya Naryn ilisikiliza kesi ya rufani dhidi ya Bi. Zhumalieva mnamo Agosti 5, 2014. Mahakimu waliuliza maswali mengi, wakitaka kuwaelewa Mashahidi wa Yehova na ujumbe wanaoshiriki na jirani zao. Baada ya kuchunguza ushahidi uliotolewa, mahakimu waliahirisha kesi hiyo hadi Baraza la Katiba litoe uamuzi huo wa Septemba 4, 2014.

Baadaye, Mahakama ya Wilaya ya Naryn ilisikiliza tena kesi ya Bi. Zhumalieva. Mahakama iliamua kuwa hakuna sheria yoyote iliyokiukwa na kwamba raia wote wanahaki ya kikatiba ya kudhihirisha imani yao ya kidini. Ikitegemea uamuzi wa Baraza la Katiba, mahakama ilieleza kuwa Mashahidi wa Yehova wamesajiliwa kitaifa nchini Kyrgyzstan. Ilipinga pia uamuzi wa mahakama ya chini, lakini mwendesha-mashtaka akakata rufani, akidai kuwa uamuzi wa Baraza la Katiba hauhusiani na kesi hiyo ya uhalifu. Desemba 24, 2014, Mahakama Kuu ilikataa rufani hiyo, na kuunga mkono uamuzi ya Mahakama ya Wilaya ya Naryn ya kumwachilia huru Bi. Zhumalieva na hivyo kutetea haki yake ya kushiriki pamoja na jirani zake imani yake ya kidini.

Haki Yapatikana Jijini Osh Licha ya Shutuma za Uwongo

Mwaka wa 2013, Oksana Koriakina na mama yake, Nadezhda Sergienko, walifungwa kifungo cha nyumbani kwa shutuma za kufanya uhalifu walipokuwa wakieleza wengine kuhusu imani yao. Wenye mamlaka jijini Osh walitumia shutuma hizo za uwongo kama msingi wa kudai kuwa Mashahidi wa Yehova wanajihusisha katika “utendaji wa kidini kinyume cha sheria.” Wenye mamlaka wanashikilia kuwa Mashahidi wa Yehova hawaruhusiwi kufanya utendaji wowote hadharani unaohusisha imani yao ya kidini, kwa sababu ya kutosajiliwa kwa shirika lao la kidini.

Mahakama jijini Osh zilifutilia mbali mashtaka hayo ya uhalifu dhidi wanawake hao. Katika uamuzi wake wa Oktoba 7, 2014, hakimu alileleza kuwa wachunguzi wa kesi hiyo walifanya makosa makubwa wakati wa uchunguzi wao na kwamba walikuwa wamewafungulia mashtaka Bi. Koriakina na Bi. Sergienko kwa sababu tu wao ni Mashahidi wa Yehova.

Mwendesha-mashtaka jijini Osh alikata rufani ili kupinga uamuzi wa mahakama iliyosikiliza kesi hiyo. Aliomba irudishwe kwa wachunguzi wa kesi za uhalifu ili “warekebishe” makosa hayo na awafungulie mashtaka Bi. Koriakina na Bi. Sergienko kwa mara ya pili. Mahakama ya rufani ilipokataa ombi lake, alikata rufani kwa Mahakama Kuu ya Kyrgyzstan. Mahakama imepanga kesi hiyo isikilizwe Machi 3, 2015, na Mashahidi wanatumaini kwamba uamuzi wa mahakama hiyo utatetea haki kwa mara nyingine tena.

Je, Uhuru wa Kidini Utaongezeka au Utapungua Nchini Kyrgyzstan?

Shahidi mmoja wa Yehova aliyekuwapo wakati wa kusikilizwa kwa kesi ya Bi. Zhumalieva alieleza hivi: “Tangu mwaka wa 1998, wenye mamlaka wamekuwa wakitusumbua kwa sababu hatujaandikishwa kisheria katika jimbo la Naryn. Hivyo, kupitia maamuzi haya ya Mahakama Kuu, tunatumaini kwamba hatimaye sasa tutasajiliwa.”

Mashahidi wa Yehova wanasubiri kwa hamu kusajiliwa katika jimbo la Naryn, jijini Osh, na sehemu nyinginezo kusini mwa Kyrgyzstan ili wafanye ibada kwa amani bila kusumbuliwa. Ikiwa nchi ya Kyrgyzstan itafuata maamuzi ya mahakama yake kuu, itakuwa imepiga hatua katika kutetea uhuru wa kidini wa raia zake.

^ fu. 2 Ona makala “Mahakama Kuu ya Kyrgyzstan Yatetea Uhuru wa Kidini wa Mashahidi wa Yehova” ili upate maelezo zaidi kuhusu uamuzi wa Septemba 4, 2014, wa Baraza la Katiba la Mahakama Kuu.

^ fu. 3 Mashahidi wamesajiliwa kitaifa, na pia katika mashirika yao ya kidini katika maeneo ya kaskazini ya nchi. Hata hivyo, wenye mamlaka wamewanyima tena na tena usajili katika maeneo ya kusini mwa nchi.

^ fu. 5 Kipengele cha 395(2) cha Administrative Code of the Kyrgyz Republic kinakataza ukiukwaji wa “sheria za kupanga na kufanya mikutano ya kidini, maandamano, na sherehe nyingine za kidini.”