Hamia kwenye habari

Hamia kwenye menyu ya pili

Mashahidi wa Yehova

Kiswahili

NOVEMBA 5, 2014
KYRGYZSTAN

Mahakama Kuu ya Kyrgyzstan Yatetea Uhuru wa Kidini wa Mashahidi wa Yehova

Mahakama Kuu ya Kyrgyzstan Yatetea Uhuru wa Kidini wa Mashahidi wa Yehova

Septemba 4, 2014, ilikuwa tarehe muhimu kwa Mashahidi wa Yehova na kwa uhuru wa kidini nchini Kyrgyzstan. Siku hiyo Baraza la Katiba la Mahakama Kuu ya Kyrgyzstan lilitangaza kwamba visehemu vya Sheria ya Kidini * ya mwaka wa 2008 havipatani na katiba. Uamuzi huo ulithibitisha kwamba Mashahidi wana haki ya kuendesha shughuli zao za kidini kwa uhuru katika eneo la kusini mwa Kyrgyzstan, eneo ambalo, kwa miaka minne iliyopita, wamekuwa wakinyimwa kibali cha kisheria.

Mashahidi wa Yehova walijiandikisha nchini Kyrgyzstan mwaka wa 1998, na kotekote katika nchi hiyo, walifurahia kiasi fulani cha uhuru. Hata hivyo, tangu Sheria ya Kidini ilipoanza kufanya kazi mwaka wa 2008, polisi wamekuwa wakiwashambulia Mashahidi wa Yehova katika mikutano yao ya kidini katika maeneo ya kusini mwa Kyrgyzstan, wakidai kwamba shughuli za Mashahidi ni “kinyume cha sheria“ eti kwa sababu hawajajiandikisha pamoja na mashirika ya kidini ya eneo hilo. Wakati huohuo, Kamati ya Taifa ya Mahusiano ya Kidini (SCRA) ilitumia vibaya vizuizi vilivyo katika Sheria ya Kidini ya mwaka wa 2008 kuzuia jitihada Mashahidi kuandikishwa katika maeneo hayo. Uamuzi uliofanywa Septemba 4 uliondoa vikwazo hivyo.

Hatua Muhimu ya Kisheria

Sheria ya Kidini ya mwaka wa 2008 inakataza “shughuli na kazi za shirika la kidini” bila kuandikishwa (Kifungu cha 8(2)). Kamati ya SCRA ilielewa kwamba kifungu hicho kilimaanisha kuwapiga marufuku Mashahidi wa Yehova wasifanye shughuli zozote za kidini katika miji na majiji nchini Kyrgyzstan ambapo hawajajiandikisha na mashirika ya kidini ya maeneo hayo. Sheria hiyo ilisema pia ni lazima orodha iliyotiwa sahihi kisheria ya waanzilishi 200 wa shirika la kidini ipelekwe na kuidhinishwa na baraza la jiji la eneo hilo (Kifungu cha 10(2)) kabla shirika hilo halijaomba kuandikishwa na SCRA. Jambo hilo lilikuwa gumu kwa Mashahidi wa Yehova kwa kuwa ili kuruhusiwa kisheria kukutana kwa ajili ya ibada, waliambiwa na Kamati ya SCRA kwamba lazima wawe wameandikishwa katika eneo hilo, lakini hawakuweza kuandikishwa kwa sababu baraza la jiji la eneo hilo halikuwaidhinisha waanzilishi wa shirika lao. Hilo liliipa Kamati ya SCRA na mamlaka ya eneo hilo sababu ya kuwasumbua Mashahidi kwa sababu hawakufikia viwango hivyo ili waandikishwe. Sababu ya magumu hayo, Mashahidi walipeleka mashtaka kwa Baraza la Katiba kupinga kifungu hicho cha sheria.

Katika uamuzi huo, Baraza la Katiba lilisema kwamba “mashirika yote ya kidini yako sawa machoni pa sheria na mtu yeyote au kikundi cha watu wa dini fulani hapaswi kupendelewa kuliko watu wa kutoka dini nyingine.” Mahakama iliamua kwamba Kifungu cha 10(2)—kinachodai orodha ya waanzilishi wa shirika la kidini iithinishwe na baraza la jiji la eneo hilo—hakipatani na katiba. Mahakama ilikata kauli kwamba Kifungu cha 8(2) cha sheria hiyo “kilieleweka vibaya.” Ilisema kwamba haki ya uhuru wa kidini imewekwa kuhakikisha kwamba shirika lolote la kidini linaweza kuendeleza shughuli zake za kidini katika eneo lolote nchini ambalo shirika hilo litaandika katika barua ya kujiandikisha. Barua ya 1998 ya kuanzisha ya Kituo cha Kidini cha Mashahidi wa Yehova katika Jamhuri ya Wakyrgyz tayari ilikuwa imeonyesha kwamba shughuli zake zingefanywa kotekote nchini. Hilo linamaanisha kwamba Mashahidi wa Yehova wako huru kuendesha shughuli zao za kidini katika maeneo yote ya Kyrgyzstan bila kuzuiwa.

Uamuzi Waleta Kitulizo kwa Waathiriwa wa Ubaguzi

Uamuzi uliotolewa Septemba 4 uliwafurahisha sana Mashahidi wa Yehova katika maeneo la kusini mwa Kyrgyzstan. Oksana Koriakina na mama yake, Nadezhda Sergienko, wanaoishi katika jiji la Osh ni baadhi ya waliofurahia uamuzi huo. Walikuwa wamefungwa kifungo cha nyumbani tangu Machi 2013 kwa madai ya uhalifu uliofanywa walipokuwa wanahubiri. Licha ya uthibitisho ulio wazi wa kutohusika, Oksana na Nadezhda walishtakiwa kuwatapeli pesa wanawake watatu wenye umri mkubwa.

Mnamo Septemba 2014, kesi hiyo ilifanyiwa katika Mahakama ya Osh City, na Oktoba 7, 2014, mahakama ikafutilia mbali mashtaka ya uhalifu ambayo wanawake hao walikuwa wamefunguliwa na kuamua kwamba wanapaswa kulipwa kwa sababu ya kushtakiwa kimakosa, kuwekwa chini ya kizuizi, na kufungwa kifungo cha nyumbani. Mahakama ilikiri kwamba Mashahidi hao walidhulumiwa kwa sababu ya chuki ya kidini na ubaguzi, na walikuwa shabaha kwa sababu ya dai lisilo la kweli kwamba shughuli za Mashahidi wa Yehova katika jiji la Osh zilikuwa kinyume cha sheria na eti Mashahidi hawajajiandikisha kama shirika la kidini katika eneo hilo. Katika maneno yao ya kumalizia, Oksana na Nadezhda walitumia uamuzi uliofanywa na Baraza la Katiba mnamo Septemba 4, ambao ulihalalisha shughuli za Mashahidi wa Yehova katika Osh na kotekote katika nchi ya Kyrgyzstan.

Nadezhda Sergienko na Oksana Koriakina

Jitihada za Kuunga Mkono Haki za Kibinadamu Katika Mataifa Yote

Kwa kujiunga na Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa wa Umoja wa Mataifa, Kyrgyzstan ilikubali kutetea haki za kibinadamu na uhuru wa msingi wa raia zake—uhuru wa kidini au imani, uhuru wa kukutanika, na uhuru wa kujieleza. Kupitia uamuzi huo wa karibuni wa kutetea uhuru wa kidini, Baraza la Katiba la Mahakama Kuu ya Kyrgyzstan limetetea kwa uthabiti haki za kibinadamu na uhuru wa msingi. Karibu Mashahidi wa Yehova 5,000 nchini Kyrgyzstan wanathamini uhuru wa kidini ambao wamepata na wanashukuru taasisi za kitaifa kwa kutetea na kuunga mkono uhuru wa msingi ili wote wafurahie.

^ fu. 2 Jina kamili la sheria hiyo ni “Sheria ya Jamhuri ya Wakyrgyz Kuhusu Uhuru wa Kidini na wa Mashirika ya Kidini Katika Jamhuri ya Wakyrgyz.”