Hamia kwenye habari

Hamia kwenye menyu ya pili

Mashahidi wa Yehova

Kiswahili

OKTOBA 19, 2016
KOREA KUSINI

Mahakama ya Rufani ya Korea Kusini Imewahukumu Waliokataa Kujiunga na Jeshi kwa Sababu ya Dhamiri Kuwa Hawana Hatia

Mahakama ya Rufani ya Korea Kusini Imewahukumu Waliokataa Kujiunga na Jeshi kwa Sababu ya Dhamiri Kuwa Hawana Hatia

Oktoba 18, 2016, kitengo cha rufani cha Mahakama ya Wilaya ya Gwangju kiliwaunga mkono wanaume watatu—Hye-min Kim, Lak-hoon Cho, na Hyeong-geun Kim—waliokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri kwa kueleza kwamba hawana hatia ya kuepuka kufanya utumishi wa kijeshi. Wanaume hao watatu, ambao ni Mashahidi wa Yehova, ndio watu wa kwanza kuhukumiwa kuwa hawana hatia kuhusiana na suala hili katika mahakama ya rufani nchini Korea Kusini.

Hakimu Young-shik Kim alisema hivi: “Mahakama inaamini kwamba walikataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya imani yao ya dini na dhamiri zao. Uhuru wa dini na dhamiri ni haki ya kikatiba, ambayo haipaswi kuzuiwa kwa kutoa adhabu.”

Ikiwa mwendesha-mashtaka atakata rufani kuhusiana na uamuzi huu, kesi hiyo itapelekwa kwa Mahakama Kuu ili ichunguzwe upya. Zaidi ya kesi 40 zinazohusu wanaume waliotangazwa kuwa wana hatia kwa kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri, zimepelekwa kwenye Mahakama Kuu na zinasubiri kusikilizwa. Philip Brumley, Wakili wa Mashahidi wa Yehova, alisema hivi: “Ingawa mpaka sasa Mahakama Kuu ya Korea Kusini na Mahakama ya Katiba zimekataa kutambua haki ya wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri, mahakama ya rufani imetumia viwango vya kimataifa kutambua haki hiyo. Kutambuliwa kwa haki hiyo kunaungwa mkono na maamuzi zaidi ya 500 yaliyofanywa na Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Kibinadamu.”