Hamia kwenye habari

Hamia kwenye menyu ya pili

Mashahidi wa Yehova

Kiswahili

OKTOBA 12, 2016
KOREA KUSINI

Wanaokataa Kujiunga na Jeshi kwa Sababu ya Dhamiri Wanasumbuliwa kwa Sababu ya Rekodi za Uhalifu

Wanaokataa Kujiunga na Jeshi kwa Sababu ya Dhamiri Wanasumbuliwa kwa Sababu ya Rekodi za Uhalifu

Januari 2016, Hyun-jun Gwon na Gwang-taek Oh walisafiri kwa ndege kutoka Korea Kusini wakiwa na matazamio makubwa ya kufurahia likizo yao nchini Japani. Walipofika kwenye uwanja wa ndege wa Nagoya nchini Japani, walikwenda katika ofisi za uhamiaji wakitarajia kwamba wangeingia nchini Japani bila matatizo yoyote. Badala ya kuwaruhusu waingie nchini, maofisa wa uhamiaji waliwahoji kwa sababu vibali vyao vilionyesha kwamba waliwahi kuhukumiwa kifungo gerezani kwa sababu ya uhalifu.

Vijana hao wawili waliwaeleza maofisa kwamba walitumikia vifungo gerezani kwa kukataa kujiunga na utumishi wa jeshi kwa sababu ya dhamiri na kwamba msimamo wao unatambuliwa kimataifa kuwa ni wa haki. Hata hivyo, maofisa hao walikataa kuwaruhusu kuingia Japani. Waliomba msaada wa ubalozi wa Japani nchini Korea Kusini lakini bado hawakufanikiwa. Ni jambo lenye kusikitisha sana kwamba kwa sababu ya kushikilia imani yao kidini vijana hao wanakabili hali ngumu ambazo zitaendelea kuathiri maisha yao kwa njia wasizotarajia.

Fedheha na Maumivu

Nchini Korea Kusini kuna machaguo mawili tu: ama ujiunge na jeshi au uende gerezani. Korea Kusini inakiuka waziwazi mikataba ya kimataifa kuhusu haki za binadamu kwa kutowapa chaguo lingine wale wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri. * Ukosefu huo wa haki unafanywa kuwa mbaya zaidi kwa kuwa wafungwa watakuwa na rekodi za kudumu za vifungo hivyo, ambazo serikali inakataa kuzifuta. Hilo limefanya hali iwe mbaya zaidi kwa sababu wanaendelea kutendewa isivyo haki muda mrefu hata baada ya kumaliza kifungo chao. Rekodi zao za kudumu za “uhalifu” zinafanya wakose ajira na zinawazuia kusafiri kwenda nchi nyingine, kama vile Japani—eneo ambalo hutembelewa kwa ukawaida na raia wa Korea Kusini.

Wanaume wengine nchini Korea Kusini waliofungwa kwa kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri wanakabiliana na hali kama hiyo. Kwa mfano, mnamo Desemba 2011, Bw. Jin-mo Kang na mke wake ambaye ni raia wa Japani anayeitwa Kotomi, walisafiri kwenda Japani kuwatembelea watu wa familia ya mke wake. Bw. Kang alizuiwa kuingia nchini humo kwa sababu ya rekodi ya uhalifu aliyopata baada ya kufungwa kwa kukataa kujiunga na jeshi naye akalazimika kumwacha mke wake nchini Japani na yeye akarudi Korea Kusini. Ingawa alijaribu mara nyingi kupata kibali, maofisa wa uhamiaji hawakumruhusu kuingia nchini Japani.

Nchi Pekee Inayoweka Vikwazo

Japani ndiyo nchi pekee ambayo haiwaruhusu watu waliokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri kuingia nchini humo. Hata hivyo, katika kisa cha Bw. Oh, ubalozi wa Japani nchini Korea Kusini hatimaye ulimpa viza ya kuingia Japani. Aliwapa maofisa wa ubalozi barua ya kukaribishwa na marafiki zake wa Japani ambao walifanya mipango ya mahali pa kuishi na kumpa mahitaji mengine. Alifaulu kuingia nchini Japani mwanzoni mwa Julai 2016.

Tofauti na Japani, nchi nyingi za kidemokrasia zinatambua kwamba wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri si wahalifu na zinawaruhusu kuingia nchini mwao licha ya kwamba wana rekodi ya “uhalifu.” Nchi nyingine hata zinawaruhusu kuishi humo. Australia, Kanada, na Ufaransa zimewapa hifadhi wanaume kutoka Korea Kusini ambao walikataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri. Jambo hilo linapatana na azimio la Baraza la Umoja wa Mataifa la Haki za Kibinadamu, ambalo lilihimiza nchi mbalimbali “kufikiria kuwapa hifadhi wale wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri ambao wanatoroka nchi zao kwa sababu ya kuhofia mateso watakayokabili kwa kukataa kujiunga na jeshi na ambao katika nchi zao hakuna utumishi wowote wa badala unaotolewa.” *

Wawakilishi wa Mashahidi wa Yehova wanaoshughulikia masuala ya kisheria wanajitahidi kufanya mawasiliano na maofisa wa Japani ili kusuluhisha tatizo hilo. André Carbonneau, mwanasheria wa kimataifa wa haki za kibinadamu, alisema hivi: “Kufanikiwa kwa Bw. Oh kuingia Japani kunaonyesha kwamba kushughulika na wanaume wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri si jambo gumu. Wenye mamlaka nchini Japani wanapaswa tu kuweka sheria itakayowatambua wale wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri kuwa watu wanaopenda amani wala si ‘wahalifu,’ na kwamba wanapaswa kuruhusiwa kuingia nchini humo licha ya rekodi zao za kufungwa.”

Je, Korea Kusini Itaondoa Ukosefu wa Haki?

Jamii ya kimataifa inatambua kwamba wale waliofungwa kwa sababu ya dhamiri si wahalifu. Tangu 2006 Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Kibinadamu (CCPR) imerudia mara nyingi kuihimiza Korea Kusini isiwafunge wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri. CCPR inatambua kwamba “hakuna misingi ya kisheria” ya kuwafunga wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri nchini Korea Kusini. Imeihimiza serikali ikubali sheria inayolinda haki ya kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri. Katika maamuzi yake, CCPR iliagiza Korea Kusini ifute rekodi za uhalifu za wale waliofungwa kwa kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri. *

Korea Kusini imeendelea kupuuza maamuzi ya CCPR. Hata hivyo, ikiwa Korea Kusini imekubali Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa inapaswa kutii maamuzi ya CCPR hata ingawa yatapingana na sheria ya nchi yao.

Mpaka wakati Korea Kusini itakapokubali viwango vya kimataifa na kutambua kwamba kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri ni haki ya msingi, mamia ya raia wake watakuwa wameteseka kutokana na vifungo na fedheha ya kuwa na rekodi ya uhalifu. * Mashahidi wa Yehova wanaitarajia wakati ambapo Korea Kusini itatambua haki za wale wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri na kufuta rekodi zao za uhalifu. Kwa sasa, raia wa Korea Kusini kama vile Bw. Gwon na Bw. Oh wanatumaini kwamba wenye mamlaka nchini Japani watakubali kuweka sheria maalumu ya kuwaruhusu wale wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri waingie Japani.

^ fu. 5 Kwa sasa Korea Kusini ni mojawapo kati ya nchi nne ambazo zinawafunga Mashahidi wa Yehova kwa kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri. Nchi nyingi ambazo utumishi wa kijeshi ni wa lazima zinaheshimu haki za wale wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri kwa kuwaruhusu wafanye utumishi fulani wa badala wa kiraia ambao hauhusiani na mambo ya kijeshi.

^ fu. 9 Ona Azimio 24/17 “Kukataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri,” lililokubaliwa na Baraza la Haki za Kibinadamu Oktoba 8, 2013.

^ fu. 12 Ona Mawasiliano Na. 1642-1741/2007, Jeong et al v. The Republic of Korea, Maoni yaliyokubaliwa na Kamati Machi 24, 2011.

^ fu. 14 Katika miaka mitano iliyopita, Korea Kusini iliwafunga vijana Mashahidi 2,701 waliokataa kujiunga na utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri.