Hamia kwenye habari

Familia ya Mashahidi wa Yehova nchini Korea Kusini ikishiriki katika kampeni

MACHI 1, 2018
KOREA KUSINI

Mashahidi Nchini Korea Kusini Watuma Ombi kwa Rais: Suluhisha Suala la Kukataa Kujiunga na Jeshi kwa Sababu ya Dhamiri

Mashahidi Nchini Korea Kusini Watuma Ombi kwa Rais: Suluhisha Suala la Kukataa Kujiunga na Jeshi kwa Sababu ya Dhamiri

Matukio ya karibuni ya Korea Kusini yanaonyesha kwamba huenda serikali inaweza kufanya mabadiliko makubwa kuhusiana na suala la kuzingatia haki za msingi za kibinadamu. Desemba 7, 2017, Rais wa Korea Kusini, Jae-in Moon alikutana na maofisa wa Tume ya Haki za Kibinadamu ya Korea (NHRC) na kuwaomba watoe mapendekezo yao kuhusu njia ya kuboresha hali ya haki za kibinadamu ili ifikie viwango vya kimataifa. Rais Moon aliiomba tume hiyo itoe pendekezo hususa la suluhisho ambalo litaisaidia serikali kuondoa sera yake ya kuwafunga wanaume wanaokataa kujiunga na utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri.

Baada ya habari kuhusu mkutano huo kutangazwa sana na vyombo vya habari, Mashahidi wa Yehova nchini Korea Kusini walipanga kampeni ya kukusanya sahihi za watu kuhusu maombi wanayotaka kumfikishia rais. Sera ya serikali ya kuwaadhibu kwa vifungo wale wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri imeathiri vizazi vingi vya Mashahidi. Kwa kuwa Rais Moon ametoa maagizo kwamba serikali ifanyie kazi maombi kutoka kwa raia; maombi haya ni kuhusu kuomba msaada wa rais wa kutafuta suluhisho kwa tatizo ambalo wale wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri wamekabili kwa miaka 70 hivi.

Ofisi ya taifa ya Mashahidi wa Yehova ilipanga kupeleka maombi

Majuma manne tu tangu kuanza kwa kampeni hiyo, maombi yalikuwa yamekamilika. Wale waliotia sahihi maombi hayo walitia ndani wanaume zaidi ya 14,000 walioadhibiwa kama wahalifu kwa kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri, pamoja na washiriki 26,000 wa familia ambazo ziliathiriwa na kushtakiwa na kufungwa kwa wanaume hao.

Maombi yaliwasilishwa kwenye Ofisi ya Rais, Januari 15, 2018

Januari 15, 2018, wawakilishi 6 wa Mashahidi 41,275 waliotia sahihi maombi hayo, waliyapeleka kwenye Ofisi ya Rais. Maombi hayo yalionyesha shukrani za dhati kwa kuwa rais amekazia uangalifu jambo hili, yanaonyesha matokeo mabaya ya miaka 70 ya kuwaadhibu kwa vifungo wale wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri, na yamekazia faida ambazo taifa litapata kwa kusuluhisha tatizo hili. Januari 16, 2018, Ofisi ya Rais iliyapeleka maombi hayo kwenye Wizara ya Ulinzi wa Taifa ili yashughulikiwe.

Wakati maombi hayo yalipokuwa yakitayarishwa, wawakilishi wa Mashahidi wa Yehova walikutana na maofisa wa Tume ya Haki za Kibinadamu (NHRC). Waliwaeleza sababu za Kimaandiko zinazofanya Mashahidi wa Yehova wakatae utumishi wa kijeshi. Ikiwa Mashahidi vijana wataandikishwa kwenye programu ya utumishi wa badala wa kiraia watakuwa na manufaa kwa serikali na wanaweza kutumikia kwa manufaa ya nchi badala ya kukaa tu gerezani. Maofisa hao waliwaeleza Mashahidi kwamba kukataa kujiunga na utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri ndilo suala la haki za kibinadamu lililopewa kipaumbele na Tume ya Haki za Kibinadamu katika mwaka wa 2018.

Idadi ya wale wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri ambao wamefungwa nchini Korea Kusini ni kubwa kuliko jumla ya idadi ya watu waliofungwa kwa kosa hilo katika nchi nyingine zote. Maofisa wanapoifikiria upya sera hiyo ya serikali iliyodumu kwa muda mrefu, Mashahidi wa Yehova wanatumaini kwamba mpango huu mpya utamaliza vifungo vya miaka mingi ambavyo Mashahidi vijana kwa ujumla wamekabili, yaani, vifungo vya zaidi ya miaka 36,700 kwa sababu walikataa kujiunga na utumishi wa kijeshi.