Hamia kwenye habari

Hamia kwenye menyu ya pili

Mashahidi wa Yehova

Kiswahili

JULAI 13, 2016
KOREA KUSINI

Mashahidi wa Yehova Walio Gerezani Nchini Korea Kusini Wawasilisha Malalamiko ya Ziada

Mashahidi wa Yehova Walio Gerezani Nchini Korea Kusini Wawasilisha Malalamiko ya Ziada

Tangu Januari 2016, zaidi ya wanaume 50 nchini Korea Kusini ambao wamekataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri wamewasilisha malalamiko kwenye Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Vifungo Visivyo vya Haki. Watu hao wanaishutumu serikali ya Korea Kusini kwa kuwafunga isivyo haki kwa sababu tu walitumia uhuru wao wa kidini na dhamiri.

Sababu ya Kuwasilisha Malalamiko

Kamati mbili za Umoja wa Mataifa, ile ya Vifungo Visivyo vya Haki na ile ya Haki za Kibinadamu, zimeamua kwamba kuwafunga watu wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri kunaonwa kuwa ni “vifungo visivyo vya haki.” * Uamuzi wa mwaka wa 2014 wa Kamati hiyo kuhusiana na suala hili ulisema kwamba serikali ya Korea Kusini inapaswa kukomesha adhabu zote zisizo za haki dhidi ya wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri, kuwalipa fidia wale iliyowafunga, na kufuta rekodi zao za uhalifu. Kwa msingi wa uamuzi huo, jumla ya Mashahidi 682 nchini Korea Kusini wamewasilisha malalamiko yao kwenye Kamati ya Vifungo Visivyo vya Haki. *

Uchunguzi wa Kimataifa na wa Kitaifa

Baada ya Kamati hiyo ya Vifungo Visivyo vya Haki kuwasilisha malalamiko hayo kwa serikali ya Korea Kusini na kupata jibu kutoka kwa serikali, Kamati hiyo itatoa uamuzi wake. Kamati ikikubaliana na walalamishi kwamba Korea Kusini ina hatia ya kuwafunga watu isivyo haki, Kamati hiyo itaiomba serikali ichukue hatua zinazofaa kurekebisha hali na kuepuka kuwaona kama wahalifu watu wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri.

Mbali na hilo, Mahakama ya Katiba ya Korea Kusini inachunguza ikiwa Sheria ya Utumishi wa Kijeshi inapatana na katiba. Uamuzi utatolewa hivi karibuni. Mahakama hiyo inatambua kwamba zaidi ya walalamikaji 600  wamewasilisha malalamiko kwenye Kamati ya Vifungo Visivyo vya Haki. Pia, Mahakama hiyo inatambua kwamba Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Kibinadamu imeisihi mara nyingi serikali ya Korea Kusini itambue kuwa kukataa kujiunga na jeshi ni haki na iandae programu ya utumishi wa badala wa kiraia. Jamii ya kimataifa inachunguza kwa uangalifu ione kama mahakama kuu ya Korea Kusini itatetea haki ya msingi ya wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri.

^ fu. 4 Baraza la Haki za Kibinadamu, Mapendekezo ya Kikundi Kinachoshughulikia Vifungo Visivyo vya Haki, Pendekezo Na. 16/2008 (Uturuki), UN Doc. A/HRC/10/21/Add.1, uku. 145, fu. 38 (Mei 9, 2008). Kamati ya Haki za Kibinadamu, Maoni, Young-kwan Kim et al. v. Republic of Korea, Ujumbe Na. 2179/2012, UN Doc. CCPR/C/112/D/2179/2012, fu. 7.5 (Oktoba 15, 2014).

^ fu. 4 Mnamo 2015, watu 631 waliokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri waliwasilisha malalamiko, na 51 wengine wamefanya hivyo katika mwaka huu wa 2016.