Hamia kwenye habari

KOREA KUSINI

Wamefungwa kwa Sababu ya Imani Yao​—Korea Kusini

Wamefungwa kwa Sababu ya Imani Yao​—Korea Kusini

Februari 28, 2019, baada ya jitihada nyingi za karibu miaka sabini, Mashahidi wa Yehova nchini Korea Kusini walishangilia kwa furaha tele. Siku hiyo, mwamini mwenzao wa mwisho kati ya wale waliofungwa gerezani kwa sababu ya kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri, aliachiliwa huru. Mashahidi wa Yehova wanashukuru sana kwamba sasa mahakama ya Korea Kusini inatambua kuwa mtu ana haki ya kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri na anaweza kufanya utumishi wa badala wa kiraia.

Mwaka mmoja hivi baadaye, Mahakama Kuu ilianza kufuta kesi zote za waliokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri. Februari 13, 2020, Mahakama iliwafutia mashtaka Mashahidi wa Yehova 108, kisha Februari 27, Mashahidi wengine 210 walifutiwa mashtaka.

Utekelezaji wa Utumishi wa Badala wa Kiraia

Bunge lilitunga sheria mpya kuhusu utumishi wa badala wa kiraia mwezi wa Desemba 2019, itakayomsaidia yeyote atakayekataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri. Utekelezaji wa sheria hiyo unatarajiwa kuanza miezi ijayo ukiwa na lengo la kuwaruhusu vijana Wakristo wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri, kufanya utumishi utakaonufaisha wananchi wa Korea. Kulingana na viwango vya kimataifa vya utumishi wa badala, utumishi huo unapaswa “kuwa wa kiraia” na usiosimamiwa au kuratibiwa na jeshi. Kufuatwa kikamili kwa sheria hiyo ni jambo la muhimu sana katika kuhakikisha kwamba wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri wanapewa nafasi ya kufanya utumishi halali badala wa kiraia. Kwa kuongezea, kulingana na viwango vya kimataifa, utumishi wa badala wa kiraia haupaswi kuwa adhabu. Hilo lilitajwa kwenye uamuzi wa Mahakama ya Katiba katika Juni 2018 iliposema: “Ikiwa utumishi wa badala wa kiraia utachukua muda mrefu na utapita kiasi hivi kwamba inakuwa vigumu kwa waliokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri kufanya utumishi huo, hali hiyo itakuwa kinyume au kupunguza hadhi ya utumishi wa badala wa kiraia na kuufanya uwe adhabu.”

Oktoba 26, 2020, Mashahidi 63 wa Yehova walikubali aina hiyo ya utumishi na wakaanza kufanya kazi ya miaka mitatu katika gereza moja. Hata hivyo, hali kuhusu utekelezwaji wa utumishi wa badala wa kiraia bado hazijulikani. Wenye mamlaka bado wanajadili ni kwa kadiri gani wanaume hao wataruhusiwa kuondoka gerezani baada ya saa za kazi ili kutekeleza uhuru wao wa ibada na kushiriki katika utendaji mwingine.

Wakati huu pia haijulikani ikiwa programu ya utumishi wa badala wa kiraia iliyopo sasa inapatana na viwango vya kimataifa. Ikiwa sheria itaruhusu jeshi lisimamie au kuratibu utumishi huo, au ikiwa sheria inakusudia kuadhibu, Mashahidi wa Yehova waliokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri watalazimika kukataa aina hiyo ya utumishi wa badala wa kiraia. Kwa upande mwingine, ikiwa utumishi wa badala wa kiraia hautakuwa chini ya usimamizi au uratibu wa jeshi, au ikiwa hautakusudiwa kuwa adhabu, kila Shahidi wa Yehova atayekataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri, atajiamulia mwenyewe ikiwa atakubali utumishi huo.

Mfuatano wa Matukio

 1. Machi 31, 2021

  Jin-seong Bang aachiwa huru mapema baada ya kupewa msamaha.

 2. Machi 10, 2020

  Jin-seong Bang aanza kifungo cha miezi 18 gerezani.

 3. Februari 13 na 27, 2020

  Mahakama Kuu yawafutia mashtaka Mashahidi zaidi ya 300; Shahidi mmoja apatikana na hatia.

 4. Desemba 2019

  Bunge la Korea Kusini latunga sheria inayoruhusu utumishi wa badala wa kiraia.

 5. Februari 28, 2019

  Shahidi wa Yehova wa mwisho kutumikia kifungo cha gereza aachiwa huru.

 6. Novemba 1, 2018

  Mahakama Kuu yatoa uamuzi wa kwamba si kosa la kihalifu mtu akikataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri.

 7. Juni 28, 2018

  Mahakama ya Katiba ya Korea Kusini yatangaza kwamba kutokuwa na utumishi wa badala wa kiraia kunavunja katiba.