Hamia kwenye habari

Mashahidi wa Yehova

Chagua lugha Kiswahili

JANUARI 25, 2017
KOREA KUSINI

“Mahakama Yatoa Uamuzi Bora wa Mwaka”

“Mahakama Yatoa Uamuzi Bora wa Mwaka”

Vijana watatu, Hye-min Kim, Lak-hoon Cho, na Hyeong-geun Kim, walitembea kwa uhuru kutoka mahakama ya rufani, wakifurahi kwamba hawakuhukumiwa kifungo gerezani. Jambo hilo lilishangaza sana kwa sababu kesi zao zilihusu kukataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri, na kwa msingi huo maelfu ya wanaume nchini Korea Kusini hufungwa kila mwaka. Suala hilo ambalo halijasuluhishwa kwa muda mrefu ndilo lilifanya baba zao na wanaume wengine zaidi ya 19,000 wafungwe gerezani kabla yao na wanaume wengine wanatarajia kufungwa kwa sababu ya suala hili. Kuachiliwa kwao ni mojawapo tu ya faida zinazotokana na uamuzi huu wa kihistoria wa “kutokuwa na hatia” uliotolewa na Mahakama ya Rufani ya Gwangju.

Mahakama ya Rufani Yatoa “Uamuzi Bora wa Mwaka”

Magazeti 200 hivi ya habari yaliripoti kuhusu kesi hiyo, yakikazia si kuhusu uamuzi wa kwanza wa kutokuwa na hatia kuwahi kutolewa na mahakama ya rufani tu, bali pia jinsi upendezi katika suala hilo unavyozidi kuongezeka. Gazeti moja la habari lilisema huo ndio “uamuzi bora wa mwaka uliotolewa na mahakama” na lingine lilieleza kwamba huo ni mojawapo ya maamuzi matano bora yaliyotolewa na mahakama katika mwaka wa 2016 nchini Korea Kusini.

Uamuzi huo wa mahakama ya rufani unaonyesha jinsi mtazamo wa wataalamu wa sheria na mahakimu kuhusu suala hili unavyobadilika. Katika kesi nyingi za karibuni, mahakimu waliona kwamba wanaume wanaoshtakiwa wanachochewa na sababu halali na wanashikamana sana na maadili, hivyo, kuwahukumu ili kuwashurutisha watumikie jeshini au kuwaadhibu kwa sababu ya kukataa kutumikia kungekuwa ni kukiuka uhuru wao wa dhamiri. Mahakimu hao walifikia mkataa kwamba wanaume hao wana “sababu za msingi” za kukataa kujiunga na utumishi wa kijeshi. Badala ya kuwaona wanaume hao kama watu wanaokimbia utumishi wa kijeshi, katika kipindi cha miezi 20 iliyopita mahakimu wamewahukumu wanaume 16 kuwa hawana hatia.

Mwanasheria Du-jin Oh, ambaye huwawakilisha wengi wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri, alisema hivi: “Mabadiliko haya ni muhimu. Nimefurahi sana kuona idadi kubwa ya maamuzi ya kutokuwa na hatia yanatolewa na mahakama za chini na pia hivi karibuni uamuzi huo umetolewa na mahakama ya juu. Katika kila kesi, mwendesha-mashtaka anatarajiwa kukata rufani kupinga maamuzi hayo, lakini mabadiliko hayo yaliyotukia katika fikira za mahakimu wa Korea Kusini yanaongeza mkazo juu ya uamuzi unaosubiriwa wa Mahakama ya Katiba kuhusu haki ya mtu kueleza kuhusu dhamiri yake.”

Kutafuta Suluhisho

Taifa zima linasubiri Mahakama ya Katiba nchini Korea Kusini itoe uamuzi wake. Mahakama hiyo ya juu imepewa wajibu wa kupima ikiwa mambo yanayoelezwa na katiba kuhusu uhuru wa dhamiri yanapatana na adhabu inayoonyeshwa katika Sheria ya Utumishi wa Kijeshi dhidi ya wale wanaotumia uhuru huo kukataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya imani zao za dini au imani nyingine.

Dae-il Hong, msemaji wa Mashahidi wa Yehova nchini, alisema hivi: “Maelfu ya familia nchini Korea Kusini wanasubiri suluhisho ambalo litaheshimu maadili ya kidini ya vijana ambao hawawezi kulazimishwa kutenda kinyume na dhamiri zao. Tunatarajia Mahakama ya Katiba itatoa uamuzi utakaowaheshimu vijana hao.”