Hamia kwenye habari

MACHI 1, 2018
KOREA KUSINI

Mahakama za Korea Kusini Zinajitahidi Kutafuta Suluhisho kwa Wanaokataa Kujiunga na Jeshi kwa Sababu ya Dhamiri

Badala ya kuendelea kuwafunga Mashahidi wa Yehova wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri, mahakimu nchini Korea Kusini wanajitahidi kutafuta njia ya makubaliano. Baadhi ya mahakimu wanakazia kinachofanya wanaume hao wakatae kujiunga na jeshi; ni kwa sababu ya dhamiri inayotegemea kanuni za Kimaandiko, kwamba hawataki kuwadhuru wengine. * Hivyo, kwa kutegemea haki ya msingi ya uhuru wa dhamiri, baadhi ya mahakama zimetoa uamuzi kwamba vijana hao hawana hatia ya kuepuka utumishi wa kijeshi. Tangu Mei 2015, mahakimu katika mahakama walitoa maamuzi 66 ya “kutokuwa na hatia” kwa Mashahidi wa Yehova ambao wamekataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri,—hilo linaonyesha ongezeko kubwa kutoka kesi 4 tu zilizotolewa uamuzi kama huo kwa makumi ya miaka iliyopita.

Uamuzi wa Kuvutia

Jambo moja la kipekee ni kwamba Februari 1, 2018, mahakama ya rufaa ya Busan, iliunga mkono uamuzi huu wa “kutokuwa na hatia” na kupuuza maamuzi ya awali ya Mahakama Kuu na Mahakama ya Kikatiba kuhusiana na suala hili. Uamuzi huo ulikuwa wa pekee kwa sababu mbili—Wilaya ya Busan inashikilia sana mambo ya kale, na hakimu aliyeshughulikia kesi hii, Jong-du Choi, zamani alikuwa ametangaza mtu aliyekataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri kuwa na hatia.

Jopo la mahakimu watatu lilikazia wajibu wa nchi ya Korea Kusini kulingana na katiba wa kuheshimu sheria za kimataifa ambazo taifa hili inazikubali, yaani, katika kisa hiki iheshimu Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa, ambao unatambua haki ya kukataa kujiunga na utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri. Mahakama ilieleza kwamba “kuwaadhibu wale wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri kwa kuwafunga gerezani kunapingana na sheria ya 18 ya Mkataba, kwa hiyo, . . . ni jambo linalofaa kutafsiri kwamba kukataa kujiunga na utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri ni “sababu ya msingi” ya kukataa kujiandikisha jeshini. Uamuzi huo ulitangazwa sana na watu wengi wanaamini kwamba utazichochea taasisi za kisheria kufanya maamuzi mazuri.

Kutazamia suluhisho

Miaka iliyopita, mahakimu walihukumu wastani wa vijana 500-600 kwenda gerezani kila mwaka kwa sababu ya jambo hili, lakini sasa mahakimu wengi wanaahirisha kesi hizo. Idadi ya kesi ambazo hazijafanyiwa maamuzi kwa sasa ni zaidi ya 700, na idadi hiyo inaendelea kuongezeka mahakimu wanapotarajia uamuzi wa Mahakama ya Kikatiba ambao bado haujatolewa kuhusu suala hili. Kufikia Desemba 31, 2017, Mashahidi 267 tu ndio waliokuwa gerezani—idadi ndogo zaidi kwa kipindi cha miaka kumi.

Mahakama ya Kikatiba ndiyo itakayoamua ikiwa mahakimu wanapaswa kutumia Sheria ya Utumishi wa Kijeshi kuwaadhibu wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri kwa kosa la kuepuka utumishi wa kijeshi au ikiwa haki ya kikatiba ya uhuru wa dhamiri itawalinda watu hao kulingana na viwango vya kimataifa. Watu wengi nchini Korea Kusini wanasubiri kwa hamu uamuzi wa Mahakama utakaoonyesha heshima kwa vijana ambao dhamiri yao inaweza kuwaruhusu kukubali utumishi wa badala wa kiraia utakaonufaisha jamii.

Ikiwa Mahakama itatoa uamuzi unaowaunga mkono wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri, itaifanya Korea Kusini ijipatanishe na maamuzi ya Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Kibinadamu ya kuhusu kesi za mamia ya watu. Kamati hiyo imeiagiza Korea Kusini iache kuwafunga wale wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri na iheshimu haki yao ya msingi ya uhuru wa dhamiri.

^ fu. 2 Kwa mfano, Isaya 2:4 inasema: “Watafua panga zao ziwe majembe ya plau na mikuki yao iwe miundu. Taifa halitainua upanga dhidi ya taifa lingine, wala hawatajifunza vita tena kamwe.” Yesu aliwaagiza wafuasi wake wajulikane kwa sababu ya upendo wao: “Ninawapa ninyi amri mpya, kwamba mpendane; kama vile ambavyo nimewapenda, nanyi mpendane vivyo hivyo. Kwa jambo hili wote watajua kwamba ninyi ni wanafunzi wangu—mkiwa na upendo miongoni mwenu.”—Yohana 13:34, 35.