Hamia kwenye habari

Hamia kwenye menyu ya pili

Mashahidi wa Yehova

Kiswahili

OKTOBA 1, 2013
KOREA KUSINI

Jamii ya Kimataifa Yalalamikia Ukosefu wa Haki wa Korea Kusini

Jamii ya Kimataifa Yalalamikia Ukosefu wa Haki wa Korea Kusini

Korea Kusini inawafunga gerezani mamia ya wanaume vijana ambao si wahalifu. Kwa nini? Kwa sababu wanaume hao ni Mashahidi wa Yehova walioazimia kufuata dhamiri zao kwa kukataa kufanya utumishi wa kijeshi. Kwa kuwa nchi ya Korea hailindi haki za wale wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri zao, Mashahidi wanaokamatwa huhukumiwa na kufungwa gerezani. Katika kipindi cha miaka 60 iliyopita zaidi ya Mashahidi wa Yehova 17,000 wamefungwa gerezani kwa sababu ya kukataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri.

Ili kuwafanya watu watambue suala hilo, ofisi ya kitaifa ya Mashahidi wa Yehova ya Korea Kusini ilichapisha broshua inayoitwa  Conscientious Objection to Military Service in Korea (Kukataa Utumishi wa Kijeshi kwa Sababu ya Dhamiri Nchini Korea). Broshua hiyo inaangazia jinsi ambavyo Korea imeshindwa kufuata viwango vya kimataifa na kushindwa kulinda haki za wale wanaokataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri. Pia inasimulia historia fupi ya vijana Mashahidi ambao wamefungwa gerezani kwa sababu hawangeweza kutenda jambo lisilopatana na dhamiri zao. Bw. Dae-il Hong, mwakilishi wa ofisi ya Mashahidi wa Yehova huko Korea, na Bw. Philip Brumley, Mshauri Mkuu wa Mashahidi wa Yehova huko New York, wanatufahamisha kwa kina kuhusu suala hili la muda mrefu la ukosefu wa haki nchini Korea Kusini.

Jamii ya kimataifa imetendaje kuhusu ukosefu wa haki ulioko Korea Kusini?

Philip Brumley: Nchi kadhaa zimeishutumu nchi ya Korea kwa kushindwa kutambua haki za msingi za wale wanaokataa kujiunga na utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri. Katika mkutano wa hivi karibuni wa Umoja wa Mataifa unaoitwa Universal Periodic Review, nchi nane—Hungaria, Ufaransa, Ujerumani, Poland, Slovakia, Hispania, Marekani, na Australia—ziliomba Korea iache kuwahukumu wale wanaokataa kufanya utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri na badala yake iwaruhusu kufanya utumishi wa kiraia usiohusisha mambo ya kijeshi. *

Dae-il Hong: Katika kesi 4 zilizowahusu watu 501 waliokataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri, Kamati ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (CCPR) ilifikia uamuzi kwamba Jamhuri ya Korea ilikiuka haki zao ilipowahukumu na kuwafunga gerezani. Kamati hiyo ilisema kwamba “haki ya kukataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri inahusiana kwa ukaribu na uhuru wa kufikiri, wa dhamiri, na wa kidini. Haki hiyo inamfanya kila mtu awe na ruhusa ya kutohusishwa katika utumishi wa lazima wa kijeshi iwapo utumishi huo haupatani na dini au imani ya mtu. Mtu hapaswi kulazimishwa avunje haki hiyo.” *

Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa liliangazia pia suala hili katika ripoti yake ya hivi karibuni iliyokuwa na kichwa “Ripoti ya utafiti kuhusiana na suala la kukataa kujiunga na utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri.” Ripoti hiyo inazungumzia kuhusu sheria ya kimataifa ambayo inawatetea wale wanaokataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri na inawalinda wasiadhibiwe au kushtakiwa mara kwa mara kama njia za kuwalazimisha wajiunge na utumishi huo. *

Serikali ya Korea imeitikiaje malalamiko hayo ya kimataifa?

Jengo la Mahakama Kuu

Philip Brumley: Serikali ya Korea haijatekeleza maamuzi ya Kamati ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa. Kwa hiyo imeshindwa kutii mikataba hiyo ya kimataifa na hata kukataa kutambua haki za msingi za wale wanaokataa kuingia jeshini kwa sababu ya dhamiri yao. Isitoshe, Mahakama ya Juu ya Korea Kusini na Mahakama ya Katiba ilipuuza maamuzi ya Kamati ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa kwa kukataa rufaa ya wale wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri. Bunge la Kitaifa la Korea halijaanzisha utumishi wa badala wa kiraia utakaowanufaisha wale wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri na halijaweka mikakati yoyote ya kuwalinda.

Kwa ujumla vijana hao Mashahidi wa Yehova wameathirikaje kwa kufungwa gerezani?

Dae-il Hong: Hao ni vijana wenye ujasiri. Serikali inapowaambia waingie jeshini wanajua kwamba watahukumiwa na kufungwa gerezani katika mfumo wa sasa wa utawala. Hata hivyo hawajifichi. Kabla ya kufungwa gerezani wao ni raia wazuri na wanadumisha mfano huo mzuri wakiwa gerezani. Inasikitisha kwamba wanapoachiliwa inakuwa vigumu kwao kuajiriwa katika makampuni makubwa au serikalini kwa sababu rekodi zinaonyesha waliwahi kufungwa gerezani. Wamepoteza mwaka mmoja na nusu hivi gerezani. Familia zao zimelazimika kuishi bila wao kwa kipindi chote hicho. Hayo ni mateso yasiyo ya lazima.

Je, Mashahidi wa Yehova nchini Korea wanastahili kuhukumiwa na kufungwa gerezani kama wahalifu kwa sababu ya kukataa utumishi wa lazima wa kijeshi?

Dae-il Hong: Hapana! Vijana hawa si wahalifu. Mashahidi wa Yehova wanajulikana duniani kote kuwa watu wanaopenda amani na wanaotii sheria za nchi wanamoishi na wako tayari kutumikia jamii. Wanatii mamlaka ya serikali, wanatii sheria, wanalipa kodi, na kuunga mkono miradi ya serikali ya kunufaisha nchi. Hivi majuzi hakimu mmoja wa mahakama ya wilaya wa Korea alimhukumu kijana mmoja Shahidi afungwe gerezani kwa sababu kijana huyo alikataa kutekeleza utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri yake. Hakimu huyo alimwambia kuwa hakukuwa na njia nyingine ila kumfunga gerezani. Kisha papo hapo hakimu huyo aliufunika uso wake kwa karatasi alizokuwa nazo na akaanza kulia. Inaonekana uamuzi aliotoa ulimtaabisha sana kwa kuwa haukupatana na haki. Waliohudhuria kikao hicho cha kesi walitambua ukosefu huo wa haki nao pia wakaanza kutiririkwa na machozi.

Philip Brumley: Kwa kweli huu ndio wakati ambapo serikali ya Korea inapaswa kusuluhisha tatizo hili la muda mrefu na kuanzisha mfumo utakaoheshimu haki za msingi za kibinadamu za wale wanaokataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri.

^ fu. 5 “Ripoti ya Baraza la Haki za Kibinadamu ya Universal Periodic Review Kuhusu Jamii ya Watu Walioajiriwa,” kikao kilichofanyika tarehe 12 Desemba 2012, A/HRC/22/10, ukurasa wa 7 na wa 22, fungu la 44 na la 124.53.

^ fu. 6 Jong-nam Kim na wengine dhidi ya Jamhuri ya Korea, namba ya mawasiliano 1786/2008, Maoni yaliyotolewa na Halmashauri mnamo tarehe 25 Oktoba 2012, ukurasa wa 7, fungu la 7.4

^ fu. 7 “Ripoti ya Baraza la Haki za Kibinadamu kuhusu utafiti wa suala la kukataa kujiunga na utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri,” ya tarehe 3 Juni 2013, A/HRC/23/22, ukurasa wa 3-8, fungu la 6-24; ukurasa wa 9, 10, fungu la 32, 33.

 

Pata Kujua Mengi Zaidi

MASWALI YANAYOULIZWA MARA NYINGI

Kwa Nini Mashahidi wa Yehova Hawaendi Vitani?

Ulimwenguni pote, inajulikana kwamba Mashahidi wa Yehova hawaendi vitani. Soma uone ni kwa nini sisi huchukua msimamo huo.