Hamia kwenye habari

FEBRUARI 19, 2015
KOREA KUSINI

Korea Kusini Yashutumiwa kwa Kuwafunga Watu Bila Misingi ya Kisheria

Korea Kusini Yashutumiwa kwa Kuwafunga Watu Bila Misingi ya Kisheria

Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Kibinadamu imeishutumu serikali ya Korea Kusini kwa kuwafunga gerezani bila misingi ya kisheria wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri na kwa kuwanyima haki ya kuwa na uhuru wa dhamiri. Huo ni uamuzi wa tano kutolewa na Kamati hiyo dhidi ya Korea Kusini kwa sababu ya kuwafunga wanaoongozwa na dhamiri, lakini kwa mara ya kwanza walifikia uamuzi wa kuwa vifungo hivyo “havina misingi ya kisheria.” *

Katika visa vinne vya awali vilivyohusisha jumla ya Mashahidi 501, Kamati hiyo ilipata kwamba Korea Kusini inakiuka haki ya uhuru wa kufikiri, dhamiri, na wa kidini wa Mashahidi kulingana na Kifungu cha 18 cha Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa (ICCPR). Uamuzi huu mpya wa Oktoba 15, 2014, uliotolewa kwa umma Januari 14, 2015, na uliohusisha vijana Mashahidi 50, * uliongeza maelezo zaidi. Kamati hiyo iliona kwamba kuwaadhibu wanaume hao kwa kuwafunga gerezani kwa kutumia haki yao ya msingi, serikali pia ilikiuka Kifungu cha 9 cha ICCPR, kinachokataza vifungo visivyo na misingi ya kisheria na kinatoa haki ya mtu kulipwa fidia. Kamati hiyo ilieleza kwamba “‘kufunga watu bila misingi ya kisheria’ . . . lazima kufafanuliwe zaidi ili kutie ndani vitendo visivyofaa [na] ukosefu wa haki.” Kwa hiyo Kamati hiyo iliamua kwamba “kuwahukumu kifungo cha gerezani kwa sababu ya kutumia haki ya uhuru wa kidini na dhamiri kulingana na kifungu cha 18 cha Mkataba” hakuna misingi ya sheria.

Daraka la Serikali la Kutatua Tatizo Hilo

Katika uamuzi wao, Kamati hiyo iliitaka serikali ya Korea Kusini kufuta kabisa kosa la uhalifu ambalo Mashahidi hao 50 walikuwa wamehukumiwa na kuwalipa fidia inayolingana. Pia, ilieleza kuwa serikali hiyo “ina daraka la . . . [kupitisha] sheria inayotoa haki ya kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri.” Ndani ya siku 180 baada ya kupitishwa kwa uamuzi huo, Serikali ya Korea Kusini inapaswa itoe “habari kuhusu hatua ilizochukua katika kutekeleza Maamuzi hayo.”

Korea Kusini imesisitiza kwamba haiwezi kuanzisha mpango wa utumishi wa badala kwa sababu eti ni hatari kwa usalama wa taifa na eti kwamba serikali haijaafikiana kuhusu suala hilo. Kwa mara ya tano, Kamati hiyo ilikataa sababu hizo, ikirejelea Maamuzi ya Kamati ya 2006. Katika Maamuzi hayo, Kamati hiyo ilieleza kuwa Korea Kusini “imeshindwa kuonyesha matokeo mabaya itakayopata ikiwa haki za wanaoongozwa na dhamiri zitazingatiwa kikamili.” Kuhusu kuathiri umoja na usawa katika jamii, Kamati hiyo iliona kuwa “kuheshimu imani na maamuzi yanayoongozwa na dhamiri ni hatua muhimu ya kuleta umoja na kuimarisha jamii yenye mchanganyiko wa watu.” Hivyo Kamati hiyo inasisitiza kuwa Korea Kusini haina haki ya kuwafunga gerezani wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri..

Kwa kuwafunga bila misingi ya kisheria wanaoongozwa na dhamiri, Korea Kusini inapinga kabisa ujuzi na misingi ya sheria za kimataifa zinazohusika katika suala hili.

Ingawa Korea Kusini ilitia sahihi mkataba wa ICCPR mwaka wa 1990, imekuwa ikikataa kutenda kulingana na wajibu ulio katika mkataba huo kuhusu wanaokataa kujiunga na jeshi. Na hata imeendelea kuwafunga gerezani mamia ya Mashahidi vijana kila mwaka. Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Kibinadamu imekuwa ikiwatetea wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri nchini humo. Tunasubiri kuona ikiwa serikali hiyo itabadili maoni yake kwa sababu ya shinikizo kutoka kwa mataifa mbalimbali na kukomesha vifungo visivyo na misingi ya kisheria na kuweka sheria zinazoheshimu dhamiri za wananchi.

^ fu. 2 Tazama CCPR Communication No. 2179/2012, Young-kwan Kim et al. dhidi ya Jamhuri ya Korea, Maamuzi ya Oktoba 15, 2014, fungu la. 7.5.

^ fu. 3 Katika picha juu, 30 kati ya Mashahidi vijana 50 wamesimama nje ya Mahakama Kuu ya Korea Kusini, ambapo walikata rufani ya kwanza.