Hamia kwenye habari

Hamia kwenye menyu ya pili

Mashahidi wa Yehova

Kiswahili

JULAI 7, 2015
KOREA KUSINI

Je, Mahakimu Nchini Korea Kusini Watakubali Viwango vya Kimataifa kwa Ajili ya Wanaokataa Kujiunga na Jeshi kwa Sababu ya Dhamiri?

Je, Mahakimu Nchini Korea Kusini Watakubali Viwango vya Kimataifa kwa Ajili ya Wanaokataa Kujiunga na Jeshi kwa Sababu ya Dhamiri?

Mahakama ya Katiba nchini Korea Kusini itachunguza tena ikiwa serikali inafuata katiba kwa kutotambua haki ya kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri. * Miaka minne iliyopita, yaani, mwaka 2011, Mahakama iliamua kwamba kulingana na Sheria ya Utumishi wa Kijeshi ya Korea Kusini, kuwaadhibu wanaokataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri hakuvunji katiba. Uamuzi kama huo ulitolewa mwaka 2004.

Sasa Mahakama itachukua hatua isiyo ya kawaida kwa kusikiliza kesi tatu kwa wakati mmoja za watu waliofungwa kwa sababu ya dhamiri mnamo Julai 9, 2015. Mashirika mbalimbali yametuma hati za maoni katika Mahakama hiyo ili kutetea haki ya kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri. Kwa kuwa sasa sheria za kimataifa zinawaruhusu watu kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri, nchi nyingi duniani zinahangaishwa na uamuzi wa Korea Kusini kukataa kutambua haki hiyo.

Mashirika ya Kimataifa Yazidi Kuangazia Suala Hilo

Kamati ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa imeitaka serikali ya Korea Kusini kufanya mabadiliko. Tangu mwaka 2006, kamati hiyo imeshughulikia kesi tano za watu 500 wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri * na kuamua kwamba lazima Korea Kusini iweke sheria itakayotetea haki ya kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri.

Shirika la Amnesty International linalotetea haki za binadamu lenye makao yake makuu London, lilisherehekea Siku ya Kimataifa ya Wanaokataa Kujiunga na Jeshi kwa Sababu ya Dhamiri kwa kuchapisha habari mnamo Mei 13, 2015 ambayo inazungumzia jinsi serikali ya Korea Kusini inavyowatendea wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri. Habari hiyo ilizungumzia hasa vijana Mashahidi wa Yehova waliofikisha umri wa kujiunga na jeshi na matatizo wanayokabili kutokana na sheria inayotumika sasa nchini Korea Kusini. Juma hilohilo, vyombo kadhaa vya habari vya kimataifa kama CNN na The Washington Post, vilizungumzia kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri na vijana Mashahidi waliochukua msimamo huo.

Changamoto Wanayokabili Mahakimu

Shahidi wa Yehova anapokataa kusajiliwa jeshini nchini Korea Kusini, kwa kawaida mahakimu humhukumu kwa kosa la kukataa utumishi huo. Hata hivyo, kadiri muda unavyoenda mahakimu hawafurahii kuwahukumu vijana ambao “kosa” pekee walilofanya ni kushikamana kwa unyoofu na imani ya dini yao. * Pindi moja, hakimu aliyesikiliza kesi katika Mahakama ya Wilaya ya Suwon alilia alipokuwa akitoa hukumu ya kijana mmoja Shahidi, kwa kuwa kulingana na sheria hakimu huyo hakuwa na njia nyingine zaidi ya kumhukumu kuwa na hatia.

Mei 12, 2015, hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Gwangju aliwaondolea hatia washtakiwa wa kesi ya kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri. Hakimu alitoa uamuzi huo kwa sababu alisumbuliwa na dhamiri alipokuwa akisikiliza kesi hiyo ya Mashahidi wa Yehova watatu. Akiwa na lengo la kuchochea mabadiliko, aliwaambia hivi: “Ninachofanya kwa sasa ni kuwasha njiti ya kiberiti nikitumaini kwamba hatimaye mtaweza kufanya itokeze moto mkubwa.” Hata hivyo, mwendesha mashtaka wa kesi hiyo alikata rufaa dhidi ya uamuzi huo.

Badala ya kuwahukumu wanaoshtakiwa kwa sababu ya dhamiri zao, mahakimu saba wa mahakama za wilaya wameagiza kwamba kesi hizo zisikilizwe katika Mahakama ya Katiba, licha ya uamuzi wa Mahakama hiyo wa mwaka 2004 na 2011. Mahakimu hao walikataa kumpa adhabu ya kifungo cha gereza kijana mmoja ambaye alishtakiwa kwa sababu tu ya kufuata dhamiri yake. Katika kesi moja kati ya hizo, Hakimu Young-hoon Kang wa Mahakama ya Wilaya ya Seoul Kaskazini alisema kwamba kuwaadhibu wale wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri ni “sawa na kuwanyima haki zao na utambulisho wao. Kwa kweli, jambo hilo linakiuka haki ya binadamu ya kuheshimiwa.”

Mahakimu Wachochewa “Kushinikiza Mahakama”

Desemba 2014, Baraza la Mawakili la Korea lilifanya mkutano ili kuzungumzia suala la kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri. Katika hotuba ya msingi, Hakimu wa zamani wa Mahakama Kuu, Su-an Cheon, aliita uamuzi wa Kamati ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa na maazimio ya Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa dhidi ya Korea Kusini kuwa “aibu ya taifa.” Alisema kwamba “si sawa kuwafunga gerezani mamia ya vijana” na aliwasihi mahakimu na wanasheria “kushinikiza mahakama” ili zitoe uamuzi kulingana na viwango vya kimataifa.

Bi. Cheon alimalizia hotuba yake kwa kusema: “Tunapaswa kuanzisha utumishi wa badala haraka iwezekanavyo. . . . Utumishi wa badala ukianza kutumiwa, hilo litakuwa jambo la pekee katika historia ya Korea na mafanikio makubwa katika suala la haki za binadamu chini ya utawala wa rais wa kwanza mwanamke. Kwa kufanya hivyo tu ndiyo tutaweza kufuta shutuma tunazopata za kuwa nchi isiyofuata haki za binadamu.”

Je, Mahakama ya Katiba Itafuata Viwango vya Kimataifa?

Kwa makumi ya miaka, maelfu ya Mashahidi wa Yehova nchini Korea Kusini, wameendelea kufungwa kwa sababu ya kufuata dhamiri zao zinazotegemea imani. Wanaposubiri uamuzi wa Mahakama wanajiuliza: Je, uamuzi wa haki wa Mahakama ya Katiba utatumiwa kuwasaidia wale wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri? Je, Korea Kusini itatenda kulingana na viwango vya haki za binadamu vinavyotambuliwa kimataifa?

^ fu. 2 Jamhuri ya Korea haitambui haki ya kukataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri. Kwa miaka 60 iliyopita, nchi hiyo imewafunga gerezani Mashahidi wa Yehova zaidi ya 18,000 waliokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya kushikilia kwa unyoofu imani yao ya dini. Ili kupata orodha ya karibuni zaidi ya Mashahidi waliofungwa gerezani nchini Korea Kusini, soma habari yenye kichwa “Wamefungwa kwa Sababu ya Imani Yao—Korea Kusini.”

^ fu. 5 Communications Nos. 1321/2004 na 1322/2004, U.N. Doc. CCPR/C/88/D/1321-1322/2004, 3 Novemba 2006; Communications Nos. 1593 hadi 1603/2007, U.N. Doc. CCPR/C/98/D/1593-1603/2007, 23 Machi 2010; Communications No. 1642-1741/2007, U.N. Doc. CCPR/C/101/D/1642-1741/2007, 24 Machi 2011; Communication No. 1786/2008, U.N. Doc. CCPR/C/106/D/1786/2008, 25 Oktoba 2012; Communication No. 2179/2012, U.N. Doc. CCPR/C/112/D/2179/2012, 15 Oktoba 2014.