Serikali ya Korea Kusini imewafunga mamia ya watu wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri. Pia, inawaadhibu wanaume wanaokataa kujiunga na jeshi ingawa wameandikishwa kwenye orodha ya askari wa akiba.

Tangu alipokuwa mvulana akiishi nchini Korea Kusini, Dong-hyuk Shin alitambua kwamba siku moja angeambiwa ajiunge na jeshi. Alipoitwa atimize wajibu huo wa kijeshi alikubali na mwaka wa 2005 alikamilisha utumishi wa kijeshi na kuruhusiwa kuondoka akiwa na rekodi nzuri sana. Moja kwa moja aliorodheshwa kwenye orodha ya askari wa akiba, akitarajia kuitwa mara kwa mara ili kupata mafunzo ya kijeshi yanayotolewa kwa askari wa akiba kwa miaka nane iliyofuata.

Muda mfupi baada ya kuachiliwa jeshini, Bw. Shin alijifunza Biblia. Ujumbe wa amani aliojifunza uligusa dhamiri yake na kumchochea kukataa utumishi wa kijeshi. Alipoitwa kwa mara nyingine Machi 2006 kwa ajili ya mafunzo ya askari wa akiba, aliwaeleza maofisa wa jeshi kwamba hangeweza kukubali kwa sababu dhamiri yake haikumruhusu kufanya hivyo.

Hakuna Uhuru wa Dhamiri

Korea Kusini haitambui haki ya wale wanaokataa kujiunga na utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri. Karibuni imewaagiza zaidi ya Mashahidi 40 wa Yehova wafike ili kupokea mafunzo ya askari wa akiba. Mashahidi hao tayari walikuwa wametangaza kwamba wanakataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri.

Jeshi lilipuuza ombi la Bw. Shin la kutohusishwa katika mafunzo ya kijeshi ya askari wa akiba na katika mwaka wa 2006 alitumiwa jumla ya maagizo 30 kwamba anapaswa kuripoti jeshini. Bw. Shin aliendelea kupokea barua hizo kwa miaka saba iliyofuata. Kwa ujumla, tangu Machi 2006 hadi Desemba 2013, aliitwa mara 118 kwa ajili ya mafunzo ya kijeshi ya askari wa akiba. * Kwa kuwa Bw. Shin alikataa kwa heshima kila mara alipoitwa, alifunguliwa mashtaka na kukamatwa mara 49, akafikishwa mahakama mara 69 kutia ndani mahakama za rufaa, na alihukumiwa mahakamani mara 35.

“Hakuna Njia Nyingine”

Mahakama hazikupinga kwamba uamuzi wa Bw. Shin kushikamana na dhamiri yake ni wa kweli. Katika uamuzi wa Oktoba 7, 2014, Mahakama ya Wilaya ya Ulan ilisema hivi: “Inaeleweka kwamba [Dong-hyuk Shin], baada ya kuwa Shahidi wa Yehova, hana njia nyingine ila kukubali kufanya kosa lilelile linalohusika katika kesi hii, kwa sababu anatambua ni vigumu kwake upinzani uliopo kati ya wajibu wa kijeshi, dhamiri yake, na imani yake ya kidini.”

Ingawa mahakama hiyo ya wilaya ilionyesha inatambua hali ngumu aliyokabili Bw. Shin, mahakama za Korea Kusini hazina uwezo wa kikiukamatakwa ya sheria ya utumishi wa kijeshi. Bw. Shin ametozwa na mahakama mbalimbali zaidi ya won milioni 16 (ambazo ni sawa na dola 13,322 za Marekani) na amehukumiwa mara sita vifungo vya gerezani na kila kifungo alichohukumiwa kilikuwa cha kipindi kisichopungua miezi sita. Vifungo hivyo vilibadilishwa kuwa vifungo vyenye masharti. Katika kesi moja, mahakama ilimwamuru afanye utumishi wa kijamii kwa saa 200.

Bw. Shin anasema hivi: “Nilihuzunika na kuwa na mahangaiko sana. Ilionekana kwamba jaribu hili halitawahi kwisha. Kwenda mara nyingi mahakamani kulisababisha mkazo kwa familia yangu. Nafikiri mama yangu aliteseka sana katika kipindi hicho cha miaka tisa, na mahangaiko yameathiri afya yake. Nilivunjika moyo sana kutambua jinsi anavyohuzunika kwa sababu ya hali niliyokabili. Na pia niliathirika kiuchumi. Kuitwa tena na tena jeshini na kufikishwa mahakamani na kufunguliwa kesi kulinilazimisha nibadili kazi mara saba kwa sababu nilikosa kufika kazini mara nyingi nilipokuwa nikienda mahakamani.”

Kukiuka Masharti ya Mkataba wa Kimataifa

Bw. Shin alikata rufaa katika kesi zake zote kwa mahakama mbalimbali nchini Korea Kusini, lakini hakupata msaada wowote—Mahakama Kuu ilikataa rufaa zake mara nne. Baada ya kukosa suluhisho la kisheria nchini Korea Kusini, Bw. Shin alifungua kesi kwenye Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Kibinadamu mnamo Juni 2016. Alidai kwamba kwa kumwita mara nyingi jeshini, kuteswa, na kufikishwa mahakamani, Korea Kusini ilikiuka wajibu wake wa kuheshimu Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa. Madai yake yalilenga mambo matatu:

  • Kulingana na sheria za kimataifa, kumwagiza mtu anayekataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri aripoti kwa ajili ya utumishi wa kijeshi na kisha kumwadhibu tena na tena ni kukiuka haki yake ya kuwa na kesi inayoendeshwa kwa haki.

  • Kuagizwa mara nyingi kufika kwa ajili ya mafunzo ya kijeshi na mateso yaliyofuata yanathibitisha kwamba lengo la wenye mamlaka wa nchini Korea ni kumlazimisha afanye utumishi wa kijeshi. Kumsumbua Bw. Shin mara nyingi kwa kumshtaki mahakamani na kumwona kuwa mhalifu kwa kufuata dhamiri yake ya kidini ni adhabu iliyomvunjia heshima.

  • Kwa sababu kukataa kwa Bw. Shin kujiunga na utumishi wa kijeshi kunategemea hasa imani yake ya kidini, aliwasilisha malalamiko kwamba haki yake ya uhuru wa dhamiri na wa kuabudu ilikuwa imekiukwa.

Tumaini la Kupata Kitulizo

Bw. Shin anatumaini kwamba malalamiko yake yatasikilizwa kwa haki kwa sababu Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Kibinadamu imetoa uamuzi mara nyingi kwamba Korea Kusini inapaswa kuheshimu haki ya wale wanaokataa kujiunga na utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri. * Anatarajia uamuzi ambao utatambua hali ngumu wanayokabili askari wa akiba. Bw. Shin anasema hivi: “Sijuti kwa sababu ya msimamo wangu wa kufuata kanuni za dini na dhamiri yangu, lakini ninahuzunishwa na jinsi ambavyo nimetendewa. Ninatumaini kwamba serikali ya Korea Kusini itatambua haki ya mtu ya kukataa utumishi wa kitaifa ambao unapingana na dhamiri yake.” Mashahidi wa Yehova nchini Korea Kusini na ulimwenguni pote wana maoni kama hayo.

^ fu. 7 Katika mwaka wa 2006, Dong-hyuk Shin aliagizwa aripoti jeshini mara 30, mara 35 katika mwaka wa 2007, mara 15 katika mwaka wa 2008, mara 9 katika mwaka wa 2009, mara 17 katika mwaka wa 2010, na mara 12 katika mwaka wa 2011. Si takwa kwa askari wa akiba kupata mazoezi zaidi ya kijeshi katika kipindi cha miaka miwili ya mwisho, hivyo Bw. Shin hakuitwa mwaka 2012 na 2013.

^ fu. 18 Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Kibinadamu imeshughulikia kesi tano ambazo imefikia mkataa kwamba Korea Kusini ilikiuka Kifungu 18, “haki ya uhuru wa mawazo, dhamiri, na dini”: Yeo-bum Yoon na Myung-jin Choi dhidi ya Jamhuri ya Korea, Mawasiliano Na. 1321-1322/2004, U.N. Doc. CCPR/C/88/D/1321-1322/2004 (Novemba 3, 2006); Eu-min Jung et al. dhidi ya Jamhuri ya Korea, Mawasiliano Na. 1593-1603/2007, U.N. Doc. CCPR/C/98/D/1593-1603/2007 (Machi 23, 2010); Min-kyu Jeong et al. dhidi ya Jamhuri ya Korea, Mawasiliano Na. 1642-1741/2007, U.N. Doc. CCPR/C/101/D/1642-1741/2007 (Machi 24, 2011); Jong-nam Kim et al. dhidi ya Jamhuri ya Korea, Mawasiliano Na. 1786/2008, U.N. Doc. CCPR/C/106/D/1786/2008 (Oktoba 25, 2012); na Young-kwan Kim et al. dhidi ya Jamhuri ya Korea, Mawasiliano Na. 2179/2012, U.N. Doc. CCPR/C/112/D/2179/2012 (Oktoba 15, 2014).