Hamia kwenye habari

ULIMWENGUNI POTE

Wamefungwa kwa Sababu ya Imani Yao​—Crimea

Wamefungwa kwa Sababu ya Imani Yao​—Crimea

Upinzani mkali unaoendelea nchini Urusi umeenea na kufika Crimea. Nchini Urusi serikali imefunga mashirika ya Mashahidi, na imeonyesha waziwazi kwamba imekusudia kuondoa kabisa ibada zozote zinazofanywa ingawa zinafanywa kwa amani. Tangu marufuku ya Aprili 2017, wenye mamlaka nchini Urusi wamewavamia Mashahidi wengi wanakokutanika pamoja nchini humo, na hilo limesababisha Mashahidi wengi kukamatwa na kufungwa. Unyanyasaji wa aina hiyohiyo unatumika dhidi ya Mashahidi wa Yehova nchini Crimea.

Uvamizi Uliofanyika Katika Mji wa Dzhankoy Novemba 2018

Sergey Filatov

Uvamizi wa kwanza mkubwa nchini Crimea ulifanyika Novemba 15, 2018, huko Dzhankoy, wakati ambapo polisi pamoja na wanajeshi waliokadiriwa kuwa kama 200 hivi walivamia nyumba nane ambamo vikundi vidogo vya Mashahidi vilikuwa vimekutanika ili kusoma na kuzungumzia Biblia. Maofisa 35 hivi waliofunika nyuso zao na waliokuwa na bunduki mikononi walivamia nyumba ya Sergey Filatov, ambako kulikuwa na kikundi cha Mashahidi sita. Mashahidi hao waliingiwa na hofu sana kwa sababu ya uvamizi huo wa kikatili. Wavamizi hao walimsukuma na kumbana mwanamume fulani mwenye umri wa miaka 78 ukutani, wakamlazimisha alale chini na kumfunga pingu, kisha wakampiga vibaya hivi kwamba ilibidi apelekwe hospitalini. Wanaume wengine wawili wenye umri mkubwa walishtuka sana hivi kwamba wakalazimika kukimbishwa hospitali kwa sababu ya kupanda kwa shinikizo la damu. Inasikitisha kwamba mwanamke mmoja aliyekuwa mjamzito alipovamiwa nyumbani kwake aliingiwa na hofu hadi mimba yake ikatoka.

Baada ya uvamizi huo, Bw. Filatov alifunguliwa mashtaka ya uhalifu chini ya Kifungu 282.2(1) cha Sheria ya Uhalifu ya Urusi kwa kosa la kupanga shughuli za “shirika lenye msimamo mkali.” Machi 5, 2020, mahakama ya wilaya nchini Crimea alimfunga Bw. Filatov kifungo cha miaka sita katika gereza la wahalifu. Baada ya hukumu yake kutangazwa, alipelekwa gerezani moja kwa moja. Novemba 2020, mawakili wa Bw. Filatov waliwasilisha ombi kwenye Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu kwa niaba yake. Bw. Filatov ni mwanaume aliyeoa na mwenye watoto wanne, na wawili kati yao bado wanamtegemea.

Uvamizi Mwingine wa Nyumba za Mashahidi

Artem Gerasimov

Machi 20, 2019, maofisa wa FSB walivamia nyumba nane za Mashahidi wa Yehova katika majiji ya Alupka na Yalta yaliyoko Crimea. Msako huo ulipokuwa ukiendelea, maofisa hao walichukua Biblia, kompyuta, na vifaa vya kielektroni. Baada ya hapo, Bw. Artem Gerasimov alishtakiwa kupanga utendaji wa kikundi chenye msimamo mkali kwa sababu tu alikutana na wengine kuzungumzia Biblia. Alihukumiwa kifungo cha miaka sita gerezani na amepangiwa kuachiliwa Juni 2026.

Viktor Stashevskiy

Jioni ya Juni 4, 2019, maofisa wa kitengo maalumu walivamia nyumba kumi za Mashahidi wa Yehova huko Sevastopol. Wakati wa uvamizi huo, Viktor Stashevskiy alikamatwa na baadaye kuachiliwa lakini akaamriwa asiondoke katika eneo hilo. Mbali na hilo, Bw. Stashevskiy alishtakiwa kwa kupanga utendaji wa kikundi kilicho na msimamo mkali na akahukumiwa kifungo cha miaka sita na nusu gerezani. Ataachiliwa Julai 2027.

Igor Shmidt

Oktoba 1, 2020, nyumba tisa za Mashahidi wa Yehova zilivamiwa katika eneo la Sevastopol, Crimea. Kesi ilifunguliwa dhidi ya Igor Shmidt. Oktoba 22, 2021, Mahakama ya Wilaya ya Gagarinskiy iliyoko Sevastopol ilimhukumu Bw. Shmidt kifungo cha miaka sita gerezani.

Mfuatano wa Matukio

 1. Oktoba 22, 2021

  Bw. Shmidt anahukumiwa kifungo cha miaka sita gerezani.

 2. Oktoba 1, 2020

  Nyumba tisa zavamiwa katika eneo la Sevastopol. Igor Shmidt anakamatwa na kuwekwa mahabusu.

 3. Juni 4, 2020

  Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Crimea yamhukumu Bw. Gerasimov miaka sita gerezani.

 4. Machi 5, 2020

  Bw. Filatov ahukumiwa kifungo cha miaka sita katika gereza la wahalifu.

 5. Juni 4, 2019

  Maofisa wa kikosi maalumu walivamia nyumba kumi jijini Sevastopol. Bw. Stashevskiy alihukumiwa kwa kupanga utendaji wa kikundi kilicho na msimamo mkali.

 6. Machi 20, 2019

  Maofisa wa FSB wavamia nyumba nane huko Alupka na Yalta. Bw. Gerasimov ahojiwa na baadaye kushtakiwa kupanga utendaji wa kikundi chenye msimamo mkali.

 7. Novemba 15, 2018

  Nyumba nane zavamiwa na polisi pamoja na wanajeshi zaidi ya 200 mjini Dzhankoy, kutia ndani nyumba ya Bw. Flatov.