Hamia kwenye habari

JULAI 6, 2017
KAZAKHSTAN

Kazakhstan Imesitisha Utendaji wa Makao Makuu ya Mashahidi Nchini Humo

Kazakhstan Imesitisha Utendaji wa Makao Makuu ya Mashahidi Nchini Humo

Juni 29, 2017, mahakama jijini Almaty, Kazakhstan, ililitoza faini shirika la Kituo cha Kikristo cha Mashahidi wa Yehova Nchini Kazakhstan (Christian Center of Jehovah’s Witnesses in Kazakhstan) (Kituo) na kusitisha utendaji wake wote kwa muda wa miezi mitatu. Uamuzi huo wa mahakama unategemea madai yaliyotolewa wakati wa ukaguzi kwamba kituo kinaonekana na wenye mamlaka kuwa sehemu rahisi kushambuliwa na magaidi, na ingawa kituo kina kamera 20 za ulinzi, kinahitaji kuongeza kamera tatu zaidi. Vladimir Voyevodin, mwakilishi wa Mashahidi wa Yehova nchini Kazakhstan, alisema hivi: “Uamuzi wa kusitisha utendaji wote wa Kituo hicho ni hukumu kubwa sana kwa madai hayo ya ukiukwaji wa sheria. Tunakata rufaa kupinga uamuzi huo ambao unaonekana ulikuwa umechochewa na ubaguzi wa kidini.”

Wenye Mamlaka Kuingilia Rasmi Utendaji wa Kituo

Kabla ya uamuzi wa Juni 29 kutolewa na Hakimu N. M. Pakirdinov wa mahakama hiyo, wenye mamlaka walivamia Kituo hicho wakiwa na barua inayowaruhusu kufanya ukaguzi wa usalama wa kituo. Uvamizi huo ulitokea Mei 17, 2017, na uliongozwa na Idara ya Usalama wa Taifa (ambayo zamani ilijulikana kama KGB) na maofisa zaidi ya 30, kutia ndani polisi waliopata mafunzo maalumu ya kukabiliana na hatari yoyote ambao waliziba nyuso zao na walibeba silaha nzito. Walidai kwamba walipewa agizo la kukagua majengo yote ya umma ambayo yanaweza kushambuliwa kwa urahisi na magaidi wakati wa maonyesho ya kimataifa ya mwaka wa 2017, ambayo yalianza kufanyika Juni 2017, kwenye mji mkuu Astana. Mashahidi tayari wamefuata maagizo yaliyotolewa kwenye ukaguzi wa awali wa usalama, na kituo kilichukua hatua haraka kurekebisha madai ya ukiukwaji wa sheria yaliyotolewa kwenye ukaguzi mwingine uliofanyika, Juni 5, 2017.

Mei 17, 2017, uvamizi kwenye Kituo

Mashahidi walipotambua kwamba maonyesho ya kimataifa ya mwaka wa 2017 yangefanyika jijini Astana, walipanga kufanya kusanyiko la pekee la siku tatu ili kufanya wageni wengi watakaofika kutoka mataifa mbalimbali wahudhurie. Hata hivyo, wenye mamlaka walivuruga mikataba iliyofanywa ya kukodi jengo litakalotumiwa kwa ajili ya kusanyiko, na mkataba wa kukodi jengo hilo ukabatilishwa. Kwa hiyo, wajumbe 1,500 kutoka Marekani na Ulaya, pamoja na Mashahidi wengine nchini walifanya kusanyiko kwenye jengo ambalo ni mali ya Kituo. Siku mbili za kwanza za kusanyiko hilo, polisi waliwachelewesha kwa saa tatu wajumbe zaidi 900 kutoka hoteli walizopanga, wakati maofisa walipokuwa wakikagua vibali vya madereva wa basi. Kituo kilipeleka malalamiko kwenye Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Almaty. Ingawa ofisi hiyo ya mwendesha mashtaka haikutoa jibu lolote, polisi hawakuwasumbua Mashahidi katika siku ya tatu ya kusanyiko. Hata hivyo, siku nne tu baada ya kusanyiko kumalizika, mahakama ya utawala jijini Almaty ilitoa uamuzi wake wa kusitisha utendaji wa Kituo.

Juni 23, 2017, polisi wakiwazuia wajumbe kutoka nchi nyingine kwenda kusanyikoni

Kutunga Matatizo Kupitia Sheria

Tangu Desemba 2012, serikali ya Kazakhstan imeendelea kuzuia uhuru wa ibada wa Mashahidi wa Yehova nchini kote. Serikali iliwatoza faini kubwa Mashahidi wa Yehova zaidi ya 80 kwa madai ya kufanya “kazi ya umishonari” bila kusajiliwa.

Januari 2017, wenye mamlaka nchini Kazakhstan walifungua kesi mbili za uhalifu dhidi ya Mashahidi wa Yehova kwa sababu ya kuwaeleza wengine imani yao ya dini. Mnamo Mei, Teymur Akhmedov alihukumiwa kwa sababu ya kufanya utendaji wa kidini na sasa anatumikia kifungo cha miaka mitano gerezani. Katika kisa kingine, polisi wanamchunguza Shahidi mmoja kwa madai ya kuchochea chuki ya kidini kwa sababu alimpa mtu chapisho lililopigwa marufuku nchini Urusi kwa madai kwamba ni lenye “msimamo mkali.”

Je, Kazakhstan Itaiga Jinsi Urusi Inavyowatendea Mashahidi wa Yehova?

Mashahidi wamekutana mara nyingi na Idara ya Mambo ya Kidini ili kuzungumzia haki yao ya kuabudu kwa uhuru lakini hilo halikusaidia sana. Hata hivyo, Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu (GPO), ilipoanza kufuatilia kesi ya Shahidi wa Yehova anayeitwa Andrey Korolev ambaye alishtakiwa kwa kuwaeleza wengine imani yake hadharani, ndipo Mahakama Kuu ilipochukua hatua kuhusiana na kesi hiyo. Katika uamuzi wake wa Juni 1, 2017, mahakama ilitoa hukumu kwamba Bw. Korolev hana hatia, ikitambua kwamba haki ya uhuru wa ibada inatoa uhuru wa kutangaza imani kwa amani. Ingawa Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu ilikuwa imewahakikishia Mashahidi kwamba watasambaza habari za ushindi huo kwenye mahakama nyingine, lakini mahakama za chini bado zimekataa kutumia maamuzi hayo na zinaendelea kuwahukumu Mashahidi wa Yehova kwa kile wanachodai kuwa “kufanya kazi ya umishonari bila kusajiliwa.”

Gregory Allen, Wakili wa Mashahidi wa Yehova, alisema hivi: “Licha ya matukio ya karibuni, tunatumaini kwamba mahakama za chini na maofisa wa kusimamia sheria watazingatia uamuzi wa Mahakama Kuu uliotolewa Juni 1, 2017. Inasikitisha sana kuona Kazakhstan ikifuata mfano wa Urusi wa kutumia mashtaka yasiyo na msingi kuvuruga haki inayotambuliwa kimataifa ya uhuru wa ibada. Tunahofu kwamba uamuzi wa Juni 29 wa kusitisha utendaji wa Kituo utakuwa na matokeo mabaya kuliko inavyotazamiwa, na tunatafuta haki katika rufaa yetu kupinga uamuzi huo.”

Mashahidi wa Yehova ulimwenguni pote wanahangaishwa sana na mambo yanayoendelea ambayo yanaonyesha kwamba wenye mamlaka wanapanga kuwapiga marufuku waabudu wenzao nchini Kazakhstan, kama ilivyokuwa kwa Mashahidi wa Yehova nchini Urusi.