Hamia kwenye habari

MEI 3, 2017
KAZAKHSTAN

Kazakhstan Inakandamiza Uhuru wa Ibada na Kumhukumu Teymur Akhmedov

Kazakhstan Inakandamiza Uhuru wa Ibada na Kumhukumu Teymur Akhmedov

Mei 2, 2017, mahakama ya Astana ilimhukumu Teymur Akhmedov kifungo cha miaka mitano gerezani kwa kosa la kuwahubiria wengine kuhusu imani yake. Yeye ndiye Shahidi wa kwanza wa Yehova nchini Kazakhstan tangu nchi hiyo ipate uhuru mwaka wa 1991, ambaye amehukumiwa kama mhalifu kwa sababu tu ya kushiriki utendaji wake wa kidini.

Bw. Akhmedov amekuwa mahabusu kwa zaidi ya miezi mitatu licha ya jitihada za kimataifa za kuomba aachiliwe mpaka wakati wa kusikiliza kesi yake. Ana umri wa miaka 61, ameoa na ana watoto watatu, pia anasumbuliwa na matatizo ya kiafya.

Adhabu Inatishia Uhuru wa Ibada

Mateso ya Bw. Akhmedov yalianza Januari 2017 wakati polisi wa siri wa Kazakhstan, Kamati ya Usalama wa Taifa (KNB), walipomkamata kwa madai ya uwongo kwamba alikiuka Kifungu cha 174(2) cha Sheria ya Kazakhstan Kuhusu Makosa ya Uhalifu. KNB walimshtaki kwa “kuchochea. . . chuki ya kidini” kwa kuwaeleza wengine imani yake wakiwa faraghani.

Hakimu Talgat Syrlybayev alidai kwamba maneno ya Bw. Akhmedov yalionyesha alikuwa “akichochea mgawanyiko wa kidini” na akieneza “habari za kujitenga, na kuonyesha kwamba wananchi fulani ni bora kuliko wengine kwa msingi wa dini zao.” Hakimu huyo pia alimpiga marufuku Bw. Akhmedov kushiriki hasa “utendaji wa kidini” kwa miaka mitatu—hiyo inamaanisha ibada yake imepigwa marufuku.

Philip Brumley, wakili mkuu wa Mashahidi wa Yehova, alisema hivi: “Wenye mamlaka wametumia sheria vibaya kabisa. Mwaka wa 2016, wanaume kadhaa walimwalika Teymur kwenye nyumba yao kwa ajili ya mazungumzo kuhusu imani yake. Pia, walikwenda nyumbani kwake. Hata hivyo, Teymur hakujua kwamba mazungumzo yao yalikuwa yakirekodiwa kisiri na yangetumiwa baadaye kumshtaki kwa madai yasiyo ya kweli. Hilo linaonyesha kwamba wenye mamlaka wako tayari kufanya chochote kuzuia na kuufanya utendaji wa kidini wenye amani kuwa kosa. Hiyo si haki kabisa.”

Isitoshe, familia ya Bw. Akhmedov ina wasiwasi kuhusu afya yake. Anaugua ugonjwa unaodhaniwa kuwa kansa kwa kuwa ana uvimbe unaotoa damu, lakini wenye mamlaka wamekataa kumruhusu Bw. Akhmedov atumikie kifungo cha nyumbani badala ya gerezani na pia hawampi matibabu ambayo anahitaji haraka sana. Wakili wake amepeleka malalamiko kwenye Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Vifungo Visivyo vya Haki, kwa Katibu Maalumu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia uhuru wa ibada na imani, na kwa Katibu Maalumu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia haki ya uhuru wa kukusanyika kwa amani na kushirikiana wengine.

Je, Uhuru wa Ibada Utaendelea Kuwepo Nchini Kazakhstan?

Mashahidi wa Yehova nchini Kazakhstan wamekabili changamoto nyingi katika kufanya utendaji wao wa kidini. Hata hivyo, kifungo kisichozingatia haki alichohukumiwa Bw. Akhmedov ni jambo jipya na ni shambulizi la kushtua dhidi ya ibada yao. Wawakilishi wa Mashahidi wanaendelea kuwasihi wenye mamlaka nchini Kazakhstan waheshimu mikataba ya kimataifa kwa kuunga mkono haki ya msingi ya uhuru wa ibada bila kuingiliwa na wenye mamlaka.