Mashahidi wa Yehova walianza utendaji wao katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) tangu miaka ya 1940. Wamekabili vita, kupigwa marufuku na serikali na mashambulizi makali kutoka kwa washiriki wa dini nyingine.

Upinzani wa serikali ulikoma rasmi mwaka wa 1993 baada ya Mahakama Kuu kuondoa marufuku dhidi ya utendaji wa kidini wa Mashahidi. Leo Mashahidi wa Yehova wana uhuru wa ibada na serikali haiwasumbui. Hata hivyo, baadhi ya vikundi vya kidini vinaendelea kuwasumbua au kuwanyanyasa Mashahidi. Washiriki wa dini ya kikabila iitwayo Kimbilikiti, wamewateka na kuwashambulia Mashahidi. Mara nyingi, wenye mamlaka wa maeneo hayo hawachukui hatua yoyote dhidi ya matendo hayo ya kihalifu kwa kuwa baadhi yao ni wafuasi wa Kimbilikiti. Wawakilishi wa Mashahidi wa Yehova wamepeleka mahakama kuu malalamiko yao dhidi ya ukosefu huo wa haki.

Pia, shule nyingi za umma nchini DRC ziko chini ya usimamizi wa mashirika ya kidini. Kwa sababu hiyo, shule nyingi zimewafukuza wanafunzi walio Mashahidi kwa sababu ya kukataa kushiriki katika utendaji wa kidini shuleni. Katika mwaka wa 2013, Waziri wa Elimu alitoa sheria kwa shule zote nchini humo iliyopiga marufuku ubaguzi wa kidini. Sheria hiyo na nyingine mpya ya elimu, imefanya shule nyingi kuwarudisha shule watoto Mashahidi na kuwapa diploma ambazo mwanzoni wanafunzi Mashahidi walikatiliwa kupewa.