Julai 8, 1985, ilikuwa tu siku nyingine ya kwenda shuleni kwa watoto watatu kutoka mji mdogo ulio Kerala, eneo la kusini magharibi mwa India. Lakini siku hiyo, mwalimu mkuu aliagiza wimbo wa taifa, “Jana Gana Mana,” uimbwe darasani. Wote walipaswa kusimama na kuimba. Lakini Bijoe mwenye umri wa miaka 15 na wadogo zake wa kike, Binu Mol (mwenye miaka 13) na Bindu (mwenye miaka 10), hawakufanya hivyo. Kwa kuwa wao ni Mashahidi wa Yehova, dhamiri zao hazikuwaruhusu kuimba kwa sababu waliamini kabisa kwamba kufanya hivyo ni namna ya ibada ya sanamu na ni kukosa uaminifu kwa Mungu wao, Yehova.

V. J. Emmanuel, baba ya watoto hao, alizungumza na mwalimu mkuu na walimu wengine wenye mamlaka, na walikubali watoto hao waendelee na masomo bila kulazimika kuimba wimbo huo. Lakini mfanyakazi mmoja wa shule hiyo alisikia mazungumzo hayo na kutoa ripoti. Hatimaye habari hiyo ilimfikia Mbunge aliyeamua kuiwasilisha Bungeni kwa sababu aliona tendo hilo si la kizalendo. Baada ya muda mfupi, mkaguzi mmoja wa shule mwenye wadhifa alimwagiza mwalimu mkuu awafukuze shule watoto hao ikiwa watakataa kuimba wimbo wa taifa. Bw. Emmanuel aliwasihi sana wenye mamlaka shuleni wawaruhusu watoto wake warudi shuleni, bila mafanikio. Hivyo akafungua kesi kwenye Mahakama Kuu ya Kerala. Baada ya kushindwa kwa kesi hiyo, alikata rufani kwenye Mahakama Kuu ya India.

Mahakama Kuu Yatetea Haki za Kikatiba

Agosti 11, 1986, Mahakama Kuu ya India ilipinga uamuzi uliotolewa na Mahakama Kuu ya Kerala katika kesi ya Bijoe Emmanuel dhidi ya Jimbo la Kerala. Mahakama iliamua kwamba kuwafukuza watoto hao kwa msingi wa “imani ya kidini” kulikiuka Katiba ya India. Jaji O. Chinnappa Reddy alisema hivi: “Hakuna sheria yoyote . . . inayomlazimisha mtu kuimba.” Mahakama iliona kuwa haki ya uhuru wa kusema na kujieleza pia ilihusisha haki ya kubaki kimya na kwamba kusimama wakati wa wimbo wa taifa ni ishara tosha ya heshima. Mahakama iliamuru wenye mamlaka ya shule wawarudishe watoto hao shuleni.

Jaji Reddy alisema hivi: “Wao [Mashahidi wa Yehova] hawaimbi wimbo wowote wa taifa, iwe ni ‘Jana Gana Mana’ wa India, ‘God save the Queen’ wa Uingereza, ‘The Star-Spangled Banner’ wa Marekani na kadhalika. . . . Hawaimbi kwa sababu ya imani yao ya kutoka moyoni na wamesadiki kwamba dini yao haiwaruhusu kushiriki tendo la ibada zaidi ya sala kwa Mungu wao Yehova.”

Kesi Iliyoweka Msingi wa Kisheria wa Haki za Kidini

Kesi ya Bijoe Emmanuel dhidi ya Jimbo la Kerala ni ya pekee sana kwa sababu inathibitisha kwamba hakuna sheria inayoweza kumlazimisha mtu yeyote akiuke dhamiri yake inayoongozwa na imani yake ya kidini. Kwa kutambua kwamba haki za msingi hazizingatiwi siku zote na kwamba mambo mengine yanafikiriwa kama vile amani ya wananchi, maadili, na afya, Mahakama ilidhibiti uwezo wa Nchi wa kuwawekea raia zake vizuizi visivyo na vigezo thabiti. Uamuzi huo ulisema hivi: “Kulazimisha kila mwanafunzi aimbe Wimbo wa Taifa licha ya kukataa kwa unyoofu kwa sababu ya dhamiri yake . . . kunapingana moja kwa moja na haki zinazotolewa na Kifungu cha 19(1)(a) na Kifungu cha 25(1) [cha Katiba ya India].”

Uamuzi huo unalinda pia uhuru wa msingi wa kikatiba wa vikundi vidogo. Mahakama iliendelea kusema hivi: “Uthibitisho wa demokrasia ya kweli ni wakati ambapo hata kile kikundi kidogo kabisa cha watu kinawakilishwa kwenye Katiba ya nchi.” Jaji Reddy aliongezea hivi: “Maoni na hisia zetu binafsi si muhimu. Ikiwa mtu anaamini kabisa na kuongozwa na dhamiri analindwa chini ya Kifungu cha 25 [cha Katiba].”

“Tamaduni yetu inafundisha kuheshimu haki za wengine; filosofia yetu inahubiri kuheshimu haki za wengine; katiba yetu inaheshimu haki za wengine; nasi tufanye vivyo hivyo.”—Jaji O. Chinnappa Reddy

Matokeo ya Uamuzi huo Katika Jamii

Kesi ya Bijoe Emmanuel dhidi ya Jimbo la Kerala ilitangazwa sana na kuzungumziwa Bungeni. Uamuzi huo ni sehemu ya somo la sheria za katiba katika vyuo vya sheria. Pia bado inajadiliwa kwa umaarufu wake katika majarida ya kisheria na magazetini kuwa msingi wa uhuru wa kidini katika India. Uamuzi huo umechangia sehemu kubwa katika kuweka msingi wa uhuru wa kidini katika jamii yenye mchanganyiko wa dini mbalimbali. Unalinda uhuru wa kusema na kujieleza wakati uhuru huo unapoingiliwa popote nchini India.

Kulinda Haki za Kikatiba Hunufaisha Watu Wote

Familia ya Emmanuel leo (safu ya nyuma kushoto hadi kulia) Binu, Bijoe, na Bindu; (safu ya mbele) V. J. Emmanuel na Lillykutty

Wakati wa kesi hiyo, familia ya Emmanuel ilikabili mnyanyaso, mkazo kutoka kwa wenye mamlaka, na hata vitisho vya kuuawa, lakini hawajuti kamwe walishikilia imani yao ya kidini. Bindu, mmoja wa mabinti hao ambaye sasa ameolewa na ana mtoto, anaeleza hivi: “Nilishangazwa sana kukutana na wakili mmoja aliyejifunza kesi yangu alipokuwa kwenye chuo cha sheria. Alieleza jinsi anavyothamini sana jitihada za kisheria za Mashahidi wa Yehova za kutetea haki za kibinadamu.”

V. J. Emmanuel anasimulia hivi: “Hivi karibuni nilikutana na Jaji K. T. Thomas, ambaye ni Jaji mstaafu wa Mahakama Kuu. Alipotambua kwamba mimi ni baba ya watoto watatu waliohusika katika kesi ya wimbo wa taifa, alinipongeza na kusema kwamba anapopata fursa ya kuzungumza kwenye mkusanyiko wa wanasheria, yeye huzungumzia kesi hiyo, kwa sababu kwa maoni yake ulikuwa ni ushindi mkubwa kwa haki za kibinadamu.”

Hata baada ya karibu miaka 30, kesi ya Bijoe Emmanuel dhidi ya Jimbo la Kerala bado ni nguzo ya uhuru wa kusema nchini India. Mashahidi wa Yehova wanafurahi kwamba walichangia katika kutetea uhuru wa kikatiba wa raia wote wa India.