Uhuru wa ibada wanaofurahia Mashahidi wa Yehova leo nchini Georgia ni tofauti kabisa na hali ilivyokuwa miaka kadhaa iliyopita. Sasa Mashahidi wa Yehova wamesajiliwa kisheria na serikali inawaruhusu kufanya ibada kwa uhuru. Lakini hali zilikuwa tofauti sana kuanzia mwaka wa 1999 hadi 2003, wakati huo serikali iliachilia Mashahidi washambuliwe na watu wenye msimamo mkali wa kidini na ilikataa kuwafungulia mashtaka watesaji hao.

Mateso ambayo Mashahidi walikabili katika kipindi hicho kigumu yalifanya wafungue kesi kadhaa katika Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu (ECHR). Moja kati ya kesi hizo, yaani, Kesi ya Tsartsidze na Wengine dhidi ya. Georgia, ilishughulikia matukio matatu ambayo yalitukia nchini Georgia katika kipindi cha mwaka wa 2000 na 2001 yaliyohusisha kushambuliwa na umati wenye jeuri, kuvurugwa kwa mikutano ya kidini, kuharibiwa kwa mali, na kutendewa vibaya kimwili na kusemwa vibaya na polisi.

Januari 17, 2017, mahakama ya Ulaya ilitoa hukumu yake kwa kesi ya Tsartsidze na ilitambua kwamba haki za Mashahidi zilikuwa zimekiukwa. Mahakama hiyo ilitambua kwamba polisi wa Georgia walikuwa wakijihusisha moja kwa moja na matukio hayo au hawakuingilia kati ili kuwalinda waathirika. Pia ilitambua kwamba mahakama za Georgia zilishindwa kuzuia jeuri waliyofanyiwa Mashahidi kwa sababu ya chuki na hazikuchunguza ukweli kihalisi.

Hukumu ya Tatu Inayoshutumu Mateso Yanayoungwa Mkono na Serikali

Hii ni hukumu ya tatu iliyotolewa na mahakama ya Ulaya dhidi ya serikali ya Georgia, katika maelezo ya kile ambacho mahakama hiyo ilikiita kuwa “jeuri ya kidini ya nchi nzima dhidi ya Mashahidi wa Yehova” ambayo ilitokea kati ya mwaka wa 1999 na 2003. Katika maamuzi yote matatu ya hukumu, mahakama hiyo ya Ulaya ilitambua kwamba Georgia ilikuwa imekiuka Mkataba wa Ulaya wa Haki za Kibinadamu kwa kushindwa kutetea uhuru wa ibada wa Mashahidi wa Yehova na kwa kuwabagua.

Mahakama ilieleza hali iliyokuwepo nchini Georgia wakati huo kama ifuatavyo: “Kupitia matendo ya mawakala wao, ambao ama walishiriki moja kwa moja kuwashambulia Mashahidi wa Yehova au kwa kukubaliana na kufumbia macho vitendo visivyozingatia sheria vilivyofanywa na watu binafsi, wenye mamlaka nchini Georgia walikosa kutoa adhabu, kitendo ambacho kilichochea mashambulizi zaidi dhidi ya Mashahidi wa Yehova katika nchi nzima.”

ECHR Yatetea Sheria na Uhuru wa Ibada

Katika mashambulizi hayo matatu yaliyochunguzwa na mahakama ya Ulaya katika kesi ya Tsartsidze, waathiriwa walitendewa isivyo haki kwa sababu ya matendo ya polisi au polisi hao waliunga mkono matukio hayo.

  • Septemba 2, 2000, katika jiji la Kutaisi, polisi walimchukua Bw. Dzamukov na kumpeleka kwenye kituo cha polisi. Wakachukua machapisho ya kidini aliyobeba na kisha wakamtesa na kumpiga. Siku iliyofuata, polisi walimshambulia Bw. Gabunia, walimpiga ngumi tumboni na kuchana machapisho ya kidini aliyobeba.

  • Oktoba 26, 2000, katika jiji la Marneuli, polisi walivuruga mikutano na kuchukua machapisho ya kidini. Walimchukua Bw. Mikirtumov, ambaye alikuwa akitoa hotuba ya kidini na Bw. Aliev, mmiliki wa nyumba ambapo mikutano ilikuwa ikifanywa, na kuwapeleka kwenye kituo cha polisi. Hatimaye polisi walimlazimisha Bw. Mikirtumov kuingia ndani ya gari na kumpeleka nje ya jiji, wakamwamuru asirudi tena jijini. Pia, walimwamuru Bw. Aliev asiruhusu tena mikutano ya Mashahidi wa Yehova ifanywe kwenye nyumba yake.

  • Machi 27, 2001, katika jiji la Rustavi, umati wenye msimamo mkali wa dini ya Othodoksi walivamia nyumba ya Bw. Gogelashvili wakati mkutano wa kidini ulikuwa ukiendelea katika nyumba hiyo. Waliwashambulia wahudhuriaji na kuwalazimisha waondoke. Kikundi hicho kilichukua machapisho ya kidini na siku iliyofuata waliyachoma hadharani karibu na soko. Polisi walikataa kuingilia kati ili kuwalinda waathiriwa.

Katika kila kisa, waathiriwa walikwenda kwenye mahakama za Georgia ili kupata msaada lakini hawakusaidiwa. Kama ilivyogunduliwa na mahakama ya Ulaya, mahakimu wa Georgia waliwapendelea polisi na wakashindwa kuchunguza uthibitisho wa waathiriwa kwa njia nzuri. Kuhusiana na mtazamo wa mahakimu wa Georgia waliposhughulikia kesi, ECHR ilitoa maelezo yafuatayo:

Kwa maoni ya Mahakama (ECHR) hali ya kuchunguza kijuujuu na kuzingatia upande mmoja wa kesi pamoja na kutegemea maofisa wa kusimamia sheria na mahakama kukataa bila kuwa na uthibitisho maelezo ya walalamikaji kuhusu matukio hayo, ni kuunga mkono vitendo vya jeuri vilivyofanywa dhidi ya walalamikaji.

Kwa sababu mahakama ya Ulaya ilitambua kwamba haki ya walalamikaji chini ya Kifungu cha 9 (uhuru wa kidini) na cha 14 (ubaguzi) cha Mkataba wa Ulaya Kuhusu Haki za Kibinadamu ulikuwa umekiukwa, iliamuru walalamikaji walipwe euro 11,000 (sawa na dola 11,840 za Marekani), pamoja na euro 10,000 (sawa na dola 10,762 za Marekani) kwa ajili ya gharama ya kuendesha kesi.

Je, Maamuzi Haya Yatatumika kwa Urusi na Azerbaijan?

Ili kuhitimisha kesi hii, ECHR ilieleza kuhusu mkataa waliofikia kwenye kesi za awali zilizowahusu Gldani na Begheluri kutoka Georgia na kesi zilizowahusu Kuznetsov na Krupko kutoka Urusi. Serikali ya Georgia imetekeleza hatua kwa hatua maamuzi yaliyotolewa awali, na sasa Mashahidi wa Yehova wanashukuru kufurahia ulinzi bora ambao unawawezesha kukusanyika pamoja na pia kuwaeleza wengine kuhusu imani yao kwa uhuru na usalama.

Mwanasheria wa kimataifa wa haki za binadamu André Carbonneau, ambaye alishiriki kusikiliza kesi nchini Georgia pamoja na kutayarisha maombi ya kufungua kesi hiyo kwenye mahakama ya Ulaya, alisema hivi: “Kwa uamuzi huu bora, mahakama ya Ulaya imeonyesha wazi kwamba haitavumilia matendo ya serikali yoyote chini ya mamlaka yake ambayo inategemeza au kuendeleza ukandamizaji wa uhuru wa ibada wa raia zake. Mashahidi wa Yehova wanashukuru kwamba serikali ya Georgia inaendelea kutekeleza maamuzi haya ya hukumu hivi kwamba wanaweza kuabudu kwa uhuru. Tunatumaini nchi nyingine katika Baraza la Ulaya, kama vile Urusi, zitazingatia hilo.”

Uamuzi huo wa karibuni wa mahakama ya Ulaya unalinda uhuru wa kukusanyika pamoja kwa ajili ya ibada na kuwaeleza majirani imani yao ya kidini kwa amani. Mashahidi wa Yehova duniani pote wanatumaini kwamba uamuzi huo wenye nguvu uliotolewa na mahakama ya Ulaya utatumika katika kesi zilizosalia dhidi ya Urusi na Azerbaijan zinazohusiana na jambo hilohilo.