Eritrea huwakamata na kuwafunga gerezani Mashahidi wa Yehova na watu wengine bila kuwashtaki au kutozingatia utaratibu wa kisheria. Wanaume na wanawake Mashahidi, kutia ndani watoto na watu waliozeeka, wanafungwa gerezani kwa sababu ya kushiriki ibada au kwa sababu zisizojulikana. Wanaume vijana wanafungwa kwa kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri.

Eritrea ilipopata uhuru mwaka wa 1993, Mashahidi wa Yehova walipoteza uhuru wao wa msingi. Rais Afewerki alifutilia mbali uraia wao kupitia Amri ya Rais iliyotolewa Oktoba 25, 1994, kwa sababu Mashahidi hawakushiriki kupiga kura ya maoni kuhusu kupata uhuru mwaka wa 1993 na pia kwa sababu walikataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri. Tangu wakati huo, vikosi vya ulinzi vya Eritrea vimewafunga gerezani, kuwatesa, na kuwadhulumu Mashahidi wa Yehova ili kuwalazimisha kukana imani yao.

Vifungo Gerezani Visivyo na Mwisho Chini ya Hali Ngumu Sana

Wanaume watatu, Paulos Eyasu, Isaac Mogos, na Negede Teklemariam, wamefungwa gerezani tangu Septemba 24, 1994 kwa kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri zao. Baadhi ya Mashahidi wamefungiwa katika makontena ya chuma na wengine katika majengo ya mawe au ya chuma yaliyofukiwa nusu ardhini. Mfungwa mmoja aitwaye Misghina Gebretinsae, mwenye umri wa miaka 62, alikufa Julai 2011 kwa sababu ya joto kali alipofungiwa mahali pa kuwaadhibia wafungwa panapoitwa “underground” (yaani, “chini ya ardhi”) katika Gereza la Kambi ya Meitir. Yohannes Haile, mwenye umri wa miaka 68, alikufa Agosti 16, 2012, baada ya kufungwa chini ya hali kama hizo kwa karibu miaka minne katika Gereza la Kambi ya Meitir. Tangu wakati huo Mashahidi wachache waliofungwa walikuwa wameachiliwa kutoka katika Gereza la Kambi ya Meitir baada ya kupata matatizo mabaya ya afya.

Visa vya Karibuni vya Kukamatwa

Oktoba 25, 2015, wanawake wawili Mashahidi wa Yehova waliwekwa chini ya ulinzi walipokutwa wakifanya utendaji wao wa kidini. Mmoja wa wanawake hao ambaye si raia wa Eritrea, aliachiliwa huru baada ya kushikiliwa kwa juma moja. Alikuwa amekuja nchini kuwatembelea jamaa zake. Mwenzake ambaye ni raia wa Eritrea mwenye umri wa miaka 53, bado yupo gerezani.

Aprili 5, 2016, Saron Gebru alianza kutumikia kifungo chake cha miezi sita gerezani baada ya kushtakiwa kwa sababu ya kuhudhuria Ukumbusho wa Kifo cha Kristo wa mwaka 2014.

Mfuatano wa Matukio

 1. Juni 15, 2017

  Jumla ya Mashahidi 53 wamefungwa gerezani.

 2. Julai 25, 2014

  Wengi wa waliokamatwa Aprili 14 waachiliwa huru, lakini 20 kati ya wale waliokamatwa Aprili 27 bado wanazuiliwa; jumla ya Mashahidi 73 wamefungwa gerezani.

 3. Aprili 27, 2014

  Mashahidi thelathini na moja hivi wakamatwa wakati wa mkutano wa kujifunza Biblia.

 4. Aprili 14, 2014

  Mashahidi zaidi ya 90 wakamatwa wakati wa sherehe ya kila mwaka ya Kuadhimisha Kifo cha Yesu.

 5. Novemba 2013

  Jumla ya Mashahidi 52 waliofungwa gerezani chini ya hali ngumu sana.

 6. Agosti 16, 2012

  Yohannes Haile, mwenye umri wa miaka 68 anakufa, akitumikia kifungo chini ya hali ngumu sana.

 7. Julai 2011

  Misghina Gebretinsae, mwenye umri wa miaka 62 anakufa, akitumikia kifungo chini ya hali ngumu sana.

 8. Juni 28, 2009

  Wenye mamlaka wavamia nyumba ya Shahidi wakati wa ibada na kuwakamata Mashahidi wote 23 waliohudhuria, kuanzia umri wa miaka 2 hadi 80. Jumla ya idadi ya Mashahidi walio gerezani yaongezeka na kufikia 69.

 9. Aprili 28, 2009

  Wafungwa wahamishwa, lakini mmoja ambaye ni Shahidi wa Yehova azuiliwa katika kituo cha polisi kwenye Gereza la Kambi ya Meitir.

 10. Julai 8, 2008

  Wenye mamlaka waanza kuvamia nyumba na mahali pa kazi na kuwakamata Mashahidi 24, wengi wao wana familia zinazowategemea.

 11. Mei 2002

  Serikali yafunga vikundi vyote vya kidini ambavyo si sehemu ya vikundi vinne vya kidini vilivyokubaliwa na serikali.

 12. Oktoba 25, 1994

  Rais atoa Amri ya kufutilia mbali uraia wa Mashahidi wa Yehova na kuwaondolea haki za kimsingi za uraia.

 13. Septemba 24, 1994

  Paulos Eyasu, Isaac Mogos, na Negede Teklemariam wafungwa bila kushtakiwa au kufikishwa mahakamani na bado wako gerezani.

 14. Miaka ya 1940

  Mwanzo wa kuwepo kwa Mashahidi wa Yehova nchini Eritrea.