Hamia kwenye habari

JUNI 14, 2016
BULGARIA

Tume ya Bulgaria Yatoa Adhabu kwa Sababu ya Ubaguzi wa Kidini

Tume ya Bulgaria Yatoa Adhabu kwa Sababu ya Ubaguzi wa Kidini

Mashahidi wa Yehova nchini Bulgaria wamepata ushindi unaotetea haki ya uhuru wa kusema na pia kumlinda mtu mmoja-mmoja na mashirika dhidi ya ubaguzi wa kidini. Tume ya Ulinzi Dhidi ya Ubaguzi nchini Bulgaria, ilibaini kwamba kituo cha televisheni cha Bulgaria kiitwacho SKAT TV na waandishi wawili wa habari wa kituo hicho walisambaza kimakusudi habari za uwongo kuhusu Mashahidi wa Yehova na kuchochea chuki dhidi yao. Tume hiyo ilihitimisha maamuzi yake kwa kusema kwamba jambo lililofanywa na SKAT TV “haliwezi kupuuzwa.”

Utangazaji Unaochochea Ubaguzi wa Kidini na Jeuri

Mara kwa mara kituo hicho cha televisheni cha Bulgaria kilikuwa kikirusha programu iliyokuwa na habari za kuwakashifu Mashahidi wa Yehova. Waandishi wa habari wa SKAT TV waliwachongea Mashahidi na kuwadanganya watazamaji waamini kwamba Mashahidi wana hatia ya makosa makubwa ya uhalifu. Programu hizo zimerushwa nchi nzima na kuwekwa kwenye Intaneti.

Pia, programu hizo zilichochea jeuri na chuki dhidi ya Mashahidi. Kipindi kilichorushwa Mei 2011 na SKAT TV kilitetea uhalali wa shambulizi lililofanywa dhidi ya Mashahidi wa Yehova na Jumba lao la Ufalme (jengo la ibada) jijini Burgas. Mashahidi walikuwa wamekusanyika ili kuadhimisha Ukumbusho wa kila mwaka wa kifo cha Yesu, wakati ambapo kundi la watu liliwavamia na kuwapiga kikatili baadhi ya wahudhuriaji. Mashahidi watano walipelekwa hospitali wakiwa wamejeruhiwa. Kipindi hicho kwenye SKAT TV kiliwachochea watu wafanye mashambulizi kama hayo, na programu nyingine zilizorushwa baada ya hapo zilidai kwamba Mashahidi wanastahili kushambuliwa. *

Baada ya kurushwa kwa matangazo hayo, Mashahidi walishambuliwa mara kwa mara na Majumba mengi ya Ufalme yakaharibiwa. Baadhi ya mikoa na manispaa hata zilitunga sheria ndogondogo za kuzuia utendaji wa Mashahidi.

Mashahidi wakiwa kwenye mkutano katika Jumba la Ufalme jijini Burgas

Tume Yawaadhibu kwa Kukiuka Sheria na Maadili

Februari 2012, Mashahidi wa Yehova walipeleka malalamiko kwenye Tume hiyo kuhusiana na programu sita zilizorushwa na kituo cha SKAT TV mwaka wa 2010 na 2011. Mashahidi walitoa hoja za kuthibitisha kwamba SKAT TV walikuwa wametumia lugha iliyoficha ukweli kuwahusu na kwamba kusambaza matangazo hayo ni kitendo cha unyanyasaji na uchochezi wa chuki dhidi yao. Pia, walithibitisha kwamba vitendo vya ubaguzi walivyofanyiwa ni kwa sababu ya programu hizo zilizoonyeshwa katika televisheni hiyo.

Januari 25, 2016, kwa kauli moja Tume iliamua kuwaunga mkono Mashahidi, na kuthibitisha kwamba kituo cha televisheni cha SKAT TV pamoja na waandishi wake wa habari waliwashambulia Mashahidi wa Yehova kwa madai ya uwongo na yasiyothibitishwa. Tume ilitambua wazi kwamba kurushwa kwa zile programu sita za televisheni hiyo kilikuwa kitendo cha ubaguzi wa kidini dhidi ya Mashahidi wa Yehova na kulionyesha wazi kwamba walipuuza kabisa viwango vya uandishi wa habari.

Ilipokuwa ikitoa adhabu, Tume ilisema kwamba “washiriki wote wa dini hii wametendewa kinyume na mapendezi yao na kinyume cha sheria, vitendo vinavyoweza kufafanuliwa kuwa unyanyasaji.” Baada ya kufafanua wazi kwamba haki ya uhuru wa kujieleza ina mipaka na inadhibitiwa ili kuzuia uhasama, Tume ilisema kwamba “vitendo vya washtakiwa katika kesi hii haviwezi kusamehewa.”

Tume ilieleza kuwa maneno ya uwongo dhidi ya Mashahidi wa Yehova ni jambo zito. Pia haikukubaliana na kitendo cha kituo hicho cha SKAT TV pamoja na waandishi wake wa habari kukataa kuwajibika kwa vitendo vyao na kwa kukataa kukubali makosa yao. Ili kuonyesha uzito wa ukiukwaji huo wa sheria, Tume iliwaamuru walipe faini kubwa kuliko ilivyo kawaida.

Hukumu Nzuri Yasahihisha Kosa

Mashahidi wanaipongeza Tume kwa kuchukua hatua dhidi ya uandishi wa habari wenye uchongezi na unaoficha ukweli. Isitoshe, kwa kuwa Mashahidi wa Yehova wamekabili hali kama hiyo kutoka kwa vyombo vingine vya habari nchini Bulgaria, uamuzi huu umekuwa onyo kwa vyombo hivyo visirushe habari za uwongo na zinazochochea chuki.

Krassimir Velev, msemaji wa Mashahidi wa Yehova nchini Bulgaria anasema hivi: “Hakuna mtu anayependa kuona habari za uwongo kumhusu zikisambazwa, hata sisi hatupendi. Kwa kuwa watu nchini Bulgaria wamesikia habari hizo za uwongo, ni muhimu kwamba sasa wasikie habari za kweli kuhusu Mashahidi wa Yehova na tunafurahi kwamba Tume imechukua hatua ili kuweka mambo sawa.”

^ fu. 5 Julai 8, 2015, SKAT TV ilirudia tena kurusha video iliyoonyesha shambulizi dhidi Mashahidi Aprili 17, 2011, wakiendeleza uchongezi wao dhidi ya Mashahidi na kuwachochea watu wawachukie.