Hamia kwenye habari

Hamia kwenye menyu ya pili

Mashahidi wa Yehova

Kiswahili

BULGARIA

Maelezo Mafupi Kuhusu Bulgaria

Maelezo Mafupi Kuhusu Bulgaria

Mashahidi wa Yehova wamekuwepo nchini Bulgaria tangu 1888. Mwaka 1938, walisajili shirika lao la kisheria, lakini usajili huo ulifutwa mwaka wa 1944 nchi hiyo ilipoanza kuwa chini ya utawala wa Kikomunisti. Mashahidi walikabili vizuizi vingi mpaka mwaka wa 1991, wakati ambapo shirika lao la kisheria Christian Association of Jehovah’s Witnesses, lilisajiliwa rasmi. Hata hivyo, mwaka wa 1994 baada ya kampeni ya kushutumu dini ambazo “si za asili” na pia sheria inayodhibiti uhuru wa dini ilipopitishwa, Mashahidi wa Yehova walipoteza usajili wao pamoja na dini nyingine. Kwa sababu hiyo, polisi waliwakamata Mashahidi, wakavuruga mikutano yao, na kuwanyang’anya machapisho yao. Mahakama nchini Bulgaria hazikutoa ulinzi wa kisheria kwa Mashahidi.

Baada ya kutumia njia zote za kisheria nchini humo, Mashahidi walipeleka mashtaka yao kwenye Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu (ECHR). Mwaka wa 1998, wa 2001, na wa 2004, ECHR iliunga mkono makubaliano yaliyofanywa kati ya Mashahidi na serikali ya Bulgaria. Baada ya makubaliano hayo serikali iliwasajili tena Mashahidi wa Yehova kuwa dini inayotambuliwa nchini humo. Pia, serikali iliunga mkono haki ya Mashahidi ya uhuru wa kuabudu, kutia ndani haki kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri, haki ya kushiriki utumishi wa badala wa kiraia, na haki ya kuwaambia wengine imani yao bila kuzuiwa.

Mashahidi wa Yehova nchini Bulgaria wanashukuru kwa uhuru wa ibada wanaofurahia na kutimiza shughuli zao za kidini bila vizuizi. Hata hivyo, baadhi ya manispaa zimezuia utendaji wa Mashahidi kwa kutumia vibaya sheria za nchi ili kukataza mahubiri yao ya hadharani au kuwanyima Mashahidi vibali vya kujenga Majumba ya Ufalme. Zaidi ya hayo, baadhi ya watu katika jamii wamewashambulia na kuwasumbua Mashahidi wa Yehova. Ingawa maofisa wa kutekeleza sheria hutoa msaada kwa kiasi fulani, hawawaadhibu washambuliaji wala hawawalindi wanaoshambuliwa. Mashahidi wanaendelea kukutana na maofisa wa Bulgaria ili kusuluhisha matatizo hayo na kesi kuhusu kibali cha kujenga Jumba la Ufalme imepelekwa kwenye Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu.