Wenye mamlaka nchini Azerbaijan wasababisha ongezeko la ubaguzi wa kidini kwa kutoza Mashahidi wa Yehova faini kubwa na kuwafunga gerezani. Wenye mamlaka wanawafungulia mashtaka ya uhalifu Mashahidi kwa kukusanyika pamoja kwa ajili ya ibada na kwa sababu ya kuzungumza na wengine kuhusu imani yao.

Utendaji wa Kidini Waonwa Kuwa Uhalifu

Desemba 5, 2014, Mashahidi wawili wa Yehova—Irina Zakharchenko, mjane mwenye umri wa miaka 55 aliye na ulemavu fulani, na Valida Jabrayilova mwenye umri wa miaka 38, ambaye anamtunza mama yake—walikuwa wakiwahubiria wakazi walio katika jengo fulani jijini Baku. Wanawake hao wawili walikuwa wakitoa bila malipo broshua Wafundishe Watoto Wako, iliyokusudiwa kuwasaidia wazazi kuwafundisha watoto wao hadithi na masomo ya Biblia. *

Mpelelezi wa polisi aliwafungulia wanawake hao shtaka la kutoa machapisho ya Biblia bila “ruhusa maalumu.” Shtaka hilo dhidi ya wanawake hao lilikuwa ni shtaka la uhalifu waliofanya wakiwa chini ya kikundi rasmi, kosa linalotozwa faini kubwa sana, kati ya dola 6,690 hadi 8,600 za Marekani * au vifungo vya miaka miwili hadi mitano gerezani.

Uchunguzi wa kesi hiyo ulipokuwa ukiendelea, mpelelezi wa polisi na Wizara ya Usalama wa Taifa (MNS) iliwaita wanawake hao tena na tena ili kuwahoji. Walipoitwa tena Februari 17, 2015 wakahojiwe na MNS, walijikuta bila kutarajia wakiwa mbele ya Mahakama ya Wilaya ya Sabail jijini Baku ili kesi yao isikilizwe.

Baada ya kuwasilisha mashtaka hayo ya uhalifu, mpelelezi wa Wizara ya Usalama wa Taifa (MNS) aliomba wanawake hao wafungwe gerezani wakingoja kusikilizwa kwa kesi yao sababu aliona kuwa wanawake hao wangerudia kosa hilo tena na “kutoroka na kujificha uchunguzi ukiendelea.” Wakili wa wanawake hao alipinga jambo hilo, akieleza kuwa kifungo hicho hakina sababu za msingi katika kisa hiki kwa sababu wanawake hao walishirikiana na serikali. Ingawa hakimu alijua kwamba wanawake hao hakuwahi kushtakiwa awali kwa kosa lolote, bado aliuita utendaji wao kuwa ni “hatari kwa umma” na kukubali ombi la mpelelezi kwa kuagiza wafungwe katika gereza linaloendeshwa na polisi wa siri kwa miezi mitatu.

Mwanasheria wa wanawake hao alikata rufani, na Februari 26, 2015, polisi waliwasafirisha wakiwa wamefungwa pingu kutoka gerezani hadi Mahakama ya Rufani ya Baku ndani ya gari lenye vioo vyeusi. Wakati wa kusikilizwa kwa kesi hiyo, hakuna uthibitisho wowote uliotolewa na mwendesha-mashtaka au mpelelezi wa MNS kutetea kwamba wafungwe gerezani. Hata hivyo, mahakama ilikataa rufani hiyo, na Bi. Zakharchenko na Bi. Jabrayilova walirudishwa gerezani.

Machi 6, 2015, vikundi viwili kutoka MNS vilipewa vibali na mahakama kukagua nyumba ya Bi. Zakharchenko na Bi. Jabrayilova, wakachukua machapisho yao ya kidini, madaftari yaliyoandikwa mambo binafsi, kompyuta, na simu ya mkononi. Machi 10, 2015, MNS, Halmashauri ya Kitaifa Kuhusu Kazi na Mashirika ya Kidini, na polisi walipata vibali vya mahakama ili kukagua Jumba la Ufalme (nyumba ya ibada) na nyumba ya mmoja wa wazee wa kutaniko. Pia, MNS imewaita Mashahidi kadhaa kutoka Baku ili wahojiwe.

Kwa sababu ya kufungwa kwa Bi. Zakharchenko na Bi. Jabrayilova, Mashahidi wa Yehova wameandika barua kuomba msaada wa Katibu Maalumu wa Umoja wa Mataifa ili kutetea uhuru wa kidini au imani na kwa kikundi kinachoshughulikia vifungo vilivyo kinyume cha sheria (Working Group on Arbitrary Detention). Wakili kutoka eneo hilo anaandaa ombi la kubadili kifungo hicho ili kiwe kifungo cha nyumbani.

Watozwa Faini Kubwa na Kufungwa kwa Kuhudhuria Ibada

Jijini Ganja, wenye mamlaka wamewatoza faini kubwa wanaohudhuria mikutano ya kidini ya Mashahidi na kuwafunga gerezani baadhi yao. Faini hizo ni kati ya dola 1,433 hadi dola 1,911 za Marekani.

Oktoba 2014, mahakama jijini Ganja ziliwafunga Mashahidi watatu na mwanamume mmoja aliyehudhuria ibada yao kwa kutolipa faini walizokuwa wametozwa kwa sababu ya kukusanyika kwa ajili ya ibada. Ingawa walikuwa wamelipa sehemu ya faini hizo, mamlaka ziliwafunga kwa siku 3 hadi 20.

Mwanamume aliyekuwa katika ibada pamoja na Mashahidi hao alisema hivi: “Dola 1,433 za Marekani ni pesa nyingi sana kwangu. . . . Niliona sipaswi kulipa faini hiyo kwa sababu sina hatia.” Wanaume wawili Mashahidi walihisi pia kwamba adhabu hiyo si ya haki na wenye mamlaka waliwatendea kama wahalifu.

Shahidi wa tatu ambaye ni mwanamke, alisema hivi: “Hakuna aliyejaribu kuelewa hali ngumu ya kifedha ya familia yangu, kwamba ninamtunza mama yangu aliye mlemavu, asiyeweza kufanya lolote bila msaada, na kwamba nilikuwa nimeanza kuilipa faini hiyo bila kushurutishwa.”

Ingawa watu hao wanne wamemaliza kutumikia vifungo vyao, mahakama bado inadai wakamilishe malipo ya faini walizotozwa. Ikiwa watashindwa kuzilipa kwa wakati uliowekwa, mahakama itaagiza wafungwe tena.

Je, Azerbaijan Itatetea Haki?

Wenye mamlaka nchini Azerbaijan wamekuwa wakitumia njia mbalimbali kuzuia utendaji wa kidini wa Mashahidi wa Yehova. Kufikia sasa, Mashahidi wa Yehova wamefungua kesi 19 dhidi ya Azerbaijan katika Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu kushughulikia ubaguzi wanaokabili. Wakisubiri matokeo, Mashahidi wa Yehova wanatumaini kwamba mamlaka za juu nchini Azerbaijan zitarekebisha ukosefu huo wa haki wa kuwafunga gerezani Bi. Zakharchenko na Bi. Jabrayilova. Azerbaijan itakaporekebisha jambo hilo na matendo mengine ya ubaguzi wa kidini itaonyesha heshima kwa raia zake, katiba yake, na kuunga mkono haki za msingi za kibinadamu.

^ fu. 4 Halmashauri ya Kitaifa Kuhusu Kazi na Mashirika ya Kidini ya Jamhuri ya Azerbaijan iliruhusu broshua hii kuingizwa nchini, iliyochapishwa na Mashahidi wa Yehova, Agosti 11, 2014.

^ fu. 5 Kwa wastani mshahara wa mwezi mmoja nchini Azerbaijan ni manats 440 (dola 420 za Marekani), kwa makadirio ya mwezi wa Agosti 2014.