Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Vifungo Visivyo vya Haki iliiomba nchi ya Azerbaijan iwaachilie Irina Zakharchenko na Valida Jabrayilova. Inaonekana kwamba Azerbaijan iliwafunga wanawake hao kinyume na sheria kwa kufanya kwa amani uhuru wao wa kidini, iliwabagua kwa sababu ya dini yao, na kushindwa kufuata taratibu za kimataifa za kuhukumu kwa haki. Maamuzi ya taasisi hiyo hayaelezi tu kuhusu kifungo cha kabla ya kusikiliza kesi cha wanawake hao; kifungo chochote kinachohusiana na shughuli zao za kidini kingekuwa kinyume cha sheria na chenye ubaguzi.

Azerbaijan ilipuuza ombi la awali la Kamati ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa la kumwachilia huru Irina. Alishindwa kwenda kusikiliza kesi Januari 7, 2016 kwa sababu alikuwa na hali mbaya ya afya. Kesi itakaposikilizwa tena, je, Hakimu Akram Gahramanov atatii sheria ya kimataifa?