Hamia kwenye habari

Hamia kwenye menyu ya pili

Mashahidi wa Yehova

Kiswahili

JUNI 11, 2015
AZERBAIJAN

Mashahidi wa Yehova Waitaka Serikali ya Azerbaijan Ikomeshe Vifungo Visivyozingatia Haki

Mashahidi wa Yehova Waitaka Serikali ya Azerbaijan Ikomeshe Vifungo Visivyozingatia Haki

Mashahidi wa Yehova wameomba mashirika ya kimataifa yaangazie kitendo cha serikali ya Azerbaijan kuwafunga isivyo haki Irina Zakharchenko na Valida Jabrayilova. Wanawake hao wawili wamefungwa tangu Februari 17, 2015, wakati mahakama ya wilaya ya Sabail ilipoamua wawekwe mahabusu kwa miezi mitatu kwa madai ya kusambaza machapisho ya kidini yaliyopigwa marufuku. Hivi karibuni mahakama hiyo imeamuru wanawake hao wafungwe kwa miezi miwili zaidi.

Irina Zakharchenko na Valida Jabrayilova

Wanawake Wenye Amani Watendewa Kama Wahalifu Hatari

Bi. Zakharchenko na Bi. Jabrayilova, walikamatwa na polisi Desemba 5, 2014, walipokuwa wakiongea na watu wanaoishi katika majengo ya ghorofa yenye nyumba za kupanga huko Baku kuhusu imani yao inayotegemea Biblia. Baada ya saa chache askari hao waliwaachilia, lakini askari wa upelelezi waliwaita tena ili kuwahoji. Bila kutarajia, Februari 17, 2015, watumishi wa Wizara ya Ulinzi wa Taifa (MNS) waliwachukua wanawake hao na kuwapeleka mahali ambapo waliendesha kesi kwa siri na kuwashtaki kuwa wahalifu. Ili kuonyesha kwamba hukumu hiyo ilikuwa ya haki, hakimu wa mahakama hiyo alidai kwamba wanawake hao ni “tishio kwa jamii.” Mara moja, MNS iliwafunga wanawake hao kwenye makao yao makuu yanayoonyeshwa katika picha hapo juu.

Tangu wakati huo, watumishi wa MNS wameendelea kupekua nyumba zao, wamechukua machapisho yao ya kidini, madaftari ambayo wameandika mambo yao ya kibinafsi, kompyuta, na simu zao za mkononi. Rufaa zote zilizokatwa kwa ajili ya wanawake hao zimekataliwa na hata mahakama imekataa kuwapa kifungo cha nje.

Kuhangaikia Afya ya Wanawake Hao

Mawakili, watu wa familia, na marafiki wanahangaikia afya ya wanawake hao wawili, ambayo wanaamini inadhoofika. Bi. Zakharchenko ana umri wa miaka 55. Pia, daktari amethibitisha kwamba ni mlemavu kutokana na kuugua ugonjwa wa baridi yabisi na majeraha aliyopata zamani kwenye mguu wake wa kulia.

Kuna mashaka mengi kuhusu hali ya kihisia ya wanawake hao. MNS imewaruhusu tu mawakili wao kuwatembelea na kuzungumza na wanawake hao. Ndugu zao wa ukoo wameruhusiwa kuwatumia mahitaji muhimu kama vile nguo, dawa, na sabuni mara moja tu kwa mwezi. Ili kuwafariji, washiriki wa familia wamejaribu kuwapelekea wanawake hao Biblia, lakini MNS imekataa wasipelekewe.

Je, Azerbaijan Itaendelea Kukandamiza Uhuru wa Ibada?

MNS imeendelea kuwachunguza Bi. Zakharchenko na Bi. Jabrayilova, kwa kuwaita na kuwahoji Mashahidi wengine 20 hivi na kupekua nyumba kumi. Kwa kuongezea, maofisa wa MNS, watumishi wa Halmashauri ya Taifa ya Kazi na Mashirika ya Dini, na askari wamefanya upekuzi kwenye Jumba la Ufalme ambapo wanawake hao huabudu.

Tangu serikali ya Azerbaijan ikatae rufaa ya wanawake hao wawili, Mashahidi wa Yehova wamepeleka maombi yao kwa Mkuu wa Tume ya Haki za Binadamu na wamewasiliana na mashirika mbalimbali ya kimataifa ili yafuatilie kitendo cha serikali ya Azerbaijan kuwafunga na kuwatendea isivyo haki Bi. Zakharchenko na Bi. Jabrayilova. Serikali ya Azerbaijan imesaini mikataba ya kimataifa ya kutekeleza haki za binadamu, na inajivunia kuwa nchi yenye uhuru wa ibada.

Mashahidi wa Yehova wanaiomba serikali ya Azerbaijan iheshimu mikataba iliyosaini ya haki za binadamu na iwaruhusu Mashahidi waabudu kwa amani. Wanaiomba serikali ya Azerbaijan ichukue hatua mara moja ya kuwaweka huru wanawake hao wasio na hatia.