Februari 8, 2017, Mahakama Kuu ya Azerbaijan ilifikia uamuzi kwamba Irina Zakharchenko na Valida Jabrayilova hawakuwa na hatia yoyote kwa kusambaza machapisho ya kidini bila ruhusa ya nchi. Hakimu Hafiz Nasibov, mwenyekiti wa Halmashauri ya Uhalifu ya Mahakama Kuu, alitangaza kwamba Mahakama hiyo haikuona uhalifu uliofanywa na wanawake hao wawili Mashahidi na hivyo ikafuta maamuzi yaliyokuwa yamefanywa na mahakama za chini.

Wakati wa kesi, mawakili wa Bi. Zakharchenko na Bi. Jabrayilova walionyesha jinsi serikali ilivyokiuka haki za msingi za kibinadamu kwa kuwatendea vibaya wanawake hao wawili Mashahidi bila sababu. Mahakama iliwaruhusu wanawake hao wawili wasimulie mambo waliyokabili kwa zaidi ya miezi 11 walipokuwa wamefungwa wakisubiri kupelekwa mahakamani na jinsi hilo lilivyowaathiri.

Jason Wise, wakili wa kimataifa wa haki za kibinadamu alisema hivi: “Tunafurahi kwamba Halmashauri ya Uhalifu ya Mahakama Kuu imefuta vifungo hivyo. Kwa Mashahidi wa Yehova nchini, ni jambo kubwa sana kwamba maamuzi ya mahakama za chini yamefutwa. Tunatumaini kwamba Mahakama ya Wilaya ya Baku Sabail itatambua pia kwamba wanawake hao wawili wana haki ya kulipwa ili kufidia hali walizokabili.”