Kwa mara ya pili tena Rashad Niftaliyev, mhudumu wa dini ya Mashahidi wa Yehova, amekuwa gerezani kwa miezi 14 kwa sababu ya kukosa kulipa faini alizotozwa kwa kushiriki mikutano ya kidini. Novemba 19, 2015, mahakama jijini Ganja, Azerbaijan, ilimhukumu Bw. Niftaliyev kifungo cha gerezani kwa siku 25 kwa kukosa kulipa faini aliyotozwa kwa sababu ya “kupanga na kufanya mikutano ya kidini.”

Faini aliyotozwa Bw. Niftaliyev sasa imefikia manat 9,450 (dola 11,375 za Marekani). Ingawa anaamini kwamba faini hiyo si haki, amekuwa akilipa kiasi kidogo hatua kwa hatua kulingana na uwezo wake.

Wahukumiwa kwa Kuhudhuria Mkutano wa Ibada

Bw. Niftaliyev alifungwa kwa mara ya pili siku ya Novemba 14, 2015 baada ya polisi kuvamia mkutano wa ibada Ganja, jiji la pili kwa ukubwa nchini Azerbaijan. Polisi walisimamisha mkutano wa ibada na kuwachukua watu 27 na kuwapeleka kwenye Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Kapaz kilichoko jijini humo. Polisi waliwashtaki watu 12 kati yao kutia ndani Bw. Niftaliyev—kwa sababu ya kuvunja sheria kwa kushiriki mkutano wa kidini. * Katika kesi hiyo iliyosikilizwa kuanzia Novemba 18 hadi 25, Mahakama ya Wilaya ya Kapaz jijini Ganja, iliwatoza watu tisa faini ya manat 2,000  (dola 1,911 za Marekani) kila mmoja kwa sababu ya kushiriki “mkutano wa kidini uliofanywa bila ruhusa maalumu.”

Novemba 19, maafisa wa mahakama walimwita Bw. Niftaliyev ili kumuuliza sababu inayomfanya alipe polepole faini tano alizotozwa katika kipindi cha miaka mitano kwa kosa lilelile. Bw. Niftaliyev alieleza jitihada zake za kulipa na hali anazokabili—kwamba hana kipato kikubwa na anamtunza mama yake ambaye ni mgonjwa—lakini afisa wa mahakama alifikisha jambo hilo mahakamani. Baada ya kusikiliza maelezo hayo, mara moja Mahakama ya Wilaya ya Kapaz jijini Ganja ilimfunga gerezani Bw. Niftaliyev. Pia, mahakama ilimtoza faini Bw. Niftaliyev kwa kushiriki mkutano wa kidini Novemba 14, na hivyo kumwongezea tena deni na kuendeleza ukosefu wa haki kwa kumwadhibu kwa sababu ya ibada yake.

Mikutano ya Ibada Yavurugwa

Novemba 14 ilikuwa ndiyo mara ya nane kwa polisi kuvamia mkutano wa Mashahidi tangu mwaka 2010. * Kwa kawaida, uvamizi wa polisi hufuata utaratibu huu: Mashahidi wanafanya mkutano kwa amani wakiwa kikundi kidogo katika nyumba ya mtu. Polisi wanaingia ndani ya nyumba hiyo bila hati ya upekuzi au amri ya mahakama na hawajitambulishi wala kueleza sababu iliyowaleta. Wanasimamisha mkutano, wanawanyang’anya watu Biblia na machapisho ya kidini, wanarekodi video ya eneo hilo, na kuwatukana na kuwatisha kwa maneno wale waliohudhuria.

Polisi huwachukua wote waliohudhuria, kutia ndani watoto na wazee, na kuwapeleka kwenye kituo cha polisi. Mahakama hupanga kusikiliza kesi baadaye siku hiyo, ingawa mahakama inaweza kuwapa washtakiwa nafasi ya kuwatafuta mawakili wao na kuwapa siku chache kwa ajili ya kuandaa hoja za kujitetea. Katika visa mbalimbali, vyombo vya habari nchini Azerbaijan vimetangaza jinsi Mashahidi walivyokamatwa na hata kuwaonyesha wakiwa wamesubiri ndani ya kituo cha polisi.

Wanapaswa Kusajiliwa Lakini Maombi Yanakataliwa Kila Mara

Kwa sababu Mashahidi jijini Ganja wameshindwa kupata usajili wa Kitaifa, watu wenye mamlaka wanawaambia kuwa mikutano yao kwa ajili ya ibada inafanywa kinyume na sheria. Mahakama ya Wilaya ya Kapaz jijini Ganja ilitumia sababu hiyo kuwatoza faini watu wote walioshiriki mkutano uliofanyika Novemba 14, wakidai kwamba “shirika la Mashahidi wa Yehova halijapata kibali rasmi kutoka kwenye mamlaka husika ili kuendesha ibada zao jijini Ganja.” *

Kinyume cha uamuzi huo, hakuna sheria nchini Azerbaijan inayoonyesha kwamba lazima uwe na kibali cha Taifa ili kukutana kwa ajili ya ibada. Kifungu cha 21 cha Sheria Kuhusu Uhuru wa Imani ya Kidini kinasema: “Ibada, . . . sherehe na desturi za ibada zinapaswa kufanywa kwa uhuru katika sehemu za ibada . . . pia kwenye vyumba vya kuishi au nyumba za raia.”

Mashahidi wa Yehova wamesajiliwa katika mji mkuu unaoitwa Baku, na wamekuwa wakipeleka maombi mbalimbali ya kusajiliwa jijini Ganja tangu mwaka wa 2010. Hata hivyo, Halmashauri ya Kitaifa Kuhusu Kazi na Mashirika ya Kidini imekuwa ikikataa maombi yao kila wakati ikidai kwamba kuna makosa fulani ya kiufundi au wakati mwingine haijibu kabisa. Maombi ya hivi karibuni ya Mashahidi jijini Ganja, yalitumwa Novemba 10, 2015, lakini bado hayajajibiwa.

Jitihada za Kuondoa Vizuizi vya Uhuru wa Kidini

Mashahidi wa Yehova wanaendelea kujaribu kukutana na wenye mamlaka nchini Azerbaijan ili wasajiliwe na kupata haki zao za kibinadamu. Hata hivyo, kwa sababu ukosefu wa haki unaoendelea, Mashahidi nchini Azerbaijan wamepeleka kesi 21 kwenye Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu katika visa ambavyo mamlaka zimeingilia haki yao ya uhuru wa kidini na uhuru wa kutangaza imani yao.

Mashahidi wa Yehova wameiomba serikali ya Azerbaijan iwape haki ambazo zimepitishwa na nchi hiyo kwa ajili ya raia wote zinazotia ndani uhuru wa ibada na kwamba iache kuwaadhibu waabudu wanyoofu kama vile Bw. Niftaliyev.

^ fu. 5 Walishutumiwa kwa kuvunja sheria katika Kifungu cha 299.0.2 cha Code of Administrative Violations, iliyokataza “kupanga na kufanya mikutano ya kidini, maandamano, na sherehe za kidini” bila ruhusa ya wenye mamlaka nchini Azerbaijan.

^ fu. 8 Pia wamewahi kuvamia maeneo ya Lankaran, Lokbatan, Mingachevir, Shamkir, na Zagatala.

^ fu. 11 Wenye mamlaka wanatumia Kifungu cha 12 cha Sheria Kuhusu Uhuru wa Imani ya Kidini, kinachosema: “Shirika lolote la kidini linaweza kuendesha shughuli zao baada ya kusajiliwa na mamlaka husika na kuwekwa kwenye orodha ya taifa ya mashirika ya kidini.” Hata hivyo, kifungu hicho kinazungumzia mashirika ya kisheria ya kidini. Kifungu hicho hakiwazuii watu kukutana kwa ajili ya ibada. Pia tazama Sheria ya Uhuru wa Kukusanyika, Kifungu cha 4, ambacho hakihusishi “sherehe za kidini.”