Hamia kwenye habari

FEBRUARI 15, 2018
ARMENIA

Jinsi Armenia Ilivyotambua Haki ya Wanaokataa Kujiunga na Jeshi kwa Sababu ya Dhamiri

Jinsi Armenia Ilivyotambua Haki ya Wanaokataa Kujiunga na Jeshi kwa Sababu ya Dhamiri

Uamuzi wa karibuni wa Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu (ECHR) ilikazia zaidi haki za vijana waliokataa kujiunga na utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri. Katika kesi ya Adyan na Wengine dhidi ya Armenia iliyofanyika Oktoba 12, 2017, Mahakama ya Ulaya iliweka vigezo vinavyopaswa kufuatwa kuhusiana na aina ya utumishi wa badala wa kiraia ambayo vijana hao wanapaswa kupewa.

Kwa miaka mingi, Mahakama ya Ulaya haikuwa na sheria hususa kuhusu haki ya wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri, na watu wengi waliteswa na kufungwa gerezani. Hata hivyo, msimamo wa mahakama hiyo ulibadilika kwenye maamuzi yake ya mwaka 2011 katika kesi iliyomhusu Bayatyan dhidi ya Armenia, ambapo ilitambua kwamba kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri ni haki ya msingi. Katika uamuzi uliofanywa karibuni zaidi kwenye kesi ya Adyan, Mahakama ya Ulaya imeeleza kwamba wale wanaokataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri wanapaswa kupewa utumishi wa badala wa kiraia ambao hauhusiani hata kidogo na masuala ya kijeshi na haupaswi kuwa kama adhabu.

Historia fupi ya wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri nchini Armenia inaonyesha jinsi maamuzi ya Mahakama ya Ulaya katika kesi zinazowahusu Bayatyan, Adyan, na wengine yalivyotokeza mabadiliko makubwa kuhusiana na jinsi serikali inavyowatendea wale wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri.

Ahadi ya Armenia, na Ilivyoshindwa Kutekeleza Programu ya Utumishi wa Badala wa Kiraia

Si utumishi wa badala bali ni adhabu. Armenia ilipojiunga na Baraza la Ulaya mwaka wa 2001, ilikuwa imekubali kutekeleza sheria inayohusu utumishi wa badala wa kiraia ambao unapatana na viwango vya Ulaya, yaani programu hiyo ya utumishi wa badala haikupaswa kuwa chini ya jeshi na haikupaswa kutolewa kama adhabu. Pia, ilikubali kuwasamehe wote wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri. * Hata hivyo, Armenia ilipokuwa ikisubiriwa kutekeleza ahadi zake, ilimwita jeshini Shahidi wa Yehova aitwaye Vahan Bayatyan, ambaye alikataa kujiunga na utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri. Mwaka wa 2002, Vahan Bayatyan alishtakiwa na akahukumiwa kifungo cha gerezani kwa sababu alikataa kujiunga na jeshi, na Armenia haikuwa na mpango wa utumishi badala wa kiraia. Mwaka wa 2003, Bw. Bayatyan alipeleka malalamiko yake kwenye Mahakama ya Ulaya, akidai kwamba Armenia ilikiuka uhuru wa dhamiri na dini ilipomwadhibu kifungo cha gerezani.

Utumishi wa badala ulio na kasoro—kisha adhabu. Mwaka wa 2004, Armenia ilitekeleza sheria ya utumishi wa badala na vijana wengi Mashahidi walikubali pendekezo la kushiriki utumishi wa badala kiraia badala ya utumishi wa kijeshi. Hata hivyo, muda mfupi baada ya kujiandikisha katika utumishi huo walitambua kwamba programu hiyo ilisimamiwa na jeshi badala ya taasisi za kiraia, hivyo baada ya kutoa taarifa kuhusu hilo, vijana hao waliamua kuacha kufanya kazi hizo. Kwa kufanya hivyo, walikamatwa na kuteswa, na baadhi yao walihukumiwa vifungo gerezani. Mei 2006, Hayk Khachatryan na Mashahidi wengine 18 ambao walikataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri walituma malalamiko yao katika Mahakama ya Ulaya, wakidai kwamba haki zao zimekiukwa kwa kufunguliwa kesi isiyo ya haki. *

Miaka inapita bila mabadiliko yoyote. Kwa miaka mingi serikali ya Armenia haikuchukua hatua yoyote ili kurekebisha sheria yake kuhusu utumishi wa badala wa kiraia. Mashahidi waliendelea kukataa utumishi huo wa badala wa kiraia uliokuwa na kasoro, na Armenia iliendelea kuwafunga gerezani—watu 317 walihukumiwa kati ya mwaka 2004 (sheria kuhusu utumishi wa badala ilipotekelezwa) na mwaka 2013 (sheria ya utumishi wa badala iliporekebishwa) na walitumikia vifungo vya kati ya miezi 24 hadi 36.

Katika kipindi hicho, Mahakama ya Ulaya ilifanya marekebisho kidogo kuhusiana na suala la utumishi wa badala. Mwaka wa 2009, ilipitia malalamiko ya Bw. Bayatyan, ambapo ilikubali kwamba kukataa kwake kujiunga na utumishi wa badala wa kiraia kunalindwa na Kifungu cha 9 cha Mkataba wa Ulaya, ambao unampatia haki ya uhuru wa dhamiri na dini. Hata hivyo, Mahakama ya Ulaya iliendelea kutegemea maamuzi iliyofanya kwa miaka mingi. Iliendelea kukubali kwamba nchi husika ndiyo inayopaswa kwanza kuamua ikiwa inatambua haki ya kukataa kujiunga utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri. Ikiwa nchi itakataa kutambua haki hiyo, Kifungu cha 9 hakiwezi kutumiwa kuwapa haki ya uhuru wale wanaoteswa kwa kukataa kujiunga na utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri. Kwa kuwa uamuzi huo haukuonyesha wazi utaratibu wa kimataifa kwa ajili ya wale wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri, mawakili wa Bw. Bayatyan walikata rufaa ya kesi hiyo na kuipeleka katika Baraka Kuu la Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu ili ichunguze upya kesi hiyo.

Kesi ya Bayatyan dhidi ya Armenia, ikisikilizwa Novemba 24, 2010 kwenye Baraza Kuu la Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu

Mabadiliko muhimu. Mabadiliko yalitokea wakati Baraza Kuu la Mahakama ya Ulaya lilipochunguza tena malalamiko ya Bw. Bayatyan. Julai 7, 2011, kwa mara ya kwanza Mahakama ya Ulaya ilieleza wazi kwamba kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri ni haki inayolindwa na Kifungu cha 9 cha Mkataba wa Ulaya. Ilieleza kwamba Mkataba “unafanya kazi” na unapotafsiriwa, inahitajika kutolewa kwa sheria ambayo “itakuwa makubaliano halisi na ya ujumla ambayo yatashughulikia matatizo ya Ulaya na maeneo mengine.” Uamuzi huo wa Baraza Kuu haukuangazia tu haki ya watu wanaokataa kujiunga na utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri katika bara la Ulaya bali pia uliipatia wajibu Armenia wa kutoa utumishi wa kweli wa badala kwa ajili ya wale wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri.

“Kukataa utumishi wa kijeshi, kunapochochewa na hisia kali isiyoweza kupatanishwa kati ya kutimiza wajibu wa kutumikia jeshini na dhamiri ya mtu au imani ya mtu ya kidini au imani nyingine, ni usadikisho au imani inayostahili kuzingatiwa, kuheshimiwa, na kupatanishwa na vigezo vilivyo katika Kifungu cha 9.”—Bayatyan dhidi ya Armenia [GC], na. 23459/03, § 110, ECHR 2011

Armenia Yarekebisha Sheria Yake ya Utumishi wa Badala wa Kiraia

Tatizo la usimamizi wa utumishi wa badala wa kiraia laendelea. Katika kiangazi cha mwaka wa 2011, Mashahidi wanne nchini Armenia, kutia ndani Artur Adyan, walihukumiwa na kufungwa gerezani kwa sababu ya kukataa kufanya utumishi wa badala wa kiraia ambao ulikuwa ukisimamiwa na jeshi. Walipeleka malalamiko kwenye Mahakama ya Ulaya, wakidai kwamba Armenia ilikuwa imekiuka haki zao—utumishi wa badala ambao umekuwa ukitolewa na Armenia tangu 2004 haukupatana na viwango vya Ulaya na ulipingana na dhamiri zao.

Tatizo la utumishi wa badala wa kiraia kusimamiwa na jeshi laendelea. Novemba 27, 2012, Mahakama ya Ulaya ilitoa uamuzi wake katika kesi ya Khachatryan na Wengine dhidi ya Armenia, ambayo ilihusisha Mashahidi 19 walioacha utumishi wa badala wa kiraia uliosimamiwa na jeshi, badala ya kusimamiwa na taasisi za kiraia. Mahakama ya Ulaya ilisema kwamba kesi na vifungo wanavyokabili Mashahidi si vya haki. Ingawa maelezo ya hukumu yalisema kwamba walalamikaji walidai kwamba programu ya utumishi wa badala wa kiraia ilisimamiwa na jeshi, Mahakama haikutoa uamuzi wake kwa kutegemea jambo hilo katika kesi hiyo ya Khachatryan.

Utumishi wa badala wa kiraia unaofaa. Kiangazi cha mwaka wa 2013, serikali ya Armenia ilirekebisha sheria yake ya utumishi wa badala wa kiraia kama ilivyokuwa imeahidi mwaka wa 2001. Kufikia Oktoba 2013, Mashahidi wengi nchini Armenia walikuwa wameachiliwa, ingawa wachache kati yao ambao vifungo vyao vilikuwa vikikaribia kwisha waliamua kuendelea kutumikia hadi mwisho wa vifungo vyao. Tangu wakati huo, wale wanaokataa kujiunga na utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri nchini Armenia walipewa utumishi wa badala wa kiraia.

Mahakama ya Ulaya Yaendeleza Kesi

Maamuzi mawili ya Mahakama ya Ulaya, yaani, ya Bayatyan na Khachatryan, yalifanya iwe wazi kwamba kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri ni haki ya msingi na inapaswa kuheshimiwa na serikali ya Armenia. Hata hivyo, Mahakama ya Ulaya ilimalizia maamuzi yake kwa kusema kwamba programu ya utumishi wa badala wa kiraia haupaswi kusimamiwa na jeshi.

Mahakama ya Ulaya ilirekebisha jambo hilo ilipotoa uamuzi wake katika kesi ya Adyan na Wengine dhidi ya Armenia Oktoba 12, 2017. Katika uamuzi wa kesi ya Adyan, Mahakama ya Ulaya ilitoa maelezo kwamba kwa kuwa haki ya kukataa utumishi wa kijeshi ililindwa, Armenia ilipaswa kuwapa utumishi wa badala wa kiraia ambao unapatana na viwango vya Umoja wa Ulaya wale wanaokataa kujiunga na utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri. Programu ya utumishi wa badala wa kiraia haikupaswa kusimamiwa na jeshi na wala hakupaswa kutolewa kama adhabu kwa wahusika. Mahakama hiyo ya Ulaya ilitaka wahusika walipwe fidia kutokana na adhabu walizovumilia kwa sababu ya kukataa programu iliyokuwa na kasoro.

“Mahakama inazingatia kwamba haki ya wale wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri inayohakikishwa chini ya Kifungu cha 9 cha Mkataba inaweza kuwa ya uwongo ikiwa Nchi inakubali kupanga na kutekeleza mfumo wake wa utumishi wa badala wa kiraia katika njia ambayo inashindwa kuutoa – ama kisheria au kwa matendo – kama mbadala wa utumishi wa kijeshi ambao ni wa kiraia kabisa bila kizuizi au adhabu kwa mhusika.”—Adyan na Wengine dhidi ya Armenia, na. 75604/11, § 67, ECHR 2017

Utatuzi wa tatizo

Kufikia Januari 2018, Mashahidi 161 nchini Armenia walikuwa wamemaliza utumishi wao wa badala wa kiraia, na 105 wamejiandikisha hivi karibuni katika programu hiyo. Mashahidi na wenye mamlaka wanaona programu hii ya utumishi wa badala wa kiraia kuwa unapendeza kutokana na mafanikio yake. Unasaidia kutimiza mahitaji halisi katika jamii na unakubaliwa na wanaume wote wanaoomba utumishi wa badala kwa ajili ya kulitumikia taifa. Pia, umeondoa tatizo la haki za kibinadamu ambalo awali lilikuwepo nchini Armenia.

André Carbonneau, mmoja wa wanasheria aliyewawakilisha Mashahidi nchini Armenia, aliipongeza serikali kwa kusuluhisha tatizo hilo. Alisema hivi: “Tunapochunguza maamuzi ya Mahakama ya Ulaya dhidi ya Armenia, tumeona maendeleo kuhusiana na tatizo hili tangu wakati wa kesi ya Bayatyan ya mwaka 2011. Maamuzi ya kesi ya Khachatryan na Adyan yalifungua njia ya kuhakikisha kwamba utumishi wa badala wa kiraia hausimamiwi kabisa na jeshi. Tunatumaini kwamba nchi nyingine ambazo hazina utumishi wa badala unaofaa watajifunza kutokana na mafanikio ya Armenia ya kutekeleza programu hii ya utumishi wa badala wa kiraia ambao unakubalika kwa wale wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri na pia wenye manufaa kwa jamii.”

Baadhi ya Nchi Ambazo Utumishi wa Kijeshi Ni wa Lazima Lakini Hazina Utumishi wa Badala wa Kiraia Unaofaa

 

Hakuna Utumishi wa Kiraia

Utumishi wa Kiraia Ni Kama Adhabu

Utumishi wa Kiraia Haujatekelezwa

Azerbaijan

 

 

X

Belarus

 

X

 

Eritrea

X

 

 

Lithuania

X *

 

 

Singapore

X

 

 

Korea Kusini

X

 

 

Tajikistan

 

 

X

Uturuki

X

 

 

Turkmenistan

X

 

 

Mfululizo wa Matukio

 1. Oktoba 12, 2017

  Mahakama ya Ulaya yatoa uamuzi wa kesi ya Adyan na Wengine dhidi ya Armenia

 2. Januari 2014

  Mashahidi wa kwanza kuandikishwa kwenye programu mpya ya utumishi wa badala wa kiraia waanza kufanya kazi walizopangiwa

 3. Novemba 12, 2013

  Kwa mara ya kwanza baada ya miaka 20 kupita, hakuna hata Shahidi mmoja aliyekuwa amefungwa gerezani kwa kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri

 4. Juni 8, 2013

  Armenia yakubali kufanya marekebisho ya Sheria kuhusu utumishi wa badala wa kiraia, ambayo ilianza kutekelezwa Oktoba 2013

 5. Novemba 27, 2012

  Mahakama ya Ulaya yatoa uamuzi wa kesi ya Khachatryan na Wengine dhidi ya Armenia

 6. Januari 10, 2012

  Mahakama ya Ulaya yachunguza kesi ya Bayatyan inaposhughulikia kesi za Bukharatyan dhidi ya Armenia na Tsaturyan dhidi ya Armenia, na kugundua kwamba Armenia ilikiuka Kifungu cha 9 ilipowafunga Mashahidi

 7. Julai 7, 2011

  Baraza Kuu la Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu lagundua ukiukwaji wa haki ya uhuru wa dhamiri (Kifungu cha 9 cha Mkataba wa Ulaya), kulinda haki ya wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri katika uamuzi wa 16-1 wa kesi ya Bayatyan dhidi ya Armenia

 8. Oktoba 27, 2009

  Mahakama ya Ulaya yatoa uamuzi wa kesi ya Bayatyan dhidi ya Armenia, ikisema kwamba Kifungu cha 9 cha Mkataba wa Ulaya haiwezi kutumika kwa wale wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri; rufaa ya kesi yapelekwa kwenye Baraza Kuu la Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu

 9. 2004

  Armenia yatekeleza sheria ya utumishi wa badala wa kiraia lakini ukisimamiwa na jeshi

 10. 2001

  Armenia yaahidi kutekeleza sheria ya utumishi wa badala wa kiraia

^ fu. 6 Mapendekezo Na. 221 (2000) ya Bunge la Umoja wa Ulaya ilieleza kwamba Armenia ilikubaliwa kuwa mwanachama wa Umoja wa ulaya kwa vigezo kwamba “Armenia itakubali kuheshimu masharti yafuatayo: . . . Kutekeleza, ndani ya miaka mitatu, sheria ya utumishi wa badala wa kiraia ambao unapatana na viwango vya Ulaya, na wakati huohuo, kuwaomba msamaha wale wote waliokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri ambao iliwafunga gerezani, au uliwapa utumishi ambao ulikuwa katika mfumo wa adhabu, na badala yake, wakati sheria itakapoanza kutekelezwa, waruhusiwe kufanya utumishi ambao hauhusiani kabisa na mambo ya kijeshi au utumishi wa badala wa kiraia.”

^ fu. 7 Mateso na vifungo ambavyo Armenia iliwafanyia Mashahidi 19 vilikuwa si vya haki kwa sababu walipowakamata mwaka wa 2005, hakukuwa na sheria ya iliyoundwa nchini Armenia wakati huo iliyoonyesha kwamba kukataa utumishi wa badala ni uhalifu.

^ fu. 39 Utumishi wa badala wa ulinzi wa taifa nchini Lithuania unasimamiwa na jeshi.