Hamia kwenye habari

Kushoto hadi kulia: Picha ya Ndugu Roman Markin na Ndugu Viktor Trofimiv, kabla ya kuwekwa mahabusu

JANUARI 17, 2020
URUSI

Ndugu Markin na Ndugu Trofimov Wanaweza Kufungwa Miaka Sita na Nusu Gerezani

Hukumu ya kesi dhidi ya Ndugu Markin na Ndugu Trofimov itatolewa Januari 22, 2020. Mwendesha mashtaka ameiomba mahakama iwahukumu kipindi kisichozidi miaka sita na nusu gerezani.

Mnyanyaso huu dhidi ya ndugu zetu ulianza Aprili 18,2018, polisi waliofunika nyuso zao na kubeba silaha walipovamia nyumba zao jijini Polyarny, Urusi. Polisi walifika katika nyumba ya Ndugu Markin usiku sana na kuvunja mlango wake. Huku wakimtisha Ndugu Markin kwa bunduki, na kumlazimisha alale sakafuni mpaka watakapomaliza msako katika nyumba yake. Binti yake mwenye umri wa miaka 16, aliyekuwepo pia wakati msako ulipokuwa ukiendelea, naye alilala chini na kufunika kichwa chake kwa mikono yake.

Nyumba nyingine nne za Mashahidi wa Yehova jijini Polyarny zilivamiwa pia usiku huo. Polisi hao waliwapeleka zaidi ya ndugu na dada kumi na wawili kwenye kituo cha polisi ili kuhojiwa. Hatimaye, Mahakama ya Wilaya ya Polyarny, iliyo huko Murmansk iliamua kuwaweka mahabusu Ndugu Markin na Ndugu Trofimov. Walikaa mahabusu karibu miezi sita kisha wakapewa kifungo cha nyumbani cha miezi minne. Februari 7, 2019, mahakama iliwaachilia kutoka katika kifungo cha nyumbani. Ingawa kwa sasa wanaweza kutoka nyumbani, bado hawana uhuru wa kutosha wa kusafiri au kuwasiliana na watu wengine mpaka hukumu yao itolewe na mahakama.

Karibu Mashahidi 300 wanakabiliwa na mashtaka ya makosa ya uhalifu nchini Urusi. Tunasali kwamba wote waendelee kuwa jasiri na imara moyoni, wakiwa na uhakika kwamba hakuna kitu chochote kitakachoweza kuwatenganisha na upendo wa Mungu.—Waroma 8:38, 39.