Siku tisa tu baada ya Dennis Christensen kuhukumiwa isivyo haki katika mahakama ya Urusi, angalau Mashahidi saba wa Yehova waliteswa kimwili. Walipigwa kwa umeme, walifanywa washindwe kupumua, na wakapigwa na wachunguzi Warusi katika jiji la Surgut lililoko magharibi ya Siberia. Walipowatesa ndugu zetu, maofisa hao walitaka kujua mahali wanapokutania na majina ya Mashahidi wengine.

Tukio hilo lilianza wenye mamlaka walipovamia eneo la Surgut mapema asubuhi ya Februari 15, 2019. Baada ya kuwakamata Mashahidi na kuwapeleka kwenye ofisi za Kamati ya Uchunguzi, wenye mamlaka walianza kuwahoji ndugu zetu, ambao walikataa kutoa habari kuhusu waabudu wenzao. Baada ya mwakilishi pekee wa kisheria aliyekuwepo kuondoka, ndugu wanaripoti kwamba yafuatayo yalitukia: walivishwa mifuko kichwani ambayo ilifungwa, mikono yao ilifungwa mgongoni, na wakapigwa. Baada ya kuwavua Mashahidi nguo zote na kuwamwagilia maji mengi, walipigwa na umeme kupitia bunduki za kutoa umeme. Waliteswa hivyo kwa saa mbili hivi.

Mashahidi angalau watatu bado wamefungwa gerezani. Wale walioachiliwa walienda hospitalini kwa sababu ya majeraha waliyopata na wametuma malalamiko kwenye mashirika yanayosimamia.

Pia, baada ya nyumba za Mashahidi kupekuliwa, wenye mamlaka nchini Urusi walifungua kesi za uhalifu dhidi ya Mashahidi 19 kwa kile wanachodai kuwa “kushiriki utendaji wenye msimamo mkali” na “kupanga utendaji wa shirika lenye msimamo mkali.”

Kulingana na Sheria ya Uhalifu ya Urusi, kutumia mamlaka vibaya kwa kadiri hiyo kunaweza kuadhibiwa. Pia, Serikali ya Urusi inapaswa kutii sheria zilizowekwa na mashirika kadhaa ya kimataifa yanayowalinda watu wasiteswe. Hivyo, tutatumia njia zote za kisheria, nchini Urusi na za kimataifa, kupinga uhalifu huu.

Kwa vyovyote vile, tunajua kwamba Yehova ameona mateso ya ndugu zetu nchini Urusi, naye atatenda akiwa “msaidizi. . . na mwokozi” wao.—Zaburi 70:5.