Hamia kwenye habari

Baadhi ya ndugu na dada zaidi ya 330 katika nchi ya Urusi na Crimea ambao wamewahi kufungwa gerezani tangu hukumu ya Mahakama Kuu ya Urusi ilipotolewa mwaka 2017

JUNI 8, 2022
URUSI

Mahakama ya Ulaya Yatoa Hukumu Muhimu Inayowaunga Mkono Mashahidi wa Yehova Dhidi ya Urusi

Mahakama ya Ulaya Yatoa Hukumu Muhimu Inayowaunga Mkono Mashahidi wa Yehova Dhidi ya Urusi

Juni 7, 2022, Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu ilitoa hukumu a muhimu inayowaunga mkono Mashahidi wa Yehova kwa sababu ya mateso wanayokabili nchini Urusi. Mahakama hiyo ilitangaza kwamba nchi ya Urusi iliwapiga marufuku Mashahidi wa Yehova kinyume na sheria mwaka 2017 na kwamba nchi hiyo ilitenda kinyume na sheria kwa kupiga marufuku tovuti ya jw.org na machapisho. Nchi ya Urusi imeamuriwa ifute kesi zote zinazoendelea dhidi ya ndugu na dada zetu na iwaachilie huru wale wote walio gerezani. Imeamuriwa pia irudishe majengo yote iliyokuwa imetaifisha au ilipe euro 59,617,458 (au dola 63,684,978 za Marekani) kama fidia ya majengo hayo. Pia, nchi hiyo imeamuriwa iwalipe watu waliopeleka malalamiko yao, euro 3,447,250 (au dola 3,682,445 za Marekani) kama fidia.

Eneo la ofisi ya tawi lililotaifishwa na serikali ya Urusi lililo nje ya jiji la St. Petersburg, lenye majengo 14 kwenye eneo lenye ukubwa wa zaidi ya mita za mraba 100,000

Hukumu hiyo imetolewa baada ya kuchunguza kesi 20 zilizofunguliwa kati ya mwaka 2010 hadi 2019, kulikuwa na malalamiko zaidi ya 1,400 yaliyotoka kwa Mashahidi mbalimbali na mashirika ya kisheria. Hata hivyo, hukumu hiyo iliyotolewa na Mahakama ya Ulaya itawalinda watu wengi zaidi ya wale waliotuma malalamiko. Inasema hivi: “[Urusi] lazima isimamishe kesi zote zinazoendelea mahakamani dhidi ya Mashahidi wa Yehova . . . na iwaachilie huru Mashahidi wote wa Yehova ambao wamekuwa wakinyimwa uhuru.” (Italiki ni zetu.) Hukumu hiyo inawatetea ndugu na dada zetu wote, iwe wanaishi nchini Urusi au la, kwa kuwa wanatambulika kisheria kama raia wanaoheshimu sheria na wamekuwa wakiteswa na kufungwa gerezani isivyo haki.

Katika hukumu hiyo, Mahakama ya Ulaya imepinga kabisa madai ya Urusi ya kwamba matendo yetu, imani yetu, machapisho yetu, na tovuti yetu ni yenye msimamo mkali. Kwa mfano, ona sehemu mbalimbali kutoka kwenye hukumu hiyo:

  • Matendo: Mahakama ya Ulaya imerudia tena na tena kwamba mahakama za Urusi “hazina uthibitisho wowote unaoonyesha kwamba watu waliotuma malalamiko walitumia maneno fulani, au walifanya jambo fulani linalochochewa na chuki, ukatili au ubaguzi.”(§271)

  • Imani ya kwamba Mashahidi wa Yehova wana kweli: “Mtu anapojaribu kuwasadikisha wengine kwamba imani yake ndiyo bora kwa njia ya amani na kumchochea mwingine aache ‘dini za uwongo’ ili ajiunge na ‘dini ya kweli’ ni njia inayotambulika kisheria ya kutumia uhuru wa kidini na uhuru wa kusema.”(§156)

  • Kutiwa damu mishipani: “Mtu ana uhuru wa kukataa kutiwa damu mishipani kwa sababu mshiriki yeyote katika jamii ana haki ya kujifanyia maamuzi kuhusiana na afya yake mwenyewe, haki ambayo inalindwa na Mkataba wetu na hata sheria ya Urusi.” (§165)

  • Kukataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri: “Mtu anapokataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri nchini Urusi hajavunja sheria yoyote ya nchi hiyo.” (§169)

  • Machapisho yetu: “Utendaji wa kidini na machapisho ya watu waliotuma malalamiko ni ya amani, yanapatana na mafundisho yao ambayo yanapinga ukatili.” (§157)

  • JW.ORG: Mahakama ya Ulaya ilitathmini ujumbe ulio katika tovuti ya jw.org na kusema kwamba hauna msimamo mkali. Ikiwa wenye mamlaka hawakupendezwa na ujumbe fulani katika tovuti hiyo, walipaswa kuliomba shirika hilo liondoe sehemu hizo badala ya kupiga marufuku tovuti hiyo. (§231 na §232)

Hukumu hiyo imewakosoa wenye mamlaka nchini Urusi na kuthibitisha kwamba walitenda kwa ubaguzi na “hawakuwa wanyoofu.” (§187) Kwa mfano, ilitaja pia mambo haya ambayo Mahakama ya Ulaya ilipata katika utafiti wake:

  • “Wenye mamlaka nchini Urusi walishurutisha mashirika yote ya kidini ya Mashahidi wa Yehova yafungwe si kwa sababu ya kutekeleza sheria yoyote nchini bali utafiti umeonyesha kwamba sababu yao ni chuki walio nayo dhidi ya imani ya kidini ya Mashahidi wa Yehova. Kusudi lao lilikuwa kuwashinikiza Mashahidi wa Yehova waache dini hiyo na kuwazuia wengine wasijiunge na dini hiyo.” (§254)

  • Wenye mamlaka nchini Urusi “walipuuza utaratibu” unaopaswa kufuatwa kisheria kama katika pindi ambapo Mahakama Kuu ya Urusi ilipiga marufuku machapisho kwa kutegemea ripoti zilizowasilishwa na maofisa wa polisi na waendesha-mashtaka za wataalamu wenye ubaguzi badala ya kuchunguza machapisho yenyewe. (§203)

  • Sheria ya nchi ya Urusi dhidi ya watu wenye msimamo mkali ilirekebishwa kwa utaalamu na maana ya sheria hiyo ikapanuliwa hivi kwamba wenye mamlaka waliweza kuitumia dhidi ya Mashahidi wa Yehova. (§272)

Bado haijajulikana hukumu hii ya Mahakama ya Ulaya italeta matokeo gani nchini Urusi. Kimsingi, tumaini letu si katika mamlaka za wanadamu, bali kihalisi, sisi “tunamtarajia Yehova” kwa kuwa “Yeye ni msaidizi wetu na ngao yetu.”​—Zaburi 33:20.