Hamia kwenye habari

MEI 23, 2019
URUSI

Mahakama ya Rufaa Yashikilia Uamuzi Wake wa Kumfunga Gerezani Dennis Christensen

Mei 23, 2019, jopo la mahakimu watatu wa Mahakama ya Mkoa wa Oryol lilikataa kumweka Dennis Christensen huru na likaamua afungwe kwa miaka sita kama alivyokuwa amehukumiwa hapo awali. Karibu ndugu na dada 80 hivi walifika mahakamani ili kusikiliza kesi hiyo. Maofisa kutoka Australia na Denmark walihudhuria pia. Na uamuzi wa kesi hii umekuwa ukitangazwa kwenye vituo vya habari vya kimataifa.

Kwa miezi mitatu tangu Ndugu Christensen alipohukumiwa Februari, nyumba 115 zimevamiwa na kesi za jinai dhidi ya Mashahidi wa Yehova zimeongezeka kwa mara tatu zaidi ikilinganishwa na miezi mitatu iliyotangulia.

Tunasali kwa ajili ya Ndugu Christensen na pia waamini wenzetu wote nchini Urusi. Tuna uhakika kwamba Yehova “yuko karibu na wote wanaomwitia” na ataendelea kuwasaidia ndugu zetu wabaki waaminifu licha ya kuteswa.—Zaburi 145:18.