Hamia kwenye habari

OKTOBA 3, 2017
HABARI ZA ULIMWENGUNI POTE

Hali Baada ya Kimbunga Irma

Hali Baada ya Kimbunga Irma

NEW YORK—Ofisi za tawi za Barbados, Jamhuri ya Dominika, Ufaransa, na Marekani zimetuma ripoti zifuatazo kuhusu hali ya akina ndugu baada ya Kimbunga Irma:

Maeneo yaliyoathiriwa katika eneo la ofisi ya tawi ya Barbados ni Anguilla, Antigua na Barbuda, Montserrat, Saba, St. Eustatius, St. Kitts na Nevis, na St. Maarten (eneo linalomilikiwa na Uholanzi). Maeneo ya Barbuda na St. Maarten yameathiriwa sana.

Barbuda ni kisiwa kidogo chenye watu 1,800 hivi. Kwa kuwa huduma nyingi na nyumba karibu zote ziliharibiwa, eneo hilo limetajwa kuwa eneo la majanga na hali ya dharura imetangazwa. Tumethibitisha kwamba wahubiri wote 11 wamehamishwa bila matatizo kwenda kisiwa cha karibu cha Antigua, ambako Halmashauri ya Kutoa Msaada (DRC) inawapatia mahitaji yao. Hakuna aliyejeruhiwa kati yao.

Wahubiri 700 hivi wanaishi katika kisiwa cha St. Martin (eneo linalomilikiwa na Uholanzi na Ufaransa). Dada mmoja alijeruhiwa. Wajumbe kadhaa, kutia ndani washiriki wa ofisi za tawi za Barbados na Ufaransa na vilevile wataalamu wa kitiba, walitumwa eneo la St. Martin kuwasaidia akina ndugu.

Maeneo chini ya ofisi ya tawi ya Ufaransa yaliyoathiriwa ni Guadeloupe, Martinique, St. Barthelemy, na St. Martin (eneo la Ufaransa). Hakuna ndugu yeyote aliyejeruhiwa au kufa huko Guadeloupe au Martinique.

Kisiwa cha St. Barthelemy (jina la Kifaransa la St. Barts) kiliharibiwa, na haiwezekani kuwasiliana na wahubiri kisiwani humo. Hata hivyo, ofisi ya tawi ilipata habari kutoka kwa mwangalizi wa mzunguko wa kisiwa hicho kwamba wahubiri wote 30 wako salama, lakini Jumba la Ufalme limeathiriwa kidogo. DRC ilianzishwa ili kusimamia kazi ya kuwasambazia akina ndugu katika maeneo ya St. Barthelemy na St. Martin maji, chakula, na misaada mingine kutoka visiwa vya karibu vya Guadeloupe na Martinique.

Misaada ikitayarishwa kwa ajili ya kutumwa kwenye Jumba la Kusanyiko nchini Guadeloupe.

Eneo lililoathiriwa katika Jamhuri ya Dominika. Halmashauri ya Tawi imeanzisha halmashauri tano za kudumu za kutoa msaada (DRC) ili ziwatunze wahubiri 38,000 wa nchi hiyo. Siku kadhaa kabla ya Kimbunga Irma, kupitia mwongozo kutoka kwa waangalizi wa mzunguko, wazee waliwatembelea wahubiri wote ili kuhakikisha kwamba kila mmoja alichukua hatua za kujitayarisha kwa ajili ya janga hilo. Katika maeneo yanayoathiriwa na mafuriko kwenye pwani ya kaskazini, wazee waliwahamisha wahubiri 1,273 hadi maeneo salama zaidi na wahubiri 2,068 ambao waliishi katika nyumba ambazo hazikuwa imara sana waliombwa kutafuta makao katika Majumba ya Ufalme au waishi na familia nyingine za Mashahidi walio na nyumba imara zaidi.

Majumba ya Ufalme kadhaa yaliyojengwa hivi karibuni yaliathiriwa kidogo. Nyumba za familia tano za Mashahidi ziliharibiwa. Nyumba hizo zinarekebishwa na makutaniko au na halmashauri ya DRC. Hakuna ndugu aliyejeruhiwa au kufa.

Maeneo ya ofisi ya tawi ya Marekani yaliyoathiriwa ni Bahamas, Florida, Georgia, Puerto Riko, Visiwa vya Turks na Caicos, Visiwa vya Virgin vya Uingereza na Marekani. Tulikuwa tumeeleza hapo awali kwamba ndugu mmoja na dada mmoja walikufa. Hakuna ndugu wengine waliokufa, lakini tumepata habari kwamba ndugu 6 wamejeruhiwa na ndugu zaidi ya 3,000 wamepoteza makao. Ndugu wengi katika maeneo ya Florida na Georgia wamewakaribisha akina ndugu kwenye nyumba zao.

Katika eneo la Florida, wale walio katika Ofisi ya Utafsiri (RTO) ya Fort Lauderdale walihamishiwa kwenye Jumba la Makusanyiko la West Palm Beach, ambako walikaa kwa siku kadhaa. Ofisi za RTO zimeharibiwa na maji kwa kiasi fulani, na majengo ya makao yalikosa umeme na Intaneti kwa siku kadhaa. Sasa mifumo hiyo inafanya kazi tena, na wamerudia hali ya kawaida.

Katika majengo ya shule huko Palm Coast, Florida, wanafunzi wote waliokuja kuhudhuria Shule ya Waangalizi Wanaosafiri na Wake Zao walihamishwa, pamoja na madarasa matatu ya Shule ya Waeneza Injili. Kikundi kidogo cha watu 20 hivi walibaki kwenye majengo hayo bila matatizo. Majengo hayo hayakuathiriwa sana ingawa umeme ulipotea.

Misaada imekusanywa katika Jumba la Kusanyiko la Caguas nchini Puerto Riko.

Dawati la Kutoa Misaada katika Idara ya Utumishi na Idara ya Usanifu-Majengo na Ujenzi wanaelekeza kazi ya kutoa msaada ili kuhakikisha kwamba ndugu zetu wanapata msaada kwa njia salama na kwa wakati.

Vituo vya Kutoa Msaada vimeanzishwa nchini Marekani ili kuandaa chakula na maji kwa walioathiriwa katika eneo hilo. Pia, halmashauri ya DRC nchini Puerto Riko inaandaa msaada kwa akina ndugu visiwani.

Katika eneo la Karibea, nyumba 61 hivi zinahitaji kufanyiwa marekebisho madogo na nyumba 55 zimeharibiwa. Pia, majumba mawili ya Ufalme yameharibiwa.

Mafuriko nje ya Jumba la Ufalme huko Turks na Caicos.

Ndugu kutoka ofisi ya tawi na kutoka makao makuu wamesafiri kwenda Florida na kwenda kwenye visiwa kuwasaidia akina ndugu. Bado madhara kamili hayajajulikana.

Tunawafikiria na kusali kwa ajili ya wale walioathiriwa na Kimbunga Irma na wale wote wanaoshughulikia kutoa msaada wanapoandaa msaada na faraja.—Waroma 15:5; 2 Wakorintho 1:3, 4, 7; 8:14.

Wanahabari Wanaweza Kuwasiliana na:

David A. Semonian, Ofisi ya Habari za Umma, simu +1-845-524-3000

Barbados: John Medford, simu +1-246-438-0655

Jamhuri ya Dominika: Josué Féliz, simu +1-809-595-4007

Ufaransa: Guy Canonici, simu +33-2-32-25-55-55