Hamia kwenye habari

Picha ya Tufani Idai ilivyopiga mji wa Beira, Mozambique

MACHI 27, 2019
HABARI ZA ULIMWENGUNI POTE

Tufani Idai Yapiga Eneo la Kusini Mashariki ya Afrika

Alhamisi Machi 14, 2019, Msumbiji ilikumbwa na Tufani Idai na ikasababisha uharibifu katika maeneo ya Malawi na Zimbabwe pia. Dhoruba hiyo inahesabiwa kuwa dhoruba kali zaidi kupiga Kizio cha Kusini, na iliharibu barabara na majengo, na kuathiri maisha ya watu zaidi ya milioni 2.6. Imethibitishwa kwamba watu zaidi ya 200 wamekufa kufikia sasa. Inasikitisha kwamba miongoni mwa watu waliokufa, kulikuwa na dada zetu wawili, na watoto wawili ambao hawajabatizwa nchini Msumbiji. Na nchini Zimbabwe ndugu yetu mmoja mwenye umri wa miaka 14 alikufa, nyumba yao iliposombwa na maporomoko ya ardhi.

Jumba la Ufalme la Inhamízua Msumbiji, ambalo limeharibiwa na Tufani Idai

Tumepata taarifa kutoka ofisi ya tawi ya Msumbiji kwamba nyumba za ndugu na dada zetu pamoja na Majumba ya Ufalme yameharibiwa kwa kiwango fulani au hata kabisa. Ofisi ya tawi ya Zimbabwe imetutaarifu kwamba nyumba 15 za ndugu zetu pamoja na Majumba ya Ufalme mawili yameharibiwa na tufani hiyo. Ofisi ya tawi ya Malawi imetujulisha kwamba nyumba 764 za ndugu zetu ziliharibiwa kabisa na nyumba 201 ziliharibiwa kwa kiwango fulani. Majumba ya Ufalme mawili pia yaliharibiwa. Hivyo, Halmashauri za Kutoa Misaada zimeundwa ili kushughulikia mahitaji yao, mbili nchini Msumbiji, na nne nchini Malawi.

Matawi makubwa ya mti yakitegemeza paa za nyumba za ndugu wawili baada ya kuta za nyumba zao kuporomoka.

Tunawahurumia sana ndugu na dada zetu walioathiriwa na janga hilo la asili. Tunasali kwamba wahubiri wote walioathiriwa waendelee kumtegemea Yehova ili awape amani wanayohitaji sana.—Waroma 15:13.